loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Asili ya chimbuko la binadamu

“ENEO la Bonde la Olduvai lilipata jina hili kutokana na mmea wa katani mwitu ambao Kimasai, huitwa oldupai. Mmea huu husaidia kuhifadhi maji ambayo huwa msaada kwa baadhi ya wanyama hasa kipindi cha kiangazi na hutumika pia na wenyeji kutengeneza kamba.”

Ofisa Urithi wa Utamaduni wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Godfrey Ollemoita anabainisha hilo anapozungumzia umuhimu wa kihistoria na kiutalii wa Bonde la Oldupai akisisitiza umuhimu wa Watanzania wa kada mbalimbali wakiwamo wafanyakazi na wanafunzi, kutembelea eneo hilo ili kujifunza chimbuko la binadamu duniani.

Anasema: “Watu waje Olduvai kwenye chimbuko la binadamu. Vivutio vingine wanaweza kuvipata na kuviona kwingine, lakini hakuna sehemu nyingine duniani ambapo aina nne za zamadamu zimegundulika sehemu moja. Dunia nzima inakuja hapa.”

Anasema fuvu la binadamu wa kale maarufu kama Zinjanthropuus lilivumbuliwa katika bonde hilo pamoja na visukuu vingi vya wanyama wa kale na masalia mengi ya zana za mawe.

“Hii ndiyo sababu wengi wanaokuja kikazi, wakishaona na kujua mambo haya vizuri, huondoka na kisha kurudi na familia zao kufaidi urithi huu wa Mtanzania.”

Ollemoita anasisitiza Watanzania kutembelea eneo hilo kujifunza na kuifahamu historia hiyo na mandhari halisi ya eneo hili ndani ya Tanzania, sambamba na kuchangia pato la taifa linalosaidia kuboresha huduma za kijamii. Hata hivyo anasema: “Ninaishukuru Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kujenga makumbusho mpya ya kisasa, yenye eneo kubwa na mazingira bora ambayo yamesaidia sana kuvutia wageni wengi.

BONDE LA OLDUVAI

Eneo hili la Bonde la Olduvai linapatikana eneo la Hifadhi ya Ngorongoro katika Mkoa wa Arusha likiwa miongoni mwa maeneo muhimu zaidi duniani kwa utalii, utafiti na elimu juu ya jiolojia, akiolojia na anthropolojia na huvutia watalii na watafiti wengi kutoka ndani na nje ya nchini. Hapa ni mahali ambapo wanyama wa kale, zamadamu na zana zao waliishi kwa zaidi ya miaka milioni 2 iliyopita.

Ofisa wa Urithi wa Utamaduni wa NCAA, Ollemoita, anasema: “Hapa ndipo Mwanaakiolojia Mary Leaky alipogundua fuvu la kichwa la zamadamu maarufu kama Zinj.”

Anaongeza: “Pamoja na mabaki ya mifupa ya tembo, kongoo wenye pembe kubwa na mbuni, Julai 17, 1959 mabaki ya fuvu la kichwa la Paranthropus boisei maarufu kama Zinjanthropus. Fuvu halisi limehifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam...”

Ollemoita anasema: “Kimsingi, fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania na hata mwaka jana tulisherehekea maadhimisho ya miaka 60 ya ugunduzi wa fuvu hilo hapa…”

“Ugunduzi huo uliofanyika saa nne asubuhi Julai 17, 1959 kipindi hicho kwenye eneo la Tanganyika, ulikuwa wa vipande zaidi ya 100 ukasaidia katika kutambua asili ya watu wa awali duniani.”

Ameandika Frankrover James mtaalam wa masuala ya urithi wa Utamaduni Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, karibu na bonde hilo la Olduvai Gorge, umbali wa takriban kilometa 45 Kusini, lipo eneo lingine maarufu la Laetoli ambapo mwaka 1976/78 Mary Leakey huyohuyo aligundua nyayo za zamadamu wa kale za miaka milioni 3.6 iliyopita ambao walikuwa wanatembea kwa miguu miwili.

Kimsingi, unapotembelea eneo la Bonde la Olduvai kuona masalia hayo na kupata historia yake huku ukiliona bonde hilo lilivyo sambamba na matabaka yake ya udongo wa volkano, unakuwa na fursa pia ya kuuona mchanga unaohama kila mwaka kwa sura na umbo lilelile na mwelekeo uleule.

MCHANGA UNAOHAMA

Akielezea kuhusu mchanga huo, Ollemoita anasema: “Mchanga huu ulitokana na kulipuka kwa volkano hai ya Mlima Oldonyo Lengai takribani kilomita 60 kutoka ulipo mchanga huu kwa sasa na una asili ya sumaku...”

Mchanga huu unaohama ni moja ya vivutio vya kipekee katika eneo la Hifadhi ya Jiolojia la Ngorongoro- Lengai. Vyanzo hivyo vya habari vinabainisha kuwa, mchakato wa kuhama kwa mchanga huu kwa utaratibu maalumu unaofanya umbo la nusu mwezi lisilobadilika, ni miongoni mwa vigezo vikubwa vilivyoifanya eneo la hifadhi ya Ngorongoro kutambuliwa na UNESCO kama eneo la hifadhi ya jiolojia.

Naye Ofisa Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni wa NCAA, Selestinus Emanuel ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Olduvai anasema: “Mchanga huu unapatikana takribani kilomita 5 kutoka Bonde la Olduvai ambapo huhama kutokana na nguvu ya upepo kutoka Mashariki kuelekea Magharibi ukiwa umeshikana bila kubadili sura ya umbo lake kutokana na asili yake ya sumaku.”

“Unasogea kwa wastani wa mita 17 kwa mwaka sawa na kuhama kwa sentimeta 4.66 kila siku huku ukiendelea kushikilia sura ya mwezi mchanga isiyobadilika.”

Anasema: “Mchanga huu una asili ya sumaku na huufanya kubaki na umbo la nusu mwezi muda wote unapohama na bado tunaendelea na tafiti zaidi kuhusu mchanga huu…”

JESHI la Polisi kupitia Kikosi cha Farasi, limeanzisha huduma ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi