loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

COVID-19 unavyoweza kuathiri malengo ya Maendeleo Endelevu

MWAKA 2020 ni mwaka mwaka wa kuanza muongo wa miaka 10 ya mwisho ya Ajenda 2030 katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (MME) duniani kote.

Mipango ya kutekeleza MME imefanyika bila mpango wa dharura unaoweza kukabili janga ukubwa kama corona (Covid-19), ambalo linasababisha hasara kubwa kibiashara na kutishia uwepo wetu kiujumla.

Katibu Mkuu wa Asasi ya Umoja wa Mataifa-Tanzania (UNA Tanzania), Reynald Maeda, anasema mwishoni mwa Februari mwaka huu walikuwa Victoria Falls (Zimbabwe), kwenye mkutano wa sita wa ukanda Afrika kwa ajili ya Maendeleo Endelevu

“Tuliangalia ni jinsi gani Afrika inaendelea katika utekelezaji wa Agenda 2030 na Agenda 2063, na njia za kutekeleza ndani ya miaka 10 ya mwisho ya Agenda 2030,” anasema Maeda.

Anasema Tanzania inaendelea vizuri kuhusiana na uwajibikaji wa MME, kwa kuripoti kwa hiari maendeleo ya nchi kuhusiana na hatua zilizochukuliwa kufika malengo haya ya dunia kwa mwaka 2019.

Lakini anasema kwa sasa, karibu kila kitu duniani kote kimesimama. Mwelekeo wa dunia umechepukia kwenye kupunguza kasi ya janga la corona linalosababisha hasara kubwa, na kulazimika kuzoea mienendo mipya ya kufanya shughuli mbalimbali, huku umuhimu ukiwekwa kwenye kuokoa maisha. Sekta za MME zinazoathirika zaidi Mpaka sasa ripoti zinaonyesha kwamba duniani kote sekta karibu zote zimeshuka.

Kusitishwa kwa shughuli za kawaida na kufungia watu ndani zinaathiri tija na biashara kufungwa huku viwango vya ukosefu wa ajira vikizidi kuongezeka duniani kote. Makala haya hayatathmini sekta maalumu bali kuonesha baadhi ya MME zinazoweza kuathirika na janga la corona.

Kwa vile hili janga ni la kiafya, lengo namba tatu la Afya Bora na Ustawi ndio lengo linaloathirika kuliko mengine, lakini kwa tabia ya MME lengo moja likiathirika linaathiri malengo yote 16 yaliyobaki.

Kwa malengo namba 1 na 2; Tokomeza umaskini na Tokomeza njaa, ukosefu wa fedha unaongeza idadi ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wakati ambao uzalishaji na usambazaji wa chakula unaweza kupungua hivyo kuathiri lishe kwa wale wasiojiweza.

Kuhusu lengo namba 3 la Afya bora na Ustawi ni kama ilivyokwishaelezwa kwamba linaathiri malengo yote. Lengo la nne kuhusu elimu bora limeathirika pia, hasa kwa jamii ambazo hazina miundombinu ya kusoma mtandaoni hivyo kuacha wanafunzi wengine nyuma.

Kuna taarifa kwamba viwango vya ukeketaji wa watoto wa kike, ajira na ndoa za utotoni vimeongezeka sehemu mbali mbali hata kwa hapa Tanzania kwa kuwa kufungwa kwa shule kunawapatia wazazi nafasi za kufanya vitendo hivi.

Lengo la tano la Usawa wa Kijinsia, ripoti kutoka UNFPA zinaonyesha ongezeko la unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa wanawake walio na wenza wakatili.

Kwa lengo la nane la Kazi zenye Staha; shughuli za kiuchumi zinasimamishwa, mapato yanakwenda chini huku kukiwa na ongezeko la viwango vya ukosefu wa ajira duniani pamoja na upunguzwaji kwa fedha katika tasnia mbali mbali.

Hali huii huathiri pia lengo namba 10. Lengo namba 16, kuhusu Amani, Haki na Taasisi Imara, nchi zenye migoro zitapata shida kukubali kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupambana na corona ambayo inasababisha hasara na athari kubwa kama zile tunazoona zikitokea nchi nyingine kama vile Afrika Kusini.

Tunaona ukatili unaofanywa na vyombo vya dola na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Hali hii inaweza kugeuka kuwa msingi wa rushwa na matumizi mabaya ya fedha zilizotengwa kwa lengo la kupambana na janga hili.

Lengo namba 17; Kushirikiana kwa ajili ya Malengo, kila nchi inakazana kupambana na janga hili makwao kwanza, wakijinusuru na kudorora kwa uchumi.

Ubadilishaji wa vipaumbele unaweza kutokea hasa kwenye nchi zinazotoa misaada, hali itakayoathiri juhudi zamaendeleo kwenye nchi zinazoendelea. Uchambuzi huu unaweza kufanywa kwa malengo mengine yote, kwani huu sio uchambuzi kamili.

Kuhusu vijana Ofisa Mawasiliano na uenezi wa UNA Tanzania, Godfrida Magubo anasema ingawa ripoti zinaonyesha kwamba corona haiwadhuru vijana kiafya kwa kiasi kikubwa, bado wanaathirika na athari zingine za janga hili kiuchumi kuliko makundi mengine.

Kuna sababu nyingi zinazoweza kuangamiza kundi hili kubwa kuliko mengine.

Mwaka 2019 Shirika la Wafanyakazi Duniani (ILO) lilikadiria kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kuwa asilimia12, hiki tayari ni kiwango kikubwa, hivyo ukiunganisha na athari corona kwenye uchumi wa dunia kunakosababisha kufungwa kwa viwanda, usafiri na kuyoyoma kwa biashara inaetegemewa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kuongezeka maradufu.

Biashara ndogo zinazoendeshwa na vijana zinaathrika na hivyo kuwa na changamoto kubwa kutafuta mtaji. Na katika mashirika mengi yakiwemo ya utalii na mahoteli, vijana wamekuwa hatarini kupata likizo isiyolipwa au kuachiwa kazi kabisa.

Kuna haja ya kutenga pesa maalumu zitakazookoa biashara ndogo zinazoendeshwa na vijana. Matumaini yaliopo ni uvumilivu wa vijana pamoja na uwezo wao wa kubuni na kupambana na hali zao kulingana na mazingira.

Licha ya kiwewe kinachotokana na janga hili, kuna fursa nyingi zinazojiambatanisha pia, kwa mfano ongezeko la biashara za mtandaoni, kwa vile maisha hayatorudi kuwa kawaida mia kwa mia, ni wakati mwafaka wa kubuni mienendo mipya ya maisha.

Nini kifanyike nchi zinazoendelea? UNA Tanzania wanasema kuwa hakuna kati yetu aliye salama asilimia 100, kwa hiyo ni jukumu la kila mmoja wetu kujikinga na kuwakinga wengine.

Katika nchi nyingi zinazoendelea, kuna shida ya mtiririko wa taarifa, upatikanaji wa habari sahihi kwa wakati ni changamoto kubwa.

Kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu corona kwa wakati na kuifikisha kwa watu wote itasaidia jamii kuwa makini zaidi na janga hili kwa maana ya kuchukua tahadhari zinazotakiwa. Hatuna budi kuwa na mpango mkakati katika kutafuta suluhisho la muda mfupi na mrefu. Kila mtu anapaswa kutoa mawazo yake na kufanyiwa kazi kuanzia sekta binafsi, asasi, wabia wa maendeleo, wanasayansi, sekta ya afya na serikali kuu.

Shauku kyubwa ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma hata katika nyakati ngumu. Ushauri Huu sio wakati wa kugawanyika. Tufanye kazi kwa pamoja kutafuta suluhisho la muda mfupi na mrefu.

Kuna dalili kubwa mienendo yetu haitarudi kuwa kama kawaida kwa muda mrefu kutoka sasa, mpaka suluhisho la kudumu kama chanjo au aina fulani ya tiba ipatakane.

Hii haimaanishi tukae na kusubiri, inabidi tuwe wajasiri, uwezo wetu wakupambana wakati wa shida kubwa unapimwa, shida zetu hazijapotea.

Bado kuna wasichana wengi wanolewa wakiwa na umri mdogo, vijana wengi bado wanakosa ajira, upatikanaji wa elimu bora bado ni changamoto na kadhalika.

Hatuna budi kuendelea kuzifanyia kazi changamoto hizi huku tukipambana na corona. Iwe serikali, azaki, sekta binafsi, wabia wa maendeleo na makundi mengine, sote tunapaswa kubeba jukumu la kujenga Tanzania bora na salama kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi