loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shangwe Ligi Kuu kurejea

Baada ya Rais John Magufuli, jana kutangaza michezo itaanza Juni Mosi, wadau mbalimbali wamepongeza kurejeshwa na Bodi ya Ligi (TPBL) imesema wako tayari wanachosubiri ni utaratibu toka serikalini.

Aidha Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abasi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema wamepokea kwa unyenyekevu agizo hilo na timu zote za soka zinaruhusiwa kuanza mazoezi na taratibu za kiafya zitatolewa.

“Tumepokea kwa unyenyekevu agizo la Rais la ligi na michezo kurejea.Huu uamuzi umekuja kwa wakati.Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo tumeupokea kwa tabasamu na timu zote za ligi za soka ruksa kuanza mazoezi rasmi. Taratibu za kuzingatiwa kiafya zitatolewa,” alisema Dk Abasi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao ambao timu zao zinashiriki Ligi Kuu walisema wamepokea kwa furaha tamko hilo wakijua wazi kazi ya kupambana inaanza karibuni hivyo walitarajiwa kukutana kuweka mikakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu, Almas Kasongo alisema wameipokea taarifa kwa furaha ila wanasubiri utaratibu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Alisema wamejipanga kuhakikisha ligi inaendelea pale ilipoishia ila wanatarajiwa kukutana kwa ajili ya kujua utaratibu wa jinsi itakavyokuwa pamoja na kuandaa ratiba.

“Sisi tumesikia tamko na mikakati yetu ni ligi iendelee kuchezwa na hivyo tumejiandaa tukisubiri taratibu nyingine kutoka wizarani pia tutakutana kujua ratiba itakuwaje,” alisema Kasongo.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema wamepokea kwa furaha tamko hilo wakijua wazi kazi inaanza ya kwenda kupambana hivyo walitarajiwa kukutana jana jioni kujadili ni lini hasa wachezaji waingie kambini kuanza maandalizi ya ligi na ndani ya siku mbili wataanza mazoezi wakati wakisubiri tamko la Bodi ya Ligi. Bwire alipendekeza mfumo uliokuwa unatumika awali wa nyumbani na ugenini uendelee kutumika ili kila mmoja aweze kuvuna anachostahili.

Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema tamko la Rais Magufuli limeleta faraja kwa Watanzania kwa kuonesha namna anavyothamini michezo na wao wanamuunga mkono.

Alisema wanatarajia kuita timu kambini baada ya sikukuu ya Idd ili waanze kujipanga kwa michezo ili kumalizia michezo iliyobaki. Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa amesema wako tayari kuanza kazi kwa utaratibu maalumu utakaowekwa. Yanga ilisema kabla ya kuanza mazoezi ya maandalizi ya kurejea kwa ligi watawapima wachezaji kama wana maambukizi ya corona.

“Sisi tuko tayari kuanza ligi tunasubiri utaratibu utakaowekwa, tumejiandaa , naamini mambo yatakwenda vizuri kama yalivyopangwa ,kikubwa ni kuzingatia kanuni za afya za kujikinga ili tusipate maambukizi ya corona,” alisema.

Rais wa shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF) Phares Magesa amempongeza Rais Magufuli kurejesha michezo na sasa wanasubiri mwongozo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuwa michezo itachezwaje.

“Kulikuwa na ligi za mikoa zilianza Februari zikasimama baada ya corona, tutaendelea pale tulipoishia lakini ni muhimu kusubiri mwongozo kujua michezo itahitaji mashabiki au itachezwa bila mashabiki na ikibidi tutasogeza ratiba mbele ili imalizike, tuendelea na ligi za taifa,” alisema.

Bondia wa zamani wa ngumi za kulipwa Ally Bakari ‘Champion’ alisema kitendo cha Rais John Magufuli kurejesha rasmi michezo ni faraja kwa wanamichezo kutafuta tonge. Champion ambaye kwa sasa ni mwamuzi wa ngumi alisema kwa muda mrefu wamekuwa hawana shughuli za kufanya wakijifungia ndani kwa kuhofia wakitoka huenda wakapata maambukizi ya virusi vya corona.

“Rais Magufuli ni kichwa, namsifu kwa ujasiri aliouonyesha kwa sababu tutajifungia ndani mpaka lini, inabidi tuzoee huu ugonjwa kama yalivyo mengine, tukapambane na maisha, tumepata faraja kwa kurejesha michezo tena,” alisema.

Baada ya jana Rais John Magufuli kutoa tamko la kuruhusu michezo kuanza Juni Mosi, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liliitisha kikao cha dharura jana hiyo hiyo na wadau wake Kikao hicho kilianza majira ya mchana kwenye ofisi zao zilizopo Uwanja wa Taifa, kujadili na kutoka na mwongozo wa namna michezo itakavyoendeshwa kwa kuzingatia kanuni za afya kwa wachezaji, makocha na watu waandishi wa habari.

Katibu wa BMT, Neema Msitha alisema wanafanya kikao cha dharura kitakacho toka na mwongozo wa namna ligi itakavyochezwa.

“Tumeitisha kikao cha dharura kujadili na kutoka na mwongozo wa namna ya kuendesha michezo wakati huo tukizingatia afya na kujikinga na ugonjwa wa corona,” alisema.

Msitha alisema leo wanatarajia kutoa mwongozo baada ya kikao cha jana. Machi 17 baada ya Tanzania kuripoti mgonjwa wa kwanza wa COVID-19, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kusimamisha shughuli zote za michezo nchini pamoja na mikusanyiko yote na kufunga shule zote nchini kuanzia awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kwa siku 30 lakini baadae alitangaza kuendelea kufungwa hadi hapo serikali itakapotangaza vinginevyo. Imeandikwa na Grace Mkojera, Tuzo Mapunda na Rahel Pallangyo.

MWIGIZAJI maarufu wa tamthilia ya Karma, Wema Sepetu amewaomba radhi ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi