loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tarura inavyojenga na ‘kufufua’ barabara Tanga

KILIMO ni moja ya sekta zinayotegemewa kwa kiwango kikubwa kuchangia uchumi wa viwanda ambao Tanzania inapambana kwa hali na mali kuujenga. Mbali na kulisha Watanzania, kilimo kinachangia takribani asilimia 50 ya mali ghafi ya viwanda nchini.

Kutokana na hali ya hewa na ardhi nzuri yenye rutuba, Mkoa wa Tanga ambao makala haya yanauangazia, ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya wakazi wake na mikoa jirani. Wakazi wengi wa Tanga hutegemea kilimo, ufugaji na uvuvi katika kupata ‘mkate’ wao wa kila siku.

Mazao ya chakula yanayolimwa Tanga ni pamoja na mahindi, muhogo, ndizi, maharage na mpunga huku yale ya kilimo yakiwa katani, pamba, kahawa, chai, hiliki, nazi, tumbaku na korosho.

Mifugo ni ng’ombe, mbuzi, kondoo pamoja na kuku. Kama ilivyo kwa mikoa mingine, idadi kubwa ya wakazi wa Mkoa wa Tanga wanaishi vijijini na shughuli yao kubwa ni kilimo. Hivyo, uboreshaji wa miundombinu ya barabara na kuwapelekea umeme wa uhakika na maji ni mambo ya msingi yatakayosaidia kunyanyua kilimo katika mkoa huo na Tanzania kwa jumla hivyo, kuchochea uwekezaji katika sekta hiyo ya kilimo kukua kwa kasi.

Kuhusu barabara, Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani Tanga umekuwa na kazi muhimu ya kupanga, kusanifu, kujenga, kukarabati na kufanya matengenezo ya mtandao wa barabara za vijijini na mijini kwa kuzingatia ufanisi wa gharama kwa ajili yamaendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Takwimu za Mwaka 2012 zinaonesha kuwa, Mkoa huo wa Tanga uliopo Kaskazini mwa Tanzania ukipakana na nchi jirani ya Kenya, una watu 2,045,205. Tarura inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uboreshaji wa barabara za mijini na vijijini katika mkoa huo.

Mratibu wa Tarura katika Mkoa wa Tanga, George Tarimo, anasema Wakala huo una mtandao wa barabara wa kilomita 6,919.38 na kati ya hizo, kilomita 3,047.72 ni za mjazio), kilomita 3,278.89 ni za mkusanyo wakati kilomita 592.77 ni za jamii na vijiji.

Anasema: “Kutokana na uhitaji mkubwa wa miundombinu ya barabara vijijini na mijini katika mkoa huu, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020, Tarura mkoani hapa iliidhinishiwa Sh bilioni 13.15 kwa ajili ya kufanyia matengenezo mtandao wake wa barabara.”

“Fedha hizo zilikuwa katika mchanganuo wa matengenezo ya barabara zenye jumla ya urefu wa km 842.606, matengenezo ya sehemu korofi na matengenezo ya muda maalum.”

Mintarafu utengenezaji wa madaraja, Tarimo anasema fedha zilizopitishwa ni Sh 1,974.84. Kwa mujibu wa Mratibu huyo, tangu Tarura ianzishwe takribani miaka mwili iliyopita, imeleta mapinduzi makubwa ya miundombinu hususani katika barabara za vijijini kutokana na kufungua barabara nyingi zilizokuwa hazipitiki hapo awali.

Anasema katika Mwaka wa Fedha 2019/2020, Tarura mkoani Tanga inatekeleza miradi miwili ya maendeleo na miradi ya ahadi za viongozi miwili. Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, Theophilda Domisian, anasema halmashauri hiyo inatekeleza mradi wa maendeleo ambapo barabara ya Soni –Mponde yenye urefu wa kilomita 0.5 inajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 90.

Meneja wa Halmashauri ya Korogwe Mji, George Bwire, anasema mji huo unatekeleza mradi wa maendeleo ambapo barabara ya Kibo-Mamanko yenye urefu wa kilomita 0.35 inajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba, utekelezaji wake umefikia asilimia 20.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Meneja Elia Mgaya anasema wakala katika halmashauri hiyo unatarajia kutekeleza mradi unaotokana na ahadi za viongozi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa lami kipande cha barabara ya Kibwengo-Majimaji-Sokoni chenye urefu wa kilomita 0.6.

Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya Mji wa Handeni, Judica Makyao, anasema moja ya barabara wanazoshughulikia kwa lami ni kipande cha Bombay chenye urefu wa kilomita 0.46.

Kaimu Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya Kilindi, Vedastus David anasema kwa Mwaka wa Fedha wa 2019/2020 walipokea Sh 118,397,000.00 kwa ajili ya matengenezo ya dharura yaliyokuwa nje wa bajeti kwa ajili ya kivuko cha barabara ya Tamota-Kwadundwa- Lulago-Lwande.

Anasema walipokea Sh 52,120,000.00 kwa ajili ya matengenezo ya dharura ya Barabara ya Songe – KKKT Mvungwe na Sh 4,150,000.00 kwa ajili ya ukarabati wa dharura wa makalavati mawili katika Barabara ya Msente-Kolang’a-Kwekinkwembe, sambamba na ukarabati wa kivuko kimoja (solid drift) katika barabara ya Mpakani-Kolang’a.

Naye Meneja wa Tarura wa Halmashauri ya Handeni, Julius Omary, anasema katika Mwaka wa Fedha wa 2019/2020 walipewa Sh 82,832,160.00 zilizokuwa nje ya bajeti ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya matengezezo ya dharura barabara za Kwasambogo – Kabuku, Sindeni – Mzeri, Mbagwi –Msomera na Komsala –Mnyuzi zilizokuwa zimeharibiwa na maji.

Kwa upande wake, Meneja wa wakala huo katika Halmashauri ya Lushoto, Richard Sululu, anasema wanahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa km 657.62 na kwamba, mwaka huu wametengewa Sh bilioni 1.3.

Anasema Tarura wamefungua barabara nyingi katika Wilaya ya Lushoto ambao ni wazalishaji wakubwa wa matunda ya aina mbalimbali, hatua anayosema imewapa urahisi mkubwa wakulima kufikisha sokoni mazao yao. John Msita, Meneja wa Tarura katika Halmashauri ya Mkinga anasema wanasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 730.

Anasema katika kipindi kifupi wameweza kufungua barabara zenye urefu wa kilometa 200 ambazo hazikuwepo tangu Uhuru, hatua inayowarahisishia wananchi kuwa na barabara mbadala katika kufikia masoko na huduma za msingi za kijamii kama hospitali na shule. Kwa mujibu wa Msita, ufunguzi wa Barabara ya Horohoro – Boda yenye urefu wa maili kumi, umekuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji kwa ajili ya urahisi wa kupeleka mifugo mnadani.

“Awali walikuwa wanazunguka umbali mrefu ili kuufikia mnada. Hii imesaidia sana hasa kwa kuzingatia kwamba, Mkinga ni mpakani mwa Tanzania na Kenya,” anasema.

Anasema kufunguliwa kwa barabara hizo kumesaidia hata kufanya doria za mara kwa mara kwa ajili ya ulinzi na usalama. Meneja wa Tarura wa Jiji la Tanga, Boniface Mwambene, anasema katika jiji hilo, anasema mwamba unaotuamisha maji (water table) uko karibu na hivyo kusababisha kutuwamisha maji mengi wakati mvua zinaponyesha na kusababishya mafuriko ya mara kwa mara yanayoharibu pia barabara. Anasema maeneo ya Sahare na Magaoni ni miongoni mwa maeneo yanayokumbwa na mafuriko ya mara kwa mara.

“Tumeanzisha ujenzi wa mirefejiambayo itakayokuwa inapitisha maji kuelekea baharini na pia, kuongeza midomo ya madaraja ili kurahisisha maji yaliyopo katika upande wa Sahare kuvuka kuelekea baharini kwa urahisi,” anasema Mwambene.

Anaongeza kuwa, hali hiyo inaonesha kwamba Jiji la Tanga linafaa kuwa na barabara za kiwango cha lami zaidi na hivyo bajeti kubwa kuhitajika. Mratibu wa Tarura Tanga, Tarimo anasema katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 mkoa umependekeza bajeti ya Sh bilioni 13.2 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya barabara na Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya madaraja.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi