loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania na maadhimisho ya Siku ya Makumbusho Duniani kidijiti

Siku ya Makumbusho Duniani husherehekewa kila ifi kapo Mei 18 ambapo makumbusho zote duniani huadhimisha kwa kufanya shughuli mbalimbali za kupeleka makumbusho kwa jamii.

Sherehe hizo kwa kawaida huambatana na maandamano na shamrashamra na njonjo za kila namna. Katika siku hiyo makumbusho zote duniani zinakuwa wazi huku wanajamii wakiruhusiwa kuingia bila kutoa kiingilio ili kuona maonesho mbalimbali.

Mwaka huu hali imekuwa tofauti kwa sababu ya janga la ugonjwa wa Covid-19 ulioikumba dunia nzima. Kama moja ya njia ya kujikinga na ugonjwa huo, mikusanyiko ya watu hairuhusiwi na jamii inahimizwa kuwa na tahadhari ili kuepuka maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Makumbusho Duniani nchi nyingine zimefunga shughuli za kimakumbusho kwa muda ili kupisha janga la korona.

Makumbusho za Tanzania zinaendelea kufanya kazi huku zikizingatia maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto juu ya namna nzuri ya kujikinga dhidi ya corona.

Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeendelea kufanya majukumu yake ya utafiti, kukusanya na kuelimisha jamii kwa njia ya maonesho, semina na programu za kielimu juu ya masuala mbalimbali kuhusu urithi wa asili na utamaduni wa taifa ili kurithisha, kutoa elimu na kuburudisha jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Makumbusho Duniani yalianzishwa na Baraza la Makumbusho Duniani (International Council of Museums – ICOM) mwaka 1977 ili kujenga uelewa kwa jamii kwamba, makumbusho ni taasisi muhimu kwa nchi inayohifadhi urithi wa asili na utamaduni na jamii kubadilishana utamaduni hai.

Maadhimisho hayo yanaonesha kwamba makumbusho zina nguvu za kuleta utengamano wa jamii na kujenga umoja wa kitaifa, uzalendo na kufanya watu kuelewana zaidi, kuthamini na kuhifadhi urithi wa asili na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2020 ni: “Makumbusho kwa Usawa: Anuai na Ushirikishwaji.”

Kwa Kiingereza kaulimbiu hiyo inasema,: “Museum for Equality: Diversity and Inclusion.” Tanzania imeungana na nchi ningine duniani kuadhimisha Siku ya Makumbusho Duniani. Makumbusho ya Taifa imeonesha inavyotekeleza maelekezo ya serikali kupitia Wizara ya Afya na yale ya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kupambana na corona kupitia onesho la mtandaoni liitwalo “Makumbusho ni Salama.”

Onesho hilo lililozinduliwa siku hiyo, linaonesha namna Taasisi ya Makumbusho ya Taifa ilivyojizatiti kuhakikisha kila anayeitembelea anakuwa salama. Katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Lwoga anasema japokuwa kuna ugonjwa wa Covid-19, makumbusho zote zinaendelea kufanyakazi, lakini tahadhari kubwa imewekwa ili kuwakinga watumishi wa makumbusho hizo na wageni wanaozitembelea.

“Tumechukua kila tahadhari kulingana na maelekezo ya Wizara ya Afya kuhakikisha kila mgeni anayetembelea makumbusho zetu anaingia na kutoka akiwa salama,” anasema Dk Lwoga. Kulingana na onesho hilo hakuna mgeni anayeruhusiwa kuingia makumbusho bila kuwa na barakoa na akiingia tu, anapimwa joto ili kujua hali ya afya yake.

Anatakiwa kunawa mikono na sabuni na maji yanayotiririka au kutumia vitakasa mikono (sanitizer) huduma ambazo zipo katika kila mlango wa kuingilia na kutoka makumbusho.

Lengo la kutengeneza onesho la kidigitali ni kuhakikisha ujumbe unawafikia watu wote si wale tu wanaoweza kutembelea makumbusho zetu, bali hata walio nje ya nchi ili wajue Makumbusho ni salama, anasema Mkuu wa Idara ya Programu, Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Dar es Salaam, Ezekiel Chance.

Anasema wananchi wanaweza kutembelea makumbusho zetu zote bila kuwa na wasiwasi kwa sababu taasisi imechukua kila hatua stahiki kuhakikisha kuna usalama wa kutosha. Kama sehemu ya maadhimisho hayo, Kijiji cha Makumbusho kilichoko eneo la Kijitonyama jijini Dar es Salaam kiliandaa onesho la mila na tiba asili.

Wanajamii kutoka makabila ya Wamakonde na Wafipa walionesha namna tiba za asili zilivyotumika kutibu magonjwa mbalimbali. Onesho hilo lililokuwa mubashara katika mitandao ya kijamii ya instagram, facebook na youtube lilionesha majani yanayotumika kujifukiza na namna ya kujifukiza kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo mafua makali, kichwa na tumbo.

Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Dk Gwakisa Kamatula, anasema Kijiji cha Makumbusho kina hazina kubwa ya urithi wa utamaduni. Ukiachilia mbali uhifadhi wa nyumba za asili za jamii mbalimbali za Tanzania, Kijiji cha Makumbusho kinahifadhi msitu wa asili wenye ukubwa wa takribani heka tano wenye miti na mimea mbalimbali inayoweza kutumika kwa tiba asili.

“Tupo hapa ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi mazuri ya tiba asili hususan katika kujifukiza,” anasema Dk Kamatula. Bibi Mary Mangazini wa Kabila la Wafipa anasema, katika jamii yao kujifukiza siyo suala geni kwani hutumika sana kwa magonjwa mbalimbali kwa kutumia hasa majani ya mwarubaini, tangawizi pori, mpera, mkaratusi na mingine.

Anasema majani hayo huchemshwa kwa pamoja kwenye chungu kwa muda wa dakika 20 kisha, huipuliwa. Mgonjwa hufunikwa shuka au blanketi kulingana na uzito wa mgonjwa. Wananchi wanaweza kutembelea makumbusho zetu zote bila kuwa na wasiwasi kwa sababu taasisi imechukua kila hatua stahiki kuhakikisha kuna usalama wa kutosha.

“Mgonjwa akiwa mnene anatakiwa atumie nguo nzito zaidi ukilinganisha na mtu mwembamba,” anasema Mangazini.

Anasema mgonjwa hujifukiza kwa dakika tano mpaka 10 kutegemea ukubwa wa tatizo lake.

“Tiba hii ni rahisi sana na baada ya kujifukiza, mgonjwa hupata nafuu au kupona kabisa,” anasema Mangazini.

Nayo Makumbusho ya MajiMaji Songea ilitumia maadhimisho hayo kuombea nchi dhidi ya ugonjwa wa Covid- 19. Baraza la Kimila la Songea kwa kushirikiana na wanajamii walifika katika kaburi la haraiki la mashujaa wa Vita vya MajiMaji kuiombea nchi dhidi ya corona.

Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha walitumia maadhimisho hayo kuzindua programu ya ushirikishwaji wa vijana kwenye makumbusho hususani kupitia vikundi vya vijana vya utazamaji na utalii wa ndege katika Mkoa wa Arusha.

Mkurugenzi wa Makumbusho ya Elimu Viumbe, Christine Ngereza anasema vijana ni kundi muhimu katika uhifadhi, hivyo, ni muhimu washirikishwe ili kuwajengea uelewa na uzalendo.

“Kijana akielewa inakuwa rahisi kuendeleza uhifadhi wa mazingira na maliasili ya taifa,” anasema Ngereza.

Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Makumbusho ya Taifa, Lusekelo Kaisi anasema Makumbusho ya Taifa inaendelea kuimarisha mifumo yake ya mawasiliano ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii ili kuwawezesha wananchi na jamii kwa jumla kupata taarifa mbalimbali za kimakumbusho kwa urahisi zaidi.

“Kupitia njia hizi za mawasiliano jamii inaweza kupata taarifa, machapisho na maonesho kwa urahisi bila wao kufika makumbusho,” anasema Kaisi. Mwandishi ni Ofisa Habari wa Makumbusho ya Taifa

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Joyce Mkinga

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi