loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tusijisahau, tujilinde, tuwalinde wengine

UGONJWA wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) bado unaelezwa kuisumbua dunia tangu ulipoibuka kwa mara ya kwanza Desemba mwaka jana jijini Wuhan, jimboni Hubei, nchini China.

Hata hivyo katika nchi nyingi zilizotikiswa zaidi na ugonjwa huo, ikiwamo China ulikoanzia, Italia, Marekani na kwingineko, matumaini ya maambukizi kupungua yameendelea kuonekana na kusababisha viongozi wa mataifa hayo kutangaza kurejea kwa shughuli za kiuchumi, kijamii na kiimani.

Nchini Tanzania, tangu mgonjwa wa kwanza kutangazwa Machi 16 mwaka huu, viongozi wa kitaifa wameendelea kuweka nguvu kubwa katika kupambana na janga hili kwa kusihirikisha jamii kila hatua ili kupunguza athari zilizotabiriwa kulikumba Bara la Afrika.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Tanzania Bara) na Wizara ya Afya (Zanzibar) iliendelea kuratibu mikakati ya kinga na tiba kwa kuweka vituo, namba za simu na kamati ya elimu ya afya kwa umma juu ya ugonjwa huo uliosababisha maambukizi zaidi ya milioni tano duniani.

Hivi karibuni, Rais Magufuli akiwa katika ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wilayani Chato, mkoani Geita, alitangaza matumaini makubwa ya hali ya maambukizi ya corona nchini jinsi idadi ya wagonjwa ilivyopungua katika hospitali zilizotengwa kuwahudumia waathirika na kusisitiza Mungu ndiye amewezesha haya.

Aidha, Rais alitangaza kufungua anga kwa ajili ya kuanza kutua ndege za watalii na tayari tumeshuhudia zikitua, alitangaza hali ikiendelea vizuri atafungua vyuo na tayari vitaanza Juni Mosi na kusisitiza siku tatu za kumshukuru Mungu (zilizomalizika jana) kwa mema anayoitendea nchi dhidi ya janga hili.

Ni wazi kuwa, baada ya hotuba hiyo ya Rais Magufuli, Watanzania wengi walirejeshewa matumaini makubwa kwamba kwa hakika Mungu amesikia sala na maombi yao na sasa shughuli za kimaisha zinaweza kurejea hatua kwa hatua.

Hakuna anayepinga kuwa kulingana na utabiri wa hali ya maambukizi na vifo kwa Afrika, Tanzania ikiwemo, hakika Mungu ametusaidia.

Lakini kama alivyosema Rais Magufuli na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, tahadhari ni lazima iendelee kuchukuliwa kwa kuwa bado ugonjwa huu upo katikati yetu. Kinachonisikitisha ni kwamba, jana nimepita mitaa kadhaa jijini Dar es Salaam, nikaona jinsi watu walivyoacha kuvaa barakoa na kupuuza kunawa mikono

kwa sabuni na maji tiririka, kukaa umbali wa zaidi ya mita moja mtu kwa mtu na miongozo mingine. Tukipuuza ushauri huu wa afya hakika hali inaweza kuwa mbaya kuliko tuliojionea awali na tunaweza kuwapa vicheko wale waliotutabiria mabaya.

Niwasihi tusibweteke, tuendelee kufuata ushauri na miongozo ya wataalamu wa afya na kuchukua tahadhari mpaka serikali itakapotangaza rasmi kwamba janga hili limeondoka kabisa nchini. Kila mtu abebe dhamana ya kujilinda na kumlinda jirani yake dhidi ya maambukizi na kuwasaidia walioathirika wapone bila kuwanyanyapaa.

KATIKA miaka ya karibuni msimu wa mavuno kumekuwa na watu ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi