loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tangawizi ilivyokuza uchumi Madaba

“TANGAWIZI imetutajirisha; maisha yetu yamebadilika na hata nyumba zetu zilizopo Mkongotema na Magingo ni za kisasa na zina thamani kubwa… Huwezi kuamini kuwa zipo vijijini na ni kutokana na kilimo cha tangawizi kwani katika ekari moja, unaweza kutoa tani 7-10 hivyo kujipatia pesa nyingi.”

Ndivyo anavyosema mmoja wa wakulima wa tangawizi wa Madaba mkoani Ruvuma, Remigius Ngunja akimshukuru Joseph Mhagama anaposisitiza kuwa, mafanikio ya wakulima wa tangawizi Madaba, yametokana na juhudi na maono ya Mhagama aliyewaunganisha katika vikundi.

Joseph Mhagama ni Mbunge wa Madaba Mkoani Ruvuma.

Amejipatia umaarufu na heshima kubwa mkoani Ruvuma kutokana na ushawishi alioufanya na kufanikiwa kuwaunganisha wakulima wa tangawizi katika vikundi na sasa wengi wamenufaika na kuuza zao hilo kwa tija.

Kimsingi, Nguja anasema awali katika kilimo chake cha zao hilo, alikuwa anapata kati ya Sh 5,000,000 na 6,000,000, lakini baada ya kujiunga katika vikundi na Mhagama kuwasaidia kupata mbegu bora na kutilia maanani kilimo bora, sasa anapata kati ya Sh 8,000,000 hadi 10,000,000 kwa ekari.

Kwa mujibu wa mkulima huyo, baada ya msukomo huo kutoka kwa mbunge wao, amefanikiwa kujenga nyumba ya kulala wageni pia nyumba ya kuishi yenye thamani ya milioni 80 huku kilimo hicho kikimwezesha kununua gari aina ya ‘canter’ anayoitumia sasa kusafirishia mazao yake kutoka shambani na kuokoa pesa nyingi ambazo angetumia kukodi gari kwa hiyo.

Anasema awali, alikuwa akikodi gari kwa kati ya Sh 100,000 na Sh 120,000. Anasema gari inabeba gunia 20, hivyo ukiwa na magunia 100 utalazimika kutumia takriban Sh 600,000 kiasi anachosema sasa anakiokoa na kwamba, hali hiyo imemwezesha kufungua duka la jumla na duka la rejareja hivyo kujiongezea kipato.

Mkulima huyo anakiri kuwa, zao la tangawizi lina soko zuri ukilinganisha na mazao mengine, hasa katika msimu wa kuanzia mwezi Agosti hadi Desemba linapouzwa kwa kati ya Sh 2500 hadi Sh 3000 kwa kilo.

Anawashauri wakulima kuzalisha zao hilo kitaalamu na kutafuta masoko kwani bei kijijini hapo inasuasua ndiyo maana yeye husafirisha mazao yake kwenda Mbeya au Malawi ili kuongeza kipato.

“Tangawizi ina soko sana, lakini hupaswi kukurupuka kuuza maana utauza kwa hasara. Mfano, msimu umeanza; wapo wanaouza hadi Sh 850 kwa kilo, lakini sisi wengone tunatulia muda wetu ni mwezi Agosti tunapouza kwa bei tunayoitaka maana tangawizi haiozi,” anasema mkulima huyo.

Mkulima mwingine wa Kijiji cha Magingo, Enock Njiwa, anasema soko kubwa la zao hilo wanalolima sasa kwa ufanisi baada ya kuunganishwa katika vikundi lipo katika nchi jirani za Zambia na Malawi.

“Kutokana na watu wengi sasa kuhitaji tangawizi kwa wingi ili iwasaidie katika mapambano ya madhara yatokanayo na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19), ninaamini mwaka huu bei itapaa zaidi…,” anasema Njiwa.

Kwa mujibu wa mkulima huyu, soko lingine kubwa la zao hili lipo Dar es Salaam, Iringa, Songea, Dodoma na Mbeya.

Anabainisha kuwa, wakulima wananufaika na zao hilo la biashara kwani limekuwa mkombozi wao kiuchumi kuliko mazao kama mahindi na maharage ambahyo nayo ni muhimu kwao.

“Ukilima na kuhudumia vizuri ekari moja ya tangawizi, unapata mpaka tani 8 ambazo ukiuza, unapata zaidi ya Sh 27 milioni. Ndiyo maana tangawizi imenifanya niweze kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kujipatia kipato cha kuendesha maisha ya kila siku,” anasema Njiwa.

Kadhalika anasema: “Yote haya, tunamshukuru sana mbunge wetu Joseph Mhaga kwa kutupatia mbegu, wataalam na vitini vya kilimo cha tangawizi. Kwa kweli ametujengea uwezo na kutufanya tuzalishe kwa wingi kwani shina moja la tangawizi linawezoa kuzaa hadi kilo mbili za tangawizi kama imehudumiwa vizuri na haihitaji kuwekewa mbolea.”

Anaongeza: “Uzuri wa tangawizi, ni zao la uhakika tofauti na mazao mengine kama viazi au maharage; changamoto yake ni kung’olea majani tu, ili yasizidi… Mteja akihitaji kununua tunapatana, anaingiza pesa kwenye akaunti ndipo naenda kumchimbia tani anazohitaji na hii biashara yetu haiozi.”

Maria Luoga, Mkazi wa Madaba anasem, anaamini ubunge wa Joseph Mhagama umeacha alama kwani jitihada alizofanya ndizo zilimfanya apate nafasi hiyo kwani akiwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la Kiserikali la RUCODIA lililopo mkoani Ruvuma, alijitoa kwa hali na mali kusaidia Wakulima wa mkoani Ruvuma na mikoa mingine nchini. Kwa upande wa Madaba, mara kwa mara aliwaelekeza namna ya kuendesha kilimo bora cha tangawizi.

“Naamini kujitoa kwake ndiKo kumetufikisha hapa tulipo leo, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha jambo analotaka linafanikiwa kwa vitendo; ametuhamasisha tulime tangawizi na akatusambazia mbegu bora bure na kituo kutoa elimu. Kwa kweli tunashukuru sana kwa upendo wake maana anajitolea sana kwa ajili ya wananchi,” anasema Maria.

Anaiomba serikali kuwa karibu nao zaidi ili kuongeza thamani ya zao hilo na kutafuta soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Ofisa Kilimo Halmashauri ya Madaba, Joseph Mrimi anasema, halmashauri hiyo ina wakulima 256 wa tangawizi na malengo ya uzalishaji ni tani 1133 katika eneo la ekari 288.2 zilizolimwa.

Anasema halmashauri kupitia Siku ya Fursa za Uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma na Maonesho ya Nanenane Kanda Mbeya, wametangaza fursa za uwekezaji katika kilimo cha tangawizi katika eneo lao.

Anasema: “Tunategemea soko la ndani ya nchi hasa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya kama wanunuzi wakuu wa tangawizi yetu.”

Mrimi anaitaja mikakati ya kuongeza uzalishaji na wasindikaji wa tangawizi akisema halmashauri yake imetenga ekari 400 za ujenzi wa viwanda kwa ajili ya mazao ya kilimo. “Mkakati mwingine,” anasema:

“Ni kushirikiana na taasisi SAGCOT kutafuta masoko ya nje kwani kupitia wao, tumempata mdau ambaye ni Kampuni ya Tanzanice kwa ajili ya kuboresha tangawizi yetu ili kuuza katika masoko ya Ulaya.

Mkakati mwingine ni kushirikiana na taasisi mbalimbali na wakulima kuendeleza zao la tangawizi.

Anazitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni pamoja n RUCODIA, Vyama vya msingi (AMCOS), SAGCOT, TAMA na shirika linalojishugulisha na wakulima la NOJEPACO. Ofisa Kilimo huyo anawashauri wakulima kuendelea kulima tangawizi kwa wingi kwani zao hilo limeonesha uwezo na fursa kubwa ya kuwainua kiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba, Shafi Mpenda anakiri kuwa Mbunge huyo ana. mchango mkubwa katika kilimo cha tangawizi mkoani Ruvuma.

“Nakumbuka wakati nafika hapa mwaka 2016, tayari Mbunge (Mhagama) alikuwa amefanya uhamasishaji mkubwa wa zao hili na wananchi wakamuelewa,” anasema.

Aidha,amekuwa msaada mkubwa katika kuwatafutia masoko wakulima kwa kushirikiana na halmashauri Mpenda anasema Halmashauri inanufaika na kilimo cha zao hilo ambalo ni la kipekee kwa halmashauri linaloitambulisha halmashauri na limesaidia halmashauri kukusanya mapato zaidi yanayosaidia kutekeleza mipango mbalimbali ya halmashauri.

ASEMAVYO MBUNGE MHAGAMA

Mbunge Joseph Mhagama anasema wakati anafanya juhudi za kuwaunganisha wakulima katika vikundi, wengi hawakumwelewa na hivyo, ilikuwa ni kazi ngumu iliyoitaji muda mwingi na kujitoa sana kuwafuata wananchi vijijini.

“Nilikuwa ninawasisitiza wakulima wa tangawizi wajiunge katika vikundi ili wawe na umoja utakaowawezesha kupata huduma muhimu kama kusaidiwa kupata mbegu bora na masoko ya uhakika,” anasema Mbunge huyo wa Madaba.

 Anaongeza: “Leo hii wakulima wanazidi kunufaika kwa kuondokana na umaskini kwa kupata fursa za kuongeza mitaji kwa kuanzisha biashara mbalimbali nami najitahidi kuwawakilisha kwa nguvu, uwezo na moyo wangu wote kama kinavyosisitiza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli...”

Mhagama anakiri akisema: “Mkakati wa kupunguza umaskini katika Jimbo la Madaba umefanikiwa baada ya kuanzisha kilimo cha tangawizi na kupitia zao hilo, wananchi wengi hasa wakulima wa tangawizi na wadau wa zao hilo, wamejenga nyumba bora za kisasa, kusomesha watoto wao na kupata pesa za kuendesha maisha yao na hata wengine wamenunua vyombo vya usafiri.”

Anafahamisha akisema kuwa, zao la tangawizi liliingia Madaba yapata mwaka 2011. “Baada ya kujiridhisha kuwa linaweza kuwa na mchango mkubwa kwa kipato cha wananchi, nilitafuta ufadhili toka Belgium Technical Cooperation (BTC)kwa kushirikiana na asasi ya RUCODIA katika jitihada hizo, wakulima 300 walijengewa uwezo kuzalisha zao hili.

“Kazi ya kugawa mbegu na utafutaji masoko ilifanywa kwa ufanisi mkubwa na asasi ya RUCODIA. Kipindi hiki nimepanua wigo wa uzalishaji kwa kuchangia na kusambaza mbegu za tangawizi zenye thamani ya Sh 21,000,000,” anasema Mhagama.

Usambazaji huu ulifanyika Novemba 30, 2015 katika vijiji vya Mtyangimbole, Mbangamawe, Ngadinda, Ndelenyuma, Lutukila, Mkongotema, Mahanje, Lituta, Matetereka, Lilondo, Maweso, Igawisenga, Wino, Ifinga na Nagingo.

Mbunge huyo wa Madaba anasema: “Zao hili sasa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Madaba na Ruvuma kwa jumla kwani linachangia kipato cha wananchi mmoja mmoja na katika kipindi hiki, mchango wangu binafsi kama mbunge ni Sh 21,000,000.”

SABABU ZA JUHUDI HIZO

Mhagama anasema aliguswa na kusukumwa kuwasaidia wananchi wa madaba kwa kuwapa mbegu bure za tangawizi, Elimu na kuwahamasisha nanma ya kulima kitaalam zao la tangawizi ili wainue vipato vyao kwani walikuwa na wigo finyu wa mazao ya biashara. Anasema wananchi wengi walikuwa wanategemea mahindi na maharage, na maeneo mengine mpunga na alizeti kidogo. “Nikaona nihamasishe zao jipya mbadala la kipato na nianze na tangawizi…

Nafurahi kuona nimesaidia na kutengeneza wafanyabiashara wakubwa kupitia zao la tangawizi,” anasema na kuongeza: “Mwanzoni soko lilikuwa gumu sana na wakulima wengi walipata hasara. Ndipo nikatafuta ufadhiri kwa ajili ya kutafuta masoko, tukaitangaza tangawizi ndani na nje ya nchi hadi soko likatengamaa na sasa soko liko imara.”

CHANGAMOTO ZILIZOPO

Anasema, changamoto kubwa ni ubora na mitaji midogo ya wakulima, hivyo wakulima wanapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo hai ili kulinda mazingira na afya ya mlaji.

“Lakini pia, tunakabiliwa na changamoto ya upotevu wa rutuba ya udongo, hali inayowashawishi baadhi ya wakulima kukiuka kanuni za matumizi ya mbolea na pia, maeneo yanayofaa kwa kilimo cha tangawizi yapo mbali, mkulima kulazimika kusafiri kitambo kirefu,” anasema Mbunge huyo.

Anatoa mwito akisema: “wakati tunatafura njia za kuikabili changamoto hizo kwa kutafuta wataalamu zaidi, wananchi waendelee kuchangamkiaa fursa zitokanazo na kilimo cha tangawizi kwani ni nyingi na kilimo hiki kina tija kwa uchumi wa mkulima mmoja mmoja, na taifa kwa jumla.”

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi