loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waliopata nafasi soko la Job Ndugai kutajwa

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amesema halmashauri hiyo inaendelea kutekeleza falsafa ya Rais, Dk John Magufuli ya kuwajali na kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wadogo (machinga).

Kunambi alisema ili kila mwananchi ashiriki uchumi wa viwanda, ni wajibu wa halmashauri ya jiji hilo kuwapa nafasi watu wote ikiwa ni pamoja na mamalishe kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao katika Kituo Kikuu kipya cha mabasi cha Dodoma.

Akizungumza jijini Dodoma kuhusu kukamilika kwa kazi ya utoaji fomu kwa ajili ya maeneo ya biashara katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma na Soko Kuu la Job Ndugai, Kunambi amesema Halmashauri yake inatekeleza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwatengenezea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo.

“Niseme wazi kuwa machinga ni sehemu ya hii stendi, hivyo kama mnavyoona eneo hili katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma tumetenga maeneo mawili maalumu kwa ajili ya machinga. Kila eneo linaweza kuhudumia machinga mia tatu. Sisi kama Jiji la Dodoma tunatekeleza falsafa ya Mheshimiwa Rais, Dk John Magufuli kwa vitendo siyo maneno,” alisema Kunambi.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa halmashauri yake imeenda mbali zaidi na kuwafikiria mama lishe wanaofanya shughuli zao katika stendi ya mabasi ya Nanenane.

“Wapo mama lishe wanaofanya shughuli zao katika stendi ya sasa ya Nanenane, baada ya stendi hiyo kuhama na kuanza kutumika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Dodoma, tutahama nao. Nimemuelekeza mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana kuwaratibu vizuri ili waweze kupatiwa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri kwa ajili ya kuboresha shughuli zao,” alisisitiza Kunambi.

Alisema wamemtengea eneo kwa ajili ya shughuli zao katika Kituo Kikuu cha Mabasi ili wasafiri ambao uwezo wao utakuwa mdogo wapate chakula kutoka kwa mama lishe.

Akizungumzia mchakato wa wafanyabiashara walioomba nafasi za kufanya biashara katika Kituo Kikuu cha Mabasi na Soko Kuu la Job Ndugai, alisema kuwa orodha ya wafanyabiashara waliofaulu kupata nafasi za kufanyabiashara itatolewa hadharani.

“Kuanzia leo wafanyabiashara wote waliofaulu kupata nafasi za biashara wafuatilie majina yao katika tovuti ya Halmashauri ya Jiji (www.dodomacc.go.tz) na mbao za matangazo ili waweze kuchukua fomu za masharti ya upangaji katika maeneo ya biashara na taratibu za kulipia ada,” alisema Kunambi.

Mkurugenzi huyo ameyataja maeneo ambayo yamebaki bila kupata wapangaji kuwa ni bucha mbili na sehemu za kupokelea mizigo 11 katika Soko Kuu la Job Ndugai na maeneo ya maduka tisa ya mita za mraba 36 pamoja na vizimba 33 vya biashara.

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Leonard Akwilapo, ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi