loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Loya washukuru kuunganishiwa umeme

WAKAZI wa Kijiji cha Loya wilayani Uyui mkoani Tabora, wameishukuru serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuwaunganisha na kuwawashia umeme katika kijiji hicho ambacho awali wakazi hao walikuwa wakiona kama ni ndoto.

Wameeleza hayo baaada ya Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani juzi kuwasha umeme katika kijiji hicho na kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika wilaya hiyo.

Wakazi wa kijiji hicho walisema kuwa miaka mingi wamekuwa wakipewa ahadi zisizotekelezeka na wakati mwingine wamekuwa wakikatishwa tamaa ya kupata umeme kwa kuwa kijiji hicho kiko umbali mrefu kutoka ilipo miundombinu ya umeme, pia kuwa na jiografia isiyo rafiki kufika maeneo hayo.

“Huyu Waziri ameandika historia hapa Loya, haijawahi kutokea kiongozi mkubwa ngazi ya waziri kufika katika kijiji chetu tangu kimeanzishwa, wengi wanakuja katika wilaya hii lakini wanaishia huko mjini tu vijijini hawafiki, amekuja kutuwashia umeme tunamshukuru sana. Pia tunamshukuru Rais Magufuli kumkubalia huyu waziri kuja huku kwetu kutuletea umeme, abarikiwe sana”, alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Josephat Wamalulu.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dk Kalemani alisema baada ya kusikia malalamiko na kuona uhitaji mkubwa wa umeme kwa kijiji hicho ambapo bado hakijafikiwa na mradi wa kusambaza umeme vijijini kwa kipindi hiki, aliagiza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kupeleka umeme kwa gharama zao katika kijiji hicho.

Alisema kijiji cha Loya kina wakulima wengi wa mpunga, karanga na wafanyabiashara ambao wanahitaji huduma ya umeme katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi. Kwa mantiki hiyo, Tanesco ilitenga zaidi ya Sh bilioni tatu ili kuhakikisha umeme unafika katika kijiji hicho, ambacho kiko umbali mrefu kutoka ilipopita miundombinu ya umeme.

“Tutapeleka katika vijiji vingine, cha msingi hapa ni ninyi wananchi kusuka nyaya katika nyumba zenu, na kulipia shilingi 27,000 tu umeme utawafikia,”alisema Dk Kalemani.

Aidha aliwaagiza Tanesco, kuendelea kusambaza na kuwasha umeme kwa wakazi wa eneo hilo waliokwishalipia gharama za kuunganishiwa umeme ndani ya siku saba baada ya kulipia.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Tabora

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi