loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utalii wa jiolojia ulivyoipa hadhi nyingine Hifadhi ya Ngorongoro kutoka UNESCO

MEI 18- 23, 2020, Tanzania ilitarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Hifadhi za Urithi wa Jiolojia barani Afrika.

Kwa mujibu wa Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk Freddy Manongi, mkutano huo uliahirishwa kutokana na kuwepo kwa janga la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Mkutano huo ambao ungefanyika jijini Arusha, ulilenga kujadili mada mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa UNESCO Global Geopark zilizofanikiwa katika mabara yote duniani zikiwamo zenye uzoefu wa kutambua vivutio vya kijiolojia, kuvihifadhi na kuvifanya rasilimali za kiutalii kama moja ya bidhaa mpya ya utalii unaohusiana na miamba (jiolojia).

Ikumbukwe kuwa, Hifadhi ya Ngorongoro inapatikana Kaskazini mwa Tanzania katika Mkoa wa Arusha. Ina ukubwa wa kilomita za mraba 8, 292. Eneo la hifadhi limesheheni vivutio mbalimbali vya asili na vya kiutamaduni.

Chanzo kimoja kimeandika: “Baadhi ya vivutio hivyo ni pamoja na Kreta ya Ngorongoro yenye mkusanyiko mkubwa wa wanyama pori kuliko sehemu nyingine yoyote duniani. Ndani ya Kreta ya Ngorongoro, kuna faru weusi wanaoonekana kwa urahisi zaidi katika Hifadhi ya Ngorongoro kuliko sehemu nyingine.”

Uchunguzi wa kihabari umebaini kuwa, Bonde la Ngorongoro ni sehemu pekee duniani ambapo mtu anaweza kuwaona wanyama wakubwa watano duniani ndani ya muda mfupi. Wanyama hawa ni pamoja na nyati, simba, chui, faru na tembo.

Aidha, imebainika kuwa maeneo mawili ya Laetoli na Bonde la Oldupai yenye umuhimu mkubwa duniani katika ikolojia na mambo ya kale yanapatikana ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro nchini Tanzania.

Dk Manongi anayataja maeneo hayo muhimu ya kihistoria kuwa ni Laetoli ambapo ni maarufu kwa kugundulika kwa nyayo za zamadamu zinazosemekana kuwa na umri wa miaka milioni 3.6 iliyopita na sehemu ulipofanyika ugunduzi wa fuvu la mtu wa kale zaidi duniani yaani, Bonde la Oldupai maarufu kama Olduvai Gorge.

Kamishna Manongi anasema: “Mkutano huo ulilenga kutoa mafunzo, kubadilishana uzoefu pamoja na kuchochea uendeshaji wa hifadhi wa maeneo ya urithi wa jiolojia yatakayokuwa kivutio kipya cha kuongeza utalii nchini.”

“Unajua Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro tumeboresha rasilimali mbalimbali maana hata duniani kote, ni vigumu kupata watu wanaishi katika hifadhi wakiendesha shughuli mbalimbali na mila zao… Tunazo rasilimali na vivutio vingi ambavyo vimepewa hadhi ya urithi wa kidunia.”

“… Ndiyo maana tumepewa hadhi ya kuwa ‘Geopark’ na UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni) tukiwa nchi ya pili barani Afrika tukitanguliwa na Morocco na ya kwanza katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hadhi hii imetolewa kudunia na UNESCO…,” anasema Manongi. Anaongeza: “Hii inaonekana dhahiri na dunia kutukubali kwa viwango tulivyofikia, tunastahili kupata hadhi hiyo baada ya kukaguliwa na kukidhi vigezo. UNESCO wameona tunaendelea kuwa katika viwango na hatujawahi kufutwa wala kuingia katika viwango vinavyoashiria hatari ya kuanguka, hii inaonesha kuwa, tumeendelea kuvilinda, kuvihifadhi na kuvitunza.”

Kwa mujibu wa Ofisa Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni wa NCAA, Selestinus Emmanuel, hifadhi hiyo ni moja ya maeneo ya kipekee yenye hadhi tatu kutoka UNESCO- Urithi wa Dunia Mchanganyiko (asili na utamaduni), Man and Biosphere Reserve na UNESCO Global Geopark.

Kimsingi, eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni zaidi ya eneo la uhifadhi wa maliasili. Utajiri wa vivutio vya urithi wa utamaduni kama Nyayo za Laetoli na Bonde la Oldupai ni moja ya mambo yaliyofanya UNESCO kuipa Hifadhi ya Ngorongoro hadhi ya Urithi Mchanganyiko wa Dunia mwaka 2010.

Selestinus anafafanua kuwa, sifa zilizotajwa awali zimesaidia Hifadhi ya Ngorongoro kupata hadhi za kimataifa kwani mwaka 1979 eneo hio lilipata hadhi ya Urithi Dunia wa Asili na mwaka 2010 likapata hadhi ya Urithi wa Dunia Mchanganyiko (asili na utamaduni) na mwaka 2018 lilipata hadhi mpya iitwayo Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark. Uchambuzi wa kihabari katika vyanzo mbalimbali umebaini kuwa, ili kupata hadhi hii ya kimataifa, lazima rasilimali na vivutio vya utalii vilivyopo viwe na thamani ya kipekee vinavyokubalika kimataifa.

“Mfano mzuri ni nyayo za Laetoli, Bonde la Olduvai, Mlima Lengai, Kreta ya Ngorongoro na mchanga unaohama,” anasema Emmanuel na kuongeza: “Pia, yapo maeneo mengi nchini yanayoweza kuwa na hadhi hiyo kutokana na urithi wa kipekee uliopo katika maeneo hayo.”

“Kwa kweli tumejifunza na kuona Tanzania kuna sehemu nyingi zenye uwezekano wa kuwa utalii wa jiolojia na tunaamini tafiti mbalimbali huenda zikaendelea kufanywa na wadau mbalimbali katika kutambua maeneo ya namna hiyo.”

MAAJABU YA MCHANGA UNAOHAMA

Mchanga unaohama ni moja ya vivutio vya kipekee katika eneo la utalii wa jiolojia la Ngorongoro- Lengai. Mchanga huo wa maajabu una asili ya sumaku. Kwa mujibu wa maelezo ya wataalam na wenyeji katika eneo la Ngorogoro ulitokana na mlipukio wa Mlima Oldonyo Lengai (Mlima wa Mungu) yapata miaka milioni mbili iliyopita.

Selestinus Emmanuel, Mkuu wa Kituo cha Olduvai anasema: “Mchanga huu unapatikana takribani kilomita 5 kutoka Bonde la Olduvai ambapo huhama kutokana na nguvu ya upepo kutoka Mashariki kuelekea Magharibi ukiwa umeshikana bila kubadili sura ya umbo lake kutokana na asili yake ya sumaku na unasogea kwa takriban mita 17 kwa mwaka sawa na kuhama kwa sentimeta 4.66 kila siku huku ukiendelea kushikilia sura ya mwezi mchanga isiyobadilika.”

Inaelezwa na vyanzo kadhaa kuwa, kima cha mchanga huu ni takriban mita 5 na kwamba, huua mimea na wadudu katika eneo unapopita na huchukua muda mrefu mimea kuota tena.

Ofisa wa Urithi Utamaduni wa NCAA aliyepo eneo la Bonde la Oldupai, Godfrey Olemoita anasema mchanga huo uliotupwa na mlipuko wa Mlima Oldonyo Lengai yaani Mlima wa Mungu (Kimasai), ni sehemu inayoheshimika kwa wenyeji wa maeneo hayo hasa Wamasai na wengi huenda kufanya ibada (matambiko) wakiongozwa na ‘wazee safi katika jamii.’

“Wenyeji wa maeneo hufanya ibada na matambiko mbalimbali kuomba watoto; kwa wanawake ambao hawajapata watoto; wanakuja kuomba mvua na hata pia kuombea kutokuwapo kwa magonjwa yakiwamo ya mifugo na wengine huacha hata sadaka zao mbalimbali ambazo hata hivyo, siyo rahisi kuziona kutokana na mchanga huo kuhama,” anasema Olemoita.

Mintarafu namna ya kuzuia mchanga huu usiende mbali hata kuvuka eneo la hifadhi kwa miaka ijayo, Olemoita anasema: “Hiyo ni asili; hatuwezi kusema tuzuie hata kwa kusomba kwa malori na kurudisha unapotoka; hii kama itatokea hivyo, basi itabaki kuwa historia, lakini hatuwezi kufanya lolote kuzuia asili.”

Emmanuel yeye anasema: “Haijulikani sababu hasa ya sura ya mchanga huu kutobadilika maana unasukumwa na upepo, lakini unakwenda kama gurudumu lililoshikamana…”

“Ndiyo maana NCAA kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), tunapanga kufanya utafiti kujua mchanga huo una nini ndani yake. Tunataka kujua madini yaliyomo, ujazo wake na kujua chini yake kuna nguvu gani na pengine nguvu ya upepo.”

Vyanzo hivyo vya habari vinabainisha kuwa, mchakato wa kuhama kwa mchanga huu kwa utaratibu maalumu unaofanya umbo la nusu mwezi lisilobadilika, ni miongoni mwa vigezo vikubwa vilivyoifanya eneo la NCAA kutambuliwa na UNESCO kama eneo la utalii wa jiolojia. Inaelezwa kuwa upepo unapovuma, punje ya mwisho ya mchanga huo wenye umbo la nusu mwezi huanza kwa kusukumwa mbele na kusubiri kwanza punje nyingine kufuatia na mchakato huendelea hivyo hadi lundo lote la mchanga huo linapoisha na kuwa umesogea.

Hali hiyo huenda kwa mzunguko huo mithili ya gurudumu linalotembea na mchanga huu maarufu ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya watalii nchini Tanzania.

Mbali na vivutio vingi vya utalii wa urithi wa utamaduni vilivyopo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro vikiwamo vya Bonde la Oldupai, Makumbusho ya Leakey, Nyayo za Laetoli na vingine vingi, serikali hivi karibuni iliikabidhi NCAA vituo vitano vya mambokale ikiwemo Mapango ya Amboni yaliyoko mkoani Tanga na Kimondo cha Mbozi kilichopo Mkoani Songwe.

Vingine ni Michoro ya Miambani ya Mumba, Magofu ya Engaruka na Nyayo za Engaresero kwa ajili ya kuviboresha kimiundombinu, kuviendeleza kiutalii, na kuvitangaza ili kuvifanya kama moja ya maeneo muhimu ya utalii na kuongeza pato la taifa.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi