loader
Picha

Mahakama yaelezwa maamuzi yoyote ya Bunge hayahojiwi

SERIKALI imeieleza Mahakama ya Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuwa maamuzi yoyote yanayotolewa na Bunge, hayaruhusiwi kuhojiwa na chombo chochote.

Hayo yalielezwa jana na Wakili wa Serikali Mkuu, Vicent Tango wakati akiwasilisha mapingamizi ya awali, yenye hoja tano katika Kesi ya Kikatiba Namba 10/2020, iliyofunguliwa na Wakili Paul Kaunda, anayeiomba Mahakama Kuu kutengua amri ya Spika wa Bunge, Job Ndugai ya kumtambua Cecil Mwambe kama mbunge halali wa Ndanda Kaunda alifungua kesi hiyo dhidi ya Spika wa Bunge, Ndugai, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ndanda kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Cecil Mwambe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Tango alidai mbele ya jopo la majaji watatu, linaloongozwa na Jaji Issa Maige akishirikiana na Jaji Stephen Magoiga na Jaji Seif Kulita, kuwa chochote kinachofanyika bungeni kinalindwa na Ibara ya 100 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Alidai kuwa mahakama hiyo, haina mamlaka kusikiliza shauri hilo na kutoa nafuu, zinazoombwa kwa mujibu wa Ibara ya 100(1) ya Katiba ya Nchi na Kifungu cha 3 cha Sheria ya Bunge ya Haki, Kinga na Mamlaka.

Alidai kwamba shauri hilo halina maana, kwani ni la usumbufu tu. Alidai ibara hiyo ni maalum, kwa ajili ya kulinda mhimili wa dola, bila kuingilia mamlaka yake. Pia, alidai mdai hana haki ya kisheria, kupewa nafuu anazoziomba katika shauri hilo, na kwamba hati ya kiapo kinachounga mkono maombi hayo kina kasoro za kisheria, ambazo haziwezi kurekebishika.

“Tunaomba pingamizi likubaliwe na mahakama itoe uamuzi kwamba haina uwezo wa kusikiliza kesi hii, hivyo ifutwe kwa gharama,” alidai Tango.

Katika hoja nyingine, Wakili wa Serikali Mkuu, George Mandepo alidai mtu yoyote anaweza kwenda mahakamani kufungua kesi, lakini anapaswa kufuata sheria. Alidai kuwa shauri hilo halistahili kuwepo mahakamani hapo, kwa kuwa linakinzana na Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, pamoja na Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Nchi.

Pia, alidai mdai alitakiwa kuleta mahakamani kielelezo cha video, kuonesha chanzo cha taarifa kuhusu madai hayo amezitoa wapi na kuambatanisha hati ya kiapo kuhusu kielelezo hicho. Alidai kuwa Spika hajavunja sharti lolote la Katiba ya Nchi kama inavyodaiwa na hivyo alimtaka mdai kuthibitisha madai yake.

Serikali pia inadai kuwa Mwambe bado ni mbunge halali wa Ndanda kwa mujibu wa Katiba na Sheria nyingine za nchi na anastahili stahiki zote kwa mujibu wa sheria na kanuni, zinazotumika kusimamia masuala ya Bunge.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa mdai, Daimu Halfan alidai mtu yoyote anaweza kwenda mahakamani na kuelezea kama katiba imevunjwa. Alisema kwamba suala la kufungua kesi bila kuainisha kifungu cha sheria sio lazima, kwani kinachotakiwa ni kuona namna ya kulinda katiba. Alidai kuwa mwombaji ana mamlaka ya kuleta maombi hayo mahakamani, kwani anaona katiba inavunjwa, kwa kitendo cha Mwambe kuendelea kuwa mbunge, ilihali ameshajivua uanachama.

Hata hivyo, Jaji Maige alihoji kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatamka kwamba Mwambe sio mbunge, Je, mahakama ina mamlaka gani ya kutamka hivyo?. Wakili Halfan alidai mtu anapochaguliwa na wananchi, ndio tume inatangaza matokeo kwamba ni nani ameshinda, lakini baada ya kuchaguliwa haisemwi.

Pia, alidai Spika ndiye ana mamlaka ya kuitaarifu tume kuwa kiti cha ubunge kiko wazi baada ya kukosa sifa. Alidai kitendo cha Mwambe kujivua uanachama, moja kwa moja kinamkosesha sifa ya kuendelea kuwa mbunge halali. Jaji Maige aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 28, mwaka huu kwa ajili ya uamuzi. Aliagiza mdaiwa wa pili (Mwambe) kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo na kumpatia mdai.

Katika kesi hiyo, Wakili Kaunda anadai Mwambe alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), kauli ambayo iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliyempokea rasmi Mwambe mbele ya hadhira kwa kumkabidhi kadi ya CCM, na Mwambe naye alimkabidhi Katibu Mkuu huyo kadi yake ya Chadema.

Wakili Kaunda anadai kitendo cha Spika kumtambua Mwambe kama mbunge halali, wakati ameshajivua uanachama wa chama kilichomdhamini kama mbunge wa Ndanda (2015- 2020), ni ukiukwaji wa Ibara ya 71(1) (f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Wakili huyo anadai kuwa hakuna mamlaka yoyote nchini, achilia mbali Spika, yenye uwezo wa kumrudisha bungeni mbunge ambaye kwa hiari yake mwenyewe, ameamua kujivua uanachama wa chama cha siasa, kilichomdhamini kupata ubunge.

WANANCHI wa kisiwa cha Pemba  visiwani Zanzibar wamepongezwa kupambana na ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi