loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukizingatia ushauri kuishi na VVU si tatizo

Maambukizi ya virusi vya Ukimwi huambatana na changamoto mpya za unyanyapaa,ingawa hilo haliwezi kuwa tatizo kwa mtu aliyeikubali hali hiyo na kuamua kufuata ushauri tiba.

Pamoja na kuwepo kwa changamoto za unyanyapaa mtu mwenye maambukizi ya VVU anaweza kuishi maisha marefu zaidi kuzidi yule asiye na maambukizi na huu ni ushuhuda unaopatikana maeneo mengi nchini.

Bukoba ni miongoni mwa maeneo hayo ambapo kundi la wanaoishi na VVU wamekutana na kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na haki zao ambazo pia zinatajwa katika Sera ya Taifa ya Ukimwi ya Mwaka 2001.

Kimsingi, haki zao watu walio katika kundi hili kama zilivyo haki za wengine katika huduma za afya na matibabu, hazipaswi kuvunjwa kwa namna yoyote, bali kulindwa sambamba na fursa nyingine zote kama yalivyo makundi mengine katika jamii ambayo hayajajitangaza kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Katika kusanyiko hilo pamoja na kujadili changamoto mbalimbali na kudai haki zinazotajwa, walikumbushwa pia wajibu wao katikia kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi.

KILIO CHA MIKOPO

Imebainika kuwa, katika baadhi ya maeneo, kumekuwa na changamoto kwani licha ya serikali na wadau wengine kutoa fursa za mikopo kwa makundi mbalimbali, bado watu wengi na virusi vya Ukimwi katika vikundi vyao, wanajikuta hawakopesheki kutokana na vikwazo ambavyo ufumbuzi wake uko mikononi mwao.

Mzee Said Nshaija ni miongoni mwa wananchi wanaoishi na maambuzi ya VVU kwa miaka zaidi ya kumi huku akiwa tayari amempoteza mwenzi wake ambaye juhudi zao kuunda kikundi imara cha wenye VVU ili waweze kukopesheka zilikwama.

Anasema baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa fedha za kukopesha makundi mbalimbali aliamua kutafuta wananchi wa kundi lake ili wauunde na kusajili kikundi kwa lengo la kunufaika na mikopo hiyo juhudia ambazo hazikufanikiwa.

Kwamba wananchi wengi aliowafikia pamoja na kuwa tayari wana maambukizi, bado walikataa wazo la kuunda kikundi cha kuwatambulisha kama wenye maambukizi ya VVU na kujikuta wanashindwa kuifikia fursa hiyo.

Kwa mujibu wa Ofisa Anayehusika na Mikopo kwa Makundi Maalumu katika Manispaa ya Bukoba, Murshid Issa anasema hakuna maombi ya kundi la watu wanaoishi na maambukizi ya VVU waliojitokeza tofauti na makundi mengine.

Anasema pamoja na kupoteza nafasi hiyo pia wanakosa nafasi ya kupata matibabu bure kwa kutojiunga na Bima ya Afya ya Jamii (CHF) ili wapate bure dawa za magonjwa nyemelezi tofauti na sasa wanapolazimika kuyanunua.

Kwa wenye maambukizi kutojiunga na vikundi wanaikosa nafasi ya kunufaika na asilimia kumi ambazo hutengwa na halmashauri za wilaya kutoka kwenye mapato yao kwa ajili ya kukopesha makundi mbalimbali katika eneo lake.Mwanamke akinywa dawa baada ya kupewa maelekezo na wataalamu namna ya kuishi na virusi vya ukimwi. ( Picha na Usaid/Spring-Unicef IYCF).

Mhudumu wa afya akichukua sampuli ya damu ya mteja wake kwa ajili ya kupima maambukizi. ( Picha na Usaid/Spring-Unicef IYCF)

UMEZAJI WA DAWA KWA WATOTO

Kundi la watoto pia limethirika kwa maambukzi ya virusi vya Ukimwi. Kama walivyo watu wazima, watoto wenye maambukizo ya VVU pia wanatakiwa kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo na kupata haki zote kama walivyo watoto wengine. Hata hivyo, baadhi ya familia zimeshindwa kuwaweka wazi watoto wao kuhusu maambukizi waliyo nayo na badala yake, familia hizo zinawaanzishia matibabu bila kuwaeleza ukweli na hali hali halisi jambo linalotajwa kuibua maswali baadaye watoto hao wanapokuwa wakubwa.

Mjadala uliibuka kuwa ni wakati gani wa kutenga muda wa kuongea na mtoto na kumueleza ukweli kuhusu maambukizi ya VVU aliyonayo huku ukitarajia mtoto huyo kuanza kuibua maswali akihoji sehemu alipopata maambukizi. Hata hivyo jambo hilo siyo zito kwa Safina Migeyo mwenye watoto wawili walioambukizwa VVU.

Anasema baada ya kujitambua ana maambukizi, alianza kutumia dawa huku akiwaweka wazi watoto wake.

“Nina watoto watatu, lakini wawili wana maambukizi ya VVU; niliwaeleza na dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi zinakaa mezani kilammoja anajua na wote wanaona ni jambo la kawaida na wanafuata ratiba ya kumeza dawa,” anasema Safina.

Anasema ni hatari kumuanzishia mtoto dawa ya kufubaza VVU, bila kumwambia sababu ya kumpa dawa hizo hali aliyosema inaweza kumjengea ukatili na mazingira ya kulipiza kisasi ikiwa atapata taarifa za hali yake ukubwani jambo ambalo siyo sahihi.

Safina anashauri wazazi kuwaweka wazi watoto wao na kuwaeleza umuhimu wa kutumia dawa hizo kwa kuwaeleza kuwa, watakuwa na afya njema kuzidi hata hao wengine wanaodhani hawana maambukizi ya ugonjwa huo endapo watazingatia na kufuata taratibu na matakwa sahihi ya dawa hizo.

Anaonya kuwa siyo jambo jema mtoto kuuliza sababu ya kupewa dawa kila siku na kuendelea kumficha kwa kumtajia ugonjwa mwingine kwani hali hiyo itamshitua na kumweka katika hatari ya uwezekano wa kuchukua uamuzi mbaya baada ya kujua ukweli kuhusu afya yake.

“Mzazi akimjulisha mapema mtoto wake kuhusu maambukizi aliyo nayo, atawasaidia hata walimu shuleni kutompangia kazi ngumu na hata kuheshimu ratiba yake ya kunywa dawa za kufubaza virusi,” anasema.

BUKOBA BILA UKIMWI

Juhudi za kuwakutanisha wananchi wanaoishi na virus vya Ukimwi ni mwendelezo wa jitihada za Serikali na wadau mbalimbali wanaoendesha mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Matokeo yanayotegemewa kutokana na jitihada hizo ni kuwa na Bukoba isiyokuwa na maambukizi ya Ukimwi huku wale ambao tayari wako katika hali hiyo, wakifurahia mazingira rafiki na kushiriki shughuli za uzalishaji kwa ajili ya familia zao na taifa kwa jumla.

Ofisa wa UNAIDS aliyesikiliza changamoto za kundi hilo, Catherine Spring, anasema ndoto ya kuwa na Bukoba bila maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi inawezekana na mipango yao ni kupambana na ongezeko la maambukizi.

Anasema Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayokabiliwa na changamoto ya maambukizi ya virusi vya ukimwi huku akishangaa kuendelea kuwepo kwa unyanyapaa kwa watu waliojitangaza kuathirika.

Ofisa kutoka Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virus vya Ukimwi, Gregory Kamugisha anasema hii ni hatua ya awali ya kuwafikia walengwa na kusikia maoni yao kazi ambayo pia imefanyika katika mikoa ya Songwe na Katavi.

Anasema sehemu kubwa ya changamoto zilizotajwa na kundi hilo zinahusu malalamiko ambayo kwa upande wa pili yanachangiwa na uelewa mdogo kuhusu sera na kanuni ambazo hazifahamiki vyema kwa walengwa.

Kwamba, unahitajika mjadala wa kitaifa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wenye jukumu la kutunga na kusimamia sera zinazohusu watu wenye VVU na kuwa hatua ya kulifikia kundi hilo katika maeneo yao inasaidia kujua uhalisia wa mambo.

Mjadiliano ngazi ya taifa pamoja na mambo mengine pia yanatarajiwa kuja na ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayolalamikiwa ikiwa ni pamoja na changamoto za kisheria na unyanyapaa katika ajira na umiliki wa mali hasa kwa wanawake wajane wanaoishi na VVU.

Watu mbalimbali wakiwamo watalaamu wa afya wanasisitiza watu wanaoishi na virusi vya ukimwi au basi wenye maambukizi, kuendelea kuzingatia umuhimu wa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa na maelekezo mengine kwani kwa sasa kuishi na VVU siyo tatizo kwa wanaofuata ushauri tiba.

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi