loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Msimu Ligi Kuu Bara uende vizuri

LIGI Kuu Tanzania Bara sasa itarejea kuanzia Juni 13, kwa mujibu wa Bodi ya Ligi huku ratiba kamili ikitarajiwa kutolewa Jumapili.

Michezo nchini ilisimama tangu Machi 17 baada ya Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza kusitishwa baada ya kusambaa kwa virusi vya corona, ambavyo vimekuwa vinaisumbua dunia kuanzia Desemba mwaka jana vilipobainika kwa mara ya kwanza nchini China.

Ligi Kuu Tanzania Bara kama michezo mingine, nayo ilisimama tangu wakati huo hadi pale michezo iliporejeshwa tena na Rais Dk John Magufuli kuanzia Juni Mosi mwaka huu.

Kwa kweli kurejea kwa michezo ni jambo la faraja kubwa, kwani linarudisha ule msisimko uliokuwepo hasa katika soka kupitia Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine.

Ni matarajio yetu kuwa kurejea kwa Ligi Kuu licha ya kubaki mechi chache, lakini itarejea kwa nguvu zote kuanzia wachezaji kuwa fiti, waamuzi kuchezesha vizuri kwa kufuata sheria 17 za soka, makocha na wahusika wengine kufuata taratibu za mchezo huo.

Tumezoea kuona ratiba ya Ligi Kuu ikibadilishwa mara kwa mara, hilo hatulitarajii katika kipindi hiki, ambacho mechi zitachezwa katika kituo kimoja cha Dar es Salaam katika viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex.

Hatutarajii kuona Bodi ya Ligi kubadili ratiba bila utaratibu maalum na kuzivuruga timu na mashabiki, ambao wengi watakuwa wakifuatilia kwenye televisheni.

Jumla ya mechi zilizobaki ni kama 148, ambapo kuna timu zimebakiza kuanzia mechi sita hadi tisa, huku Yanga ikiwa na kiporo kimoja baada ya kushuka dimbani mara 27 wakati Tanzania Prisons ikicheza mechi 30, ambazo ni nyingi zaidi ya wengine.

Kutokana na idadi hiyo ya mechi ni matarajio yetu kuwa Ligi Kuu itakuwa tamu sana yenye mvuto mkubwa, ambao utamfurahisha kila mtu kutokana na wachezaji kucheza vizuri na waamuzi, ambao mara nyingi wamekuwa kero, nao watachezesha vizuri.

Wakati huu ni kipindi cha timu kufanya mazoezi baada ya wachezaji wao kuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili, wengi wao walikuwa wakijifanyia mazoezi binafsi ndani kutokana na janga hilo la corona.

Baadhi ya wachezaji kweli walizingatia maelekezo ya makocha wao ya nini cha kufanya katika mazoezi wakati wote wa kukaa ndani, lakini wengine huenda walizembea na hao ndio watakuwa na wakati mgumu wakati huu wa mazoezi.

Kikubwa ni kumshukuru Rais Magufuli kwa kurejesha michezo na hasa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani itasaidia kuwachangamsha watu hasa katika kipindi hiki cha COVID-19.

Pamoja na kupungua sana kwa wagonjwa katika vituo na hospitali zetu, bado viongozi wetu wanasisitiza uwepo wa tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi