loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Furaha iliyoje michezo kurejea

HONGERA Amri Jeshi Mkuu na Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli kwa kuruhusu michezo yote kuchezwa. Michezo yote nchini ilisimamishwa takribani miezi miwili iliyopita, baada ya kulipuka kwa janga la virusi vya corona duniani kote. Dk Magufuli Alhamisi alilihutubia taifa kutoka Ikulu ya Chamwimom Dodoma baada ya kuwaapisha watu aliowateua kushika nyadhifa tofauti tofauti.

Baada ya zoezi hilo, Rais Magufulu alihutubia taifa kutoka mkoani Dodoma, ambapo alizungumza mengi, ikiwemo kurejesha michezo yote kuanzia Juni Mosi. Rais ametoa tangazo hilo baada ya kuridhika na ari ya corona, kwani sio mbaya na inaendelea vizuri na ni matarajio ya wengi kuwa Tanzania itaendelea kuwa katika hali nzuri na mambo mengine yataachiwa kuendelea.

Mbali na michezo, pia vyuo pamoja na kidato cha sita watarudi madarasani kuanzia siku hiyo ya Juni Mosi, huku madarasa mengine yakisubiri kuona hali inaendaje kabla na wao kuruhusiwa. Safu hii inampongeza sana Rais Magufuli kwa kuamua michezo kuendelea, huku taratibu zingine zikiachiwa wahusika pamoja na mamlaka zinazohusika na michezo ikiwemo Wizara ya Afya kushughulikia.

Baada ya kurejeshwa kwa michezo sasa ni jukumu la mashirikisho ya michezo, Wizara husika na vyombo vingine kukaa chini na kuangalia utaratibu gani utatumika, hasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuendelea.

Ligi Kuu Tanzania Bara inaweza kuchezwa kwa makundi, ambapo timu zinaweza kupangwa katika kituo kimoja na kucheza, hii itasaidia ligi kumalizika mapema na kwa wakati licha ya kutochezwa kwa takribani mwezi mmoja.

Huu ni mfumo mzuri kwani pia utasaidia timu kukaa mahali pamoja na kusaidia wachezaji kutokutana na watu tofauti tofauti mitaani, kitu ambacho kitasaidia kupunguza uwezekano wa wachezaji kupata corona.

Ni matumaini ya safu hii kuwa mashirikisho pamoja na vyama vyote vya michezo vitapokea tamko la Rais Magufuli kwa furaha kubwa na kupanga mikakati na taratibu za jinsi ya kuendesha michezo yao wakati wa kipindi hiki.

Tayari, Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga imeanza na wiki hii inaingia katika juma la pili tangu ilipoanza, hivyo tunaweza kuangalia wanafanya nini, kwani nao wanacheza bila mashabiki na sisi hivyo hivyo tutacheza kwenye viwanja vitupu kwanza.

Ni matarajio kuwa michezo itaanza na itakwenda vizuri na hadi kila mchezo utamaliza msimu wake na bingwa kupatikana na hao mabingwa ndio watawakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.

Na kwa upande wa wachezaji, bila shaka sasa wanatakiwa kuanza mazoezi ili kujiweka fiti kwa ajili ya mashindano mbalimbali watakayoshiriki na wanachotakiwa ni kutoa burudani huku wakizingatia kanuni za afya.

Katika soka hasa Ligi Kuu pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho, mechi hizi zenyewe zitakuwa mubashara katika Azam TV, hivyo ni matarajio ya wengi kuwa wataona burudani safi na yenye kuvutia kutoka kwa timu shiriki.

Wachezaji wakati wa `lockdown’ walikuwa wakifanya mazoezi mmoja mmoja, lakini sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wanaweza kutoa mwongozi nini kifanyike ili kuhakikisha wachezaji wanaanza kufanya mazoezi ya pamoja.

Maisha lazima yaendelea na hasa katika kipindi hiki, ambacho wagonjwa wa corona wamepungua sana ni muhimu shughuli za michezo zikaendelea ili kuhakikisha watu wanafanya mazoezi na kuweka miili fiti.

Utamu wa michezo sasa unarudi tena, hivyo ni matarajio ya wadau kuwa timu zitajiandaa vizuri ili kumalizia sehemu iliyobaki ya msimu kuanzia mchezo wa bao hadi soka, lengo ni kupata bingwa wa nchi.

GWIJI wa muziki wa Bongo Fleva ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi