loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Pango la Habiba na vivutio lukuki wilayani Nanyumbu

MTWARA ni mkoa unaojivunia kuwa na maliasili nyingi na maeneo mengi yenye uoto wa asili, huku maeneo hayo yakiwa bado yanatunzwa na wazee wanaojua asili yake.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkoa wa Mtwara una misitu inayochukua asilimia 42.4 ya mkoa mzima na kati ya hiyo, asilimia 93.7 inahifadhiwa na Serikali Kuu.

Licha ya kuwa na vivutio vingi vya kihistoria vya utalii, bado Mkoa wa Mtwara unakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo za vivutio vingi kutotambulika rasmi, hivyo kuwa vigumu kwa jamii na wadau kupata taarifa sahihi mintarafu maeneo hayo.

Changamoto nyingine ni kutotangazwa ipasavyo kwa vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa huu na Kanda ya Kusini kwa jumla, kutohamasika kwa watalii wa ndani na wale wa nje kutembelea vivutio katika Kanda ya Kusini, na miundombinu duni ikilinganishwa na kanda nyingine ikiwamo Kanda wa Kaskazini.

Kimsingi, maeneo mengi hayajajengewa uwezo wa kuingiza pato ndani ya ukanda huu, ingawa yakiangaliwa na kuandaliwa vizuri, yanaweza kuokoa mkoa husika na kuingiza mapato makubwa zikiwmao fedha nyingi za kigeni.

Mbali na vivutio kama Shimo la Mungu lililopo wilayani Newala, mji wa kihistoria wa Mikindani, vivutio katika mji mkongwe wa Mgao na maajabu katika Wilaya ya Masasi, pia ipo Hifadhi ya Lukwika Lumesule ambayo ndani yake lipo Pango lenye historia kubwa katika Wilaya ya Nanyumbu.

Kwa mujibu wa machapisho kadhaa, Nanyumbu ni miongoni mwa wilaya chache nchini Tanzania zenye maeneo adimu ya kihistoria pamoja na vivutio vya kipekee vya utalii.

Wilaya hii iliyopo mkoani Mtwara ipo umbali wa kilomita 54 kutoka Masasi katika Barabara ya Mtwara - Songea. Nanyumbu ni wilaya inayopakana na Wilaya ya Nachingwea kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Masasi kwa upande wa Mashariki, nchi ya Msumbiji kwa upande wa Kusini na Wilaya ya Tunduru kwa upande wa Magharibi.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vikiwamo vya kimtandao, Pango la Habiba ni miongoni mwa vivutio vya kihistoria vinavyovuta hisia za watu wengi ndani na nje ya Wilaya ya Nanyumbu.

Pango hili lipo ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Lukwika Lumesule. Hili ni pango maarufu katika hifadhi hiyo ya wanyamapori. Pango hili pamoja na mwonekano wake wa kipekee, pia huwa msaada mkubwa kwa binadamu na kwa wanyama pindi wapatapo matatizo.

Ipo hadithi kuwa, kuliwapo mwanamke aliyefahamika kwa jina la Habiba aliyepata msaada wa pango hilo wakati akiwakimbia watu waovu na baadaye, akatoka salama mikononi mwao.

Hii ndiyo asili ya jina la ‘Pango la Habiba’. Ili kulitembelea Pango la Habiba, ni vizuri ukifahamu mambo kadhaa muhimu ya kihistoria, kama yalivyonukuliwa na baadhi ya machapisho ikiwemo tovuti rasmi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu.

Inasemekana kuwa, Hifadhi ya Wanyamapori ya Lukwika Lumesule inapakana na Kata ya Lumesule ambako ndiko lilikopiganwa pigano la mwisho la Vita vya Majimaji.

Zipo baadhi ya kumbukumbu katika Mlima Makong’ondera ikiwepo mifupa ya kale pamoja na mafuvu katika mapango yanayosadikiwa kuwa, huenda ni ya wapiganaji wa Vita vya Majimaji vilivyoongozwa na Kinjekitile Ngwale katika miaka ya 1905 hadi 1907.

Hifadhi ya Lukwika Lumesule hutenganishwa na Mto Ruvuma unaoigawa hifadhi hiyo upande wa Tanzania na Msumbiji. Serikali ya Tanzania kupitia mapato yake ya ndani ikishirikiana na Nchi ya Msumbiji, ilifanikiwa kujenga daraja la kisasa la Umoja katika eneo la Mtambaswala ambalo ni kivutio kingine kikubwa cha utalii katika Wilaya ya Nanyumbu.

Ofisi Uhusiano katika Daraja la Umoja Mtambaswala, Salum Lihame Mwamba Mwamba, ambaye pia ni Mtunza Kumbukumbu za Historia ya Daraja la Umoja Mtambaswala, anasimulia namna Wajerumani walivyofika hapo Mtambaswala wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) na namna vita ilivyopiganwa wakati Wajerumani wakitafuta njia ya kuvuka kwenda Msumbiji wakitokea Tanganyika.

Ukifika Mtambaswala utaoneshwa maeneo hayo ya kivita, lakini pia utafanikiwa kuifahamu vizuri historia ya utumwa na namna soko la Mkunazini Zanzibar lilivyofungwa na baadhi ya raia walioachwa huru walivyofika Mtambaswala.

Ukiwa Mtambaswala utafanikiwa pia kuliona daraja linalotembea pamoja na kuiona mbuga nzuri ya Lukwika Lumesule ambayo ndiyo hifadhi pekee inayoaminika kuwa tembo mkubwa kuliko wote katika eneo la Afrika Mashariki na Kati alipatikana humo.

Safari ya kuelekea kwenye Pango la Habiba huwafurahisha wengi kwani ukiwa njiani utapita katika Kijiji cha Nakopi kwenye Mlima Majeja. Inaelezwa kuwa, juu mlima huu kuna tumbaku ya ajabu na mtu yeyote anaruhusiwa kuvuta akiwa kule mlimani kwa masharti ya kutoondoka nayo kwani inasemekana kwamba ukijaribu kuondoka nayo lazima utapotea.

Mlima Majeja hufanana sana na ule wa Chitowe ambao unasemwa kuwa una pipa lisilofikika na pipa hilo lilikuwepo tangu kipindi cha ukoloni wa Mjerumani.

Miongoni mwa vivutio vingi vilivyopo wilayani Nanyumbu ni pamoja na Chemchem ya maji moto katika Mto Ruvuma katika Kitongoji cha Nangale kijijini Lukula. Maji haya ni ya moto yenye uwezo wa kuivisha mahindi. Aidha, ipo ardhi inayotikisika katika Kijiji cha Namatumbusi.

AMEJIPAMBANUA na vyama vya siasa, wanasiasa wasiotimiza ahadi. Amekwenda kinyume ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi