loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jamii itumie teknolojia ya mawasiliano kuchagiza maendeleo

Baraza la Ushauri wa Watuamiaji wa Huduma za Mawasiliano Nchini (TCRA -CCC) jana liliingia makubaliano na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Nchini (Taboa), yanayolenga kuielimisha jamii matumizi bora ya huduma za mawasiliano.

Elimu hiyo itakuwa ikitolewa kwa njia ya video fupi za dakika 25. Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada zinazochukuliwa na baraza hilo katika kuhakikisha kuwa wananchi wanajua njia sahihi za mawasiliano na kuyatumia kwa faida.

Baraza hilo pia limekuwa likitoa elimu kwa vijana vyuoni na sekondari na sehemu nyinginezo ambazo zinawakutanisha vijana. Lakini, pia wazazi na walezi, wamenufaika na elimu ya mawasiliano.

Hatua iliyochukuliwa jana ya kuwafikia abiria kwa kuanza na mabasi 100 ya abiria kwenda na kutoka mikoani inatia moyo, hasa ikizingatiwa idadi kubwa ya wananchi ambao ni abiria itakavyofikiwa.

Chini ya mabasi hayo 100 ya awali, abiria watakaofikiwa ni 5,000 hadi 6,000 kwa siku. Idadi ya mabasi itakapofikia 450 hadi 500, idadi ya abiria itakayofikiwa itakuwa ni 20, 000 hadi 25,000 na lengo kwa kila mwezi ni kuwafikia abiria 550,000 hadi 600,000.

Binafsi licha ya kupongeza jitihada hizo za baraza chini ya Katibu Mtendaji wake, Mary Msuya, napenda kuwashauri wananchi waliokwishanufaika au watakaonufaika na elimu hiyo, kuitumia kuleta tija katika jamii.

Ni dhahiri kuwa teknolojia ya mawasiliano ikitumika vema, itabadilisha mambo mengi katika jamii, hasa kutokana na mfumo unaotumiwa wa utoaji wa taarifa muhimu za kukuza uchumi.

Hii ni hasa pale taarifa husika, zikichagiza maendeleo lengwa. Ni muda sasa kwa jamii kuwafichua watu wote wanaotumia mawasiliano kutapeli, kudhalilisha utu wa watu na kuhamasisha ukiukwaji wa maadili ya Kitanzania.

Kwa kuwa video fupi zitakazokuwa zikioneshwa kwenye mabasi hayo zinahusiana na sheria, miongozo na maadili ya matumizi ya mawasiliano, naona kuwa huo ni mwongozo mzuri wenye tija.

Kwa kuwa madereva wa mabasi, wao wamepewa jukumu la kuzionesha video hizo, basi wahakikishe kuwa wanazionesha kila siku ili elimu hiyo iwafikie abiria kwa ufasaha zaidi.

Mbinu hii ni nzuri, kwa kuwa kama abiria hao hawajawahi kupata wasaha wa kupata elimu hiyo mitaani, basi watakuwa wamefikiwa kwa njia hiyo wakiwa kama abiria.

Kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja wa utekelezwaji wa mradi huo, ni wazi kuwa idadi kubwa ya watu itakuwa imeelimishwa kwa undani zaidi. Na ili elimu hiyo ilete tija, basi ni vema na wao washiriki kuisambaza kwa jamii.

Kwa kuwa TCRA CCC imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, wananufaika na mawasiliano hayo, basi isichoke kuendelea kuwapigania watumiaji wa huduma za mawasiliano huku pia ikiwaonesha fursa, zinazoweza kupatikana kutokana na huduma hiyo nyeti.

MAAMBUKIZI ya virusi vya corona katika nchi za Jumuiya ya ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi