loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Corona bado ipo, tujihadhari

WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini jana na leo wameungana na waumini wenzao duniani kote kuadhimisha sikukuu ya Eid el Fitr kuhitimisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Wamesherehekea sikukuu hiyo huku wakisindikizwa na ndugu zao wa madhehebu mengine wakati serikali ikiwa imetoa angalizo la wananchi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiepusha nchi na janga la corona lakini bila kusahau kwamba bado ipo na wazingatie ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya.

Katika kushehereka Eid el Fitr na kumshukuru Mungu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akawataka wananchi kumshukuru Mungu kwa michezo, sanaa na burudani akirejea hotuba ya Rais Dk John Magufuli ya kuwataka kutumia siku tatu, Ijumaa, Jumamosi na jana kumshukuru na kumtukuza Mungu.

Rais Magufuli alisema kuna haja kwa wananchi kumshukuru Mungu kwa maombi mengine ya sala kwa siku tatu baada ya kuwa amejibu maombi yao ya awali ya siku tatu pia ya kuwaepusha na ugonjwa corona.

Alisema, kwa tathmini ya serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona umepungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waislamu kwenye Msikiti wa Gadhafi, jijini Dodoma jana wakati wa sala la Eid El Fitr alisema, hadi jana, maambukizi yalikuwa yameshuka zaidi hapa nchini. Ni kwa muktadha huo tunaungana na viongozi hao na waumini kumshukuru Mungu kuiponya Tanzania.

Kupitia maombi ya siku tatu ya waumini kila mmoja kwa imani yake na viongozi wa kimila, machifu, mkono wa Mwenyezi Mungu umejidhihirisha kwa visa vichache vya maambukizi na vifo vya corona. Ndio maana tunasema, tumefurahishwa na mwitikio mkubwa wa Watanzania kumshukuru Mungu pia. Ni matarajio yetu kuwa, maombi kwa Mwenyezi Mungu kuendelea kuiponya nchi yetu dhidi ya corona na kuwaponya ndugu zetu, majirani wa nchi za Afrika na duniani kote yataendelea na shukrani zitazidi.

Tunawakumbusha Watanzania kwamba baada ya Rais Magufuli kutangaza maombi ya shukurani, watu wasijisahau, wakaacha kufuata ushauri unaotolewa mara kwa mara na miongozo ya Wizara ya Afya kwa kuwa naye anaendelea kusisitiza kwamba ugonjwa huo bado upo na tujifunze kuishi nao huku tukichapa kazi. Watanzania tuendelee kuzingatia masharti na miongozo ya serikali, tunapokuwa kwenye ibada makanisani na misikitini.

Tuzingatie maelekezo ya wizara na taasisi za dini juu ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tirika, nafasi ya mtu na mtu, kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono wanapokuwa katika shughuli za uzalishaji ambazo zimeruhusiwa kuendelea na hata burudani.

Mfano hai ni jana ambapo watu wameonekana fukwe za bahari ya Hindi wakijirusha bila tahadhari na hata katika usafiri wa daladala, wanaonekana hawana barakoa. Corona bado ipo, tuendelee na tahadhari.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi