loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nchi EAC ziimarishe uhusiano kikanda

HIVI karibuni wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi alizungumzia kwa kina uhusiano wa Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

Miongoni mwa mambo aliyozungumzia ni uhusiano baina ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo alisema ni mzuri na unazidi kuimarika.

Katika hotuba yake, Profesa Kabudi alizungumzia pia madai ya kuwepo kwa vikao vya EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), vinavyodaiwa kufanywa bila kumshirikisha Rais Dk John Magufuli, ikidaiwa kuwa ni kutokana na uhusiano kuzorota.

Waziri Kabudi alifafanua kuwa vikao vilivyofanyika hivi karibuni na kuwahusisha baadhi ya wakuu wa nchi za EAC na SADC, havikuwa vikao vya kijumuiya, bali vya majirani waliokuwa wanazungumzia mambo yao ya ujirani.

Aidha, kupitia hadhara hiyo, Kabudi alitoa rai muhimu kwa wananchi wa EAC na SADC, kutoruhusu mahasimu wa nje kuzitingisha jumuiya hizo za kikanda.

Kwa namna Waziri Kabudi alivyoelezea masuala mbalimbali ya uhusiano na ushirikiano, ni ukweli ulio bayana kwamba uhusiano baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani, ni imara na unazidi kuimarika siku hadi siku.

Aidha, hivi karibuni Rais Magufuli akizungumzia uhusiano baina ya Tanzania na mataifa ya Afrika Mashariki, pia alisisitiza kuwa uhusiano ni imara na kwamba mataifa ya Afrika Mashariki, hayana sababu za kuzozana wala kuhitilafiana.

Kwa dhati kabisa tunaipongeza serikali na taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa jitihada mbalimbali wanazoendelea kuchukua katika kuhakikisha kuwa uhusiano baina yetu na mataifa mbalimbali unazidi kuimarika.

Mataifa jirani na hata ambayo hayapo jirani, yanapaswa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa yanalinda uhusiano uliopo ili usiingie doa, kwani inawezekana kabisa wapo maadui, ambao hawataki kuona uhusiano huo unazidi kuimarika.

Aidha mataifa rafiki yakiwemo yaliyopo ndani ya EAC, wanapaswa kufahamu pia kuwa uhusiano mzuri au urafiki uliopo, si daraja kwa nchi moja kuingilia mambo ya ndani ya taifa lingine kwa sababu yoyote ile, kwani kufanya hivyo ni kujaribu kutafuta chokochoko, lakini pia ni kuvunja masharti ya Mkataba wa Vienna kuhusu masuala ya diplomasia.

Tumeshuhudia katika siku za hivi karibuni, nchi zikitofautiana kutokana na kila moja, kutumia mbinu zake katika kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Lakini, ni wazi kuwa ugonjwa wa corona utapita, lakini nchi zitabaki palepale.

Ni kutokana na sababu hizo na nyingine nyingi, ndio maana tunazishauri nchi mbalimbali hususani za EAC, kuendelea kuimarisha uhusiano wa kikanda, ili kuifanya jumuiya hiyo kuendelea kupata mafanikio makubwa zaidi.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi