loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba waanza kambi

WACHEZAJI wa Simba jana walifanyiwa vipimo vya afya kabla ya kuanza kambi kwa ajili ya maandalizi ya kuendelea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2019/2020.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kuwa wachezaji walifanyiwa vipimo jana kwa ajili ya maandalizi ya ligi pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam, ambapo bingwa wake uliwakilisha taifa katika Kombe la Shirikisho barani Afrika.

“Wachezaji waliofika kambini walianza na kufanyiwa vipimo ili kujua afya zao kabla ya kuanza kwa programu nyingine.”

Alisema asilimia 95 ya wachezaji wote ukiacha watatu wa kigeni, Francis Kahata, Sharaf Shiboub na Clatous Chama ambao wamekwama kwenye nchi zao, tayari wamefanyiwa vipimo hivyo ambavyo ni muhimu kuelekea msimu huu wa ligi.

“Majibu ya vipimo hivyo kwa wachezaji yatatolewa na uongozi baada ya taratibu za kimaabara kukamilika,” alisema Rweyemamu.

Juzi Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza alitoa utaratibu wa kuanza kwa kambi hiyo, ikiwemo wachezaji wote kupimwa afya zao, huku akisisitiza kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanatetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara na kutwaa ubingwa wa Kombe la FA.

Naye kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema jana kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu katika kila mchezo kati ya hiyo 10 iliyobaki ili kumaliza wakiwa na pointi nyingi.

Simba kwa sasa wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 71 baada ya kucheza mechi 28 na kutengeneza tofauti ya pointi 17 dhidi ya Azam FC waliopo katika nafasi ya pili kwa pointi 54, huku mabingwa wa kihistoria Yanga wakishika nafasi ya tatu kwa alama 51.

Alisema hali ya hewa ni nzuri kwa Simba, hivyo wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mechi zao zilizobaki. Mechi zilizobaki za Ligi Kuu Tanzania Bara zitapigwa katika kituo kimoja cha Dar es Salaam kwenye viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex baada ya ligi kusimama tangu Machi 17, 2020 kutokana na virusi vya corona.

Matola alisema wako katika viwanja vya nyumbani, hivyo wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michezo yote iliyobaki kwani hali ya hewa wameizoea. Aidha, Matola alisema benchi la ufundi limepania kumtengeneza mshambuliaji wa kikosi hicho, Meddie Kagere anaendelea kufunga kwenye kila mchezo ili kuhakikisha anavunja rekodi ya mchezaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ anayeshikilia rekodi kwa kufunga mabao 26.

Kagere ambaye msimu uliopita alitwaa kiatu hicho cha dhahabu baada ya kufunga mabao 23, ndio kinara wa mabao msimu huu hadi sasa akiwa amefunga mabao 19, akihitaji mabao saba kuifikia rekodi ya `Mmachinga’.

Tayari Kagere amesema atawakosa mashabiki wao ambao hujitokeza kwa wingi uwanjani kwa sababu mashabiki hawataruhusiwa kuingia uwanjani ligi ikirejea Juni mwaka huu.

“Kitu cha kwanza ambacho tutakikosa ni mashabiki wetu ambao kila mechi wanajitokeza kwa wingi. Unapofunga bao halafu lile shangwe linalotoka jukwaani linafurahisha, lakini kutokana na janga hili la corona hakuna njia nyingine,” alisema Kagere.

Kagere alisema baada ya kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili bila mechi kuna kitu kitakuwa kimepungua, yaani utimamu wa mwili hivyo itawachukua michezo miwili au mitatu ili kuwafanya kuwa fiti hata kama walikuwa wanafanya mazoezi.

MITAA ya mji wa Ruangwa imepambwa kwa bendera za rangi ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi