loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Halmashauri Kibaha wahitaji bil 1.2/- kukamilisha jengo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani inahitaji Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo lake jipya ambapo kwa sasa inatumia ofi si saba kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Kibaha, Butamo Ndalahwa mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi hiyo lililopo Mlandizi.

Ndalahwa alisema kuwa halmashauri hiyo imepata changamoto ya ukosefu wa ofisi kwa watumishi baada ya halmashauri zote nchini kutakiwa kuwa kwenye maeneo ya halmashauri husika ambapo zamani walikuwa wakitumia jengo la mkuu wa wilaya kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha.

Ujenzi huo ulitakiwa kukamilika mwaka jana lakini walipata changamoto ya upatikanaji wa fedha, ilibidi mkataba uongezwe kwa mkandarasi ambaye ni Suma JKT hivyo ujenzi utakamilika Julai 2020.

“Gharama za mradi ni Sh bilioni 4.6, lakini awali tulikadiria kutumia Sh bilioni 2.7, kutokana na hali ya udongo na baadhi ya vitu kutoingizwa kwenye mkataba ilibidi bajeti iongezeke na kufikia bilioni 4.6 hadi kukamilika kwake,”alisema.

Aidha alisema kuwa baadhi ya vitu ambavyo havikuingizwa kwenye mkataba na kusababisha gharama kuongezeka ni pamoja na gharama za umeme, mkongo wa taifa, miundombinu ya Tehama, uzio na thamani za ofisi kwenye majengo ya ofisi ambapo ni ghorofa tatu.

“Hadi sasa mkandarasi kashalipwa Sh bilioni 1.8 ambapo serikali kuu hadi sasa wameshatoa Sh bilioni 2.1 na kwa mwaka huu wa fedha zimetengwa Sh milioni 900 na halmashauri imepokea Sh milioni 667,” alisema.

Kwa upande wake Waziri Jafo alisema kuwa serikali imetenga fedha kwa ajili ya halmashauri zote mpya kwa ajili ya majengo ya ofisi zao, hivyo maombi hayo yatafanyiwa kazi na kitakachopatikana watapewa ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.

Jafo alisema anajua kuwa fedha hazitoshi lakini watahakikisha fedha zinapatikana ili ujenzi huo ukamilike na wananchi waweze kupata huduma kuliko ilivyo sasa. Alisema amefurahishwa na usimamizi mzuri wa jengo hilo na wakandarasi ambao ni Suma JKT kwa kazi nzuri.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: John Gagarini, Kibaha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi