loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

GGML inavyoshiriki kutokomeza corona

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi 16, mwaka huu, kumekuwa na jitihada za serikali, wadau na wananchi kwa jumla katika kudhibiti virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid- 19).

Ni dhahiri kuwa janga hili ambalo sasa limetikisa nchi 212 duniani, limetokea katika kipindi ambacho Tanzania ilikuwa katika mwendokasi wa kupiga hatua kimaendeleo, lakini kutokana na janga hili sasa nguvu ya pamoja inahitajika ili kutetea uhai wa Watanzania kwani tayari limesababisha zaidi vifo 300,000 duniani.

Misaada imetolewa ikiwamo fedha ili kuunga mkono jitihada hizo za serikali, pamoja na kampuni nyingine, kwa upande wake Kampuni ya Uchimbaji wa madini Geita (GGML), ni mojawapo ya wadau waliotenga Sh bilioni 1.6 katika kudhibiti maambukizi hayo.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 1.1 tayari zimeelekezwa kwenye mfuko maalumu wa kushughulikia maambukizi hayo ya virusi vya corona, ilihali kiasi kilichobakia kimeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ambayo kampuni hiyo imeanza kuitekeleza.

VIFAA VYA KUNAWIA MIKONO

Mojawapo ya mikakati hiyo ni pamoja na ununuzi wa matangi 10 yenye ujazo wa lita 1,000 kila moja yaliyowekwa sehemu za wazi katika mji wa Geita ili kuwawezesha wananchi kuosha mikono.

GGML pia imetoa kimiminika cha klorini ambacho kitatumika kutakasa mikono badala ya sabuni. Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Wayne Louw anasema mpango huo pia uliwezeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mjini Geita (GEUWASA) ambayo imetoa maji kila mara ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inapatikana kwa umma wakatiwote.

Matangi hayo ambayo ni sehemu ya usambazaji wa msaada huo yamewekwa katika maeneo ya Kituo cha mabasi (2), Kituo cha Mwatulole (1), Kituo cha Shilabela (1), Kituo cha Nyankumbuko (1), Soko la Nyankumbuko (1), Hospitali ya Geita (1), Soko la Dhahabu (2), na kituo cha Moyo watoto yatima cha Huruma (1).

Akizungumza wakati wa uwekaji wa matangi hayo, Ofisa wa Afya wa Mji wa Geita, Masesa Japheth anaishukuru GGML kwa msaada huo. Anasema vifaa hivyo vitapunguza visingizio vya watu kutoosha mikono yao kila mara kwa sababu mtu haitaji tena kuwa nyumbani ndipo aoshe mikono.

“Nawahimiza kila mtu asione msaada huu kama mzaha. Ni wazi, vifaa hivi vimekuja kwa gharama kubwa. Lazima tuoneshe kwamba tunathamini juhudi za washirika wetu wa maendeleo kwa kuhakikisha tunabaki salama hata baada ya janga hili kuisha. Wote tuitumie vizuri huduma hii,” anasema.

Anaahidi kuwa, Halmashauri ya Mji wa Geita itachagua msimamizi mmoja wa mradi huo atakayehakikisha kuwa wakati wote matangi hayo yanajazwa na kuwekwa dawa hiyo ya Klorini ili kutibu maji hayo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma, Adelberra Mukure anaelezea namna kituo hicho chenye watoto 168 kilivyokuwa kinajitahidi kuhakikisha wakazi wote wanapata vifaa vya kuosha mikono vinavyoendana na mazingira yao.

“Tumeweka ndoo chache za lita 20 kwa jili ya kuosha mikono kama mlivyoona, lakini hazikutosha. Tunajua jinsi watoto walivyo na michezo mingi. Wanahitaji kuosha mikono yao mara kwa mara kuliko watu wazima.”

Mukure anaongeza: “Vyombo vya lita 20 ni vidogo sana kuwahudumia, ndiyo maana kulikuwa na foleni ndefu za watoto wakisubiri kuosha mikono yao, hali ambayo pia ilikuwa inalazimu pawepo na mtu mmoja wa kusimamia na kujaza maji kila mara.”

“Tangi hili la lita 1,000 ni msaada mkubwa kwetu. Tunashukuru sana GGML na washirika wengine kwa kutufikiria pia katika msaada huu. Huu ni wakati wa janga. Wakati ambao kila mtu ana hitaji lake, msaada wa GGML unadhihirisha kuwa rafiki akusaidiaye wakati wa shida ndiye rafiki wa kweli. Tunashukuru sana kwa msaada huu, “anasema.

Aidha, Louw anasema kampuni hiyo iko katika mchakato wa ununuzi wa vifaa vya matibabu ambavyo vitatolewa kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya matumizi mbalimbali na vifaa vingine kwa ajili ya upimaji na kwenye maeneo yaliyotengwa kwa karantini.

Aidha, Makamu Rais, Maendeleo Endelevu GGML, Simon Shayo anasema mbali na vifaa hivyo, pia GGML imezindua mikakati ya kujenga uelewa juu ya janga hili kwa jamii zinazozunguka mgodi.

Anasema GGML imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye taarifa za virusi vya corona ndani na nje ya mgodi.

“Vilevile kwa kupitia vyombo vya habari, GGML imeingia ubia na Kituo cha Redio cha Rubondo Fm kinachomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kuelimisha juu ya janga la Covid-19,”anasema.

Anasema lengo la mikakati hiyo ni kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya janga hili ambalo limekwamisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“GGML inagharamia uandaaji wa tangazo na kituo cha Rubondo Fm kitatoa mchango wake kwa kurusha tangazo hilo bila malipo,” anasema.

Kituo cha Rubondo Fm kilianzishwa kwa ufadhili wa GGML chini ya mpango wa uwajibikaji kwa jamii wa kampuni hiyo.

WAZIRI UMMY

Aidha, kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anatoa mwito kwa viwanda vya ndani kuchangamkia fursa za uzalishaji wa vifaa tiba na kinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kutokana na fedha zinazochangwa na kampuni mbalimbali nchini.

Ummy anasema Sh bilioni 1.1 zilizotolewa na GGML zinatumika katika mapambano dhidi ya virusi hivyo, ikiwamo ununuzi wa barakao, vifaa tiba vingine hivyo ni fursa muhimu kwa kampuni na wawekezaji waliopo nchini kuchangamkia fursa za kutengeneza wa vifaa tiba vinavyotumika sasa kudhibiti ugonjwa huo.

Waziri huyo wa afya anasema serikali inaendelea kuthamini msaada mkubwa unaotolewa na wadau hao katika kuonesha jitihada za kuwalinda watumishi wa afya walio mstari wa mbele kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

“Niwaombe wadau wanaotoa misaada kutoka nje ya nchi, kuzingatia muongozo wa upokea wa dawa na vifaa tiba kwa kuhakiki ubora. Tutaendelea kuelekeza TMDA, kuhakikisha wanaongeza umakini na uhakiki ubora na usalama,” anasema na kufafanua kuwa, hii ni kwa kuwa kumekuwa na wimbi la uingizaji wa vifaa tiba hivyo lazima kuhakikisha na kuwa na uhakika kuwa, vifaa hjivyo ni salama na vinakidhi vigezo vya ubora vinavyohitajika.

“Pia natoa wito kwa viwanda vya ndani kwamba tunahitaji sana barakoa, PPE, sanitiza, tungependa sana hela hii ielekezwe kununua vifaa vinavyozalishwa ndani ya nchi, mfano barakoa za ndani ya nchi, kuna kiwanda Pugu, lakini uwezo bado mdogo,” anasema.

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi