loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

RC- Madiwani simamieni miradi

MADIWANI katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao ili wananchi ambao ndio walipakodi waweze kufaidi matunda ya kodi zao kwa kuboreshewa huduma za kijamii na kiuchumi.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare alisema hayo juzi wakati wa kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichojadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Sanare pia aliipongeza Manispaa hiyo kwa mwenendo mzuri wa ukusanyaji mapato ya ndani ambapo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ilikusanya Sh bilioni 5.2 sawa na asilimia 94 kutoka kwenye makadirio ya kukusanya Sh bilioni 5.6.

Mkuu wa mkoa alisema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 Manispaa hiyo iliweka bajeti ya makadirio ya kukusanya Sh bilioni 6.7 lakini hadi kufikia Mei 14, mwaka huu ilikuwa imekusanya makusanyo ya Sh bilioni 6.1 sawa na asilimia 91.

“Nawapongeza watendaji na madiwani wa halmashauri ya Manispaa hii kwa kukidhi vigezo vilivyotolewa na Tamisemi vya kukusanya mapato kwa asilimia zaidi ya asilimia 80 na si chini ya hapo kulingana na maelekezo ya Tamisemi,” alisema Sanare.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kulipongeza Baraza la Madiwani na watendaji wake kwa kuendelea kulinda mafanikio waliyofikia ya kupata hati inayoridhisha kwa muda wa miaka minne mfululizo.

“Sasa ni wajibu wa baraza la madiwani na menejimenti na halmashauri kwa ujumla, kuyalinda mafanikio ya miaka yote hiyo ili msije angukia pabaya katika ukaguzi unaoendelea tena mwaka huu,” alisema Sanare.

Hata hivyo aliutaka uongozi wa manispaa hiyo pamoja na madiwani kufanya tathimini mpya ya vyanzo vipya vya mapato vitakavyosaidia kuongeza mapato ya ndani ili kuboresha maendeleo ya huduma za kijamii na kiuchumi. Katika hatua nyingine, mkuu wa mkoa aliwataka madiwani na menejimenti ya halmashauri hiyo kuhakikisha kuna kuwa na usimamizi mzuri wa mikataba inayoingiwa na wakandarasi kwa ajili ya maslahi ya wananchi .

“Tumeona hapa mikataba miwili tayari imevunjwa kwa wakandarasi kutokuwa na vitezo na kushindwa kazi , mnatakiwa kuwa makini kuwapitiosha watandarasi wenye uwezo na sifa za kazi ili fedha za wananchi zisipotee,” alisema Sanare.

Meya wa Manispaa hiyo, Pascal Kihanga alisema halmashauri imekuwa na mafanikio mbalimbali yakiwemo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya serikali, madiwani na Chama Tawala na uendelee kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Hata hivyo, alisema pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto zilizojitokeza katika ukusanyaji wa mapato ambapo wafanyabiashara wamekuwa wakikwepa kulipa kodi halali kwa kutoa visingizio mbalimbali, lakini halmashauri inaendelea na jitihada za kutoa elimu kwao kujua umuhimu wa kulipa kodi.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa huo, Emmanuel Kalobelo alizitaka halmashauri zote za mkoa huo kuzitumia kwa wakati fedha zilizotengwa kwenye bajeti inayomalizika Juni mwaka huu ili kuepuka tabia ya kuchelewa kutumia fedha za baadhi ya miradi ya maendeleo.

“Wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa wetu tumieni kwa wakati fedha za miradi ya maendeleo kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha, unapochelewa kuzitumia fedha hizo humezwa na mfumo au kurudishwa Hazina, jambo hili lisifanyike kwa halmashauri yoyote,” alisema Kalobelo.

Rais John Magufuli ameipongeza Benki Kuu (BOT), sekta ya benki ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi