loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba, Yanga safi

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba na mabingwa wa kihistoria Yanga, mambo yameeleweka kwa upande wao, baada ya kukamilisha zoezi la upimaji wa virusi vya corona kwa wachezaji na benchi la ufundi na kuanza mazoezi rasmi.

Timu zote mbili zilikamilisha upimaji juzi kuunga mkono juhudi za Wizara ya Afya kuepusha kuenea kwa virusi vya corona, kuelekea kurejea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosimama tangu Machi 17.

Kwa upande wa Simba, Meneja wake Patrick Rweyemamu, jana alisema wameshamaliza upimaji na wameshaanza maandalizi rasmi kwenye uwanja wao wa Simba Mo Arena ulipo Bunju kujiandaa na ligi.

“Wachezaji wote na benchi la ufundi wamefanyiwa vipimo na tumeanza mazoezi ya pamoja tukijiandaa na ligi na mpaka sasa waliokosekana ambao hawajafika ni watatu, Cleatus Chama, Shiraf Shiboub na Francis Kahata,” alisema.

Yanga kupitia kwa daktari wake, Sheikh Mngazija, alisema wameshakamilisha upimaji na hakuna mgonjwa yeyote mpaka sasa na kusisitiza umuhimu wa wachezaji kuwa makini kila wakati kwa kuzingatia taratibu zote, ikiwamo kunawa mara kwa mara na kupaka vitakasa mikono au sanitaiza.

“Tunaendelea kuchukua tahadhari zote kwa wachezaji kuwa makini na kufuata taratibu za afya na kingine kuhakikisha hawasogeleani karibu, kufanya mazoezi kwa umbali kidogo,” alisema Daktari huyo wa mabingwa hao wa kihistoria.

Kwa mujibu wa Mngazija, kwenye kikosi hicho hakuna majeruhi yeyote na wote waliokuwepo akiwemo kipa Ramadhan Kabwili aliyepata ajali ambaye anaendelea vizuri na ameanza mazoezi, majeruhi wa muda mrefu Juma Mahadhi aliyekosekana kwa karibu msimu mzima naye amerejea rasmi baada ya kupona.

Timu zote mbili ziko kwenye mbio ya kuwania taji la Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam (FA) kutokana na kuwa na nafasi nzuri. Katika Ligi Kuu, mpaka sasa kinara ni wekundu hao wa Msimbazi wenye pointi 71, wakifuatiwa na Azam iliyopo katika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 54, huku Yanga wakiwa katika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 51, wakicheza mara 27, huku Simba na Azam wakishuka dimbani mara 28.

Mbali na timu hizo zilizoanza kwa kupima wachezaji wake, nyingine ni Azam FC walioingia kambini juzi na Namungo wakithibitisha hayo, utaratibu ambao utazingatiwa na klabu zote kabla ya kuanza kwa ligi mwezi ujao.

Timu zingine ambazo zimeanza mazoezi kujiandaa na ligi hiyo itakayochezwa katika kituo kimoja cha Dar es Salaam kwenye viwanja vya Taifa, Uhuru na Chamazi ni Ndanda, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar na Coastal Union.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi