loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ni simba Vs Azam, Yanga Vs Kagera Sugar

RATIBA ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA) hatua ya robo fainali imetoka, huku Simba au Yanga zikionekana safari yao ya kwenda fainali kukwama mapema kwa mmojawapo kama tu zitakutana kwenye hatua ya nusu fainali.

Katika droo iliyochezeshwa jana Dar es Salaam na Azam Media chini ya usimamizi wa Meneja Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Baraka Kizuguto, Simba itakuwa mwenyeji wa Azam FC hatua ya robo fainali na Yanga ikiikaribisha Kagera Sugar kwenye mechi zitakazochezwa kati ya Juni 27 na 28 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kizuguto, mshindi wa mechi kati ya Simba na Azam atakutana katika hatua ya nusu fainali na mshindi kati ya Yanga na Kagera Sugar, katika michezo itakayochezwa kati ya Julai 11 na 12, hivyo basi wakongwe hao wakifanikiwa kuvuka na kukutana hatua hiyo, lazima mmoja aondolewe na mwingine kusonga mbele fainali.

Timu hizo zilishakutana kwenye ligi Simba iliifunga bingwa mtetezi wa FA Azam FC michezo miwili ya mzunguko wa kwanza bao 1-0 na wa pili mabao 3-2, huku Yanga nayo haitasahau kipigo kizito kutoka kwa Kagera Sugar cha mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Uhuru hivyo, haitakuwa michezo rahisi kwa kila mmoja.

Ukiachilia mbali kila mmoja kukutana, haitasahaulika msimu huu ulikuwa ni mzuri kwa Yanga pale ilipokutana dhidi ya mtani wake wa jadi Simba na kuifunga bao 1-0 katika Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Endapo watakutana, Simba watataka kulipa kisasi cha kufungwa 1-0 katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, ambao inarejea Juni 13 baada yakusimama kwa miezi miwili kutokana na corona.

Kingine, tangu michuano hiyo irejee misimu minne iliyopita, Simba haijawahi kukutana na Yanga na kama zitakutana baadaye ni historia nyingine itatengenezwa ila Yanga iliwahi kukutana na Azam FC katika fainali kwenye msimu wa kwanza iliporudi na kushinda mabao 3-1.

Aidha, michezo mingine ya robo fainali itakayochezwa ni Namungo dhidi ya Alliance, ambapo mshindi atakutana nusu fainali na mshindi wa mchezo kati ya Ndanda dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza ya Sahare All Stars ya Tanga, ikiwa timu pekee isiyo ya Ligi Kuu iliyobaki katika mashindano hayo.

Timu itakayofanikiwa kufika fainali na hatimaye kuchukua taji ndio itakayowakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika timu zote nane zilizopo ni tatu zimewahi kuchukua taji hilo kila mmoja mara moja ambazo ni Simba, Yanga na Azam na ukitoa nje ya hizo Mtibwa Sugar iliwahi pia.

Baadhi ya viongozi wa klabu hizo wamezungumzia namna walivyopokea ratiba hiyo wakiongozwa na Mtendaji wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ aliyesema kuwa wao na Simba wote ni wakubwa na ndio wanaoongoza ligi na anategemea mechi nzuri yenye ushindani wa aina yake.

“Sisi nguvu zetu zote tunategemea FA tutajiandaa kupambana kuhakikisha tunapata kikombe hiki na kuwakilisha nchi kimataifa,” alisema huku Simba iliyokilishwa na mmoja wa wazee wao maarufu kama Kisiwa akitamba kuwa wanahitaji kuchukua makombe yote ya ligi na shirikisho.

“Tumejipanga kushinda ila haitakuwa mechi rahisi bali yenye ushindani wa hali ya juu lakini tunaamini makombe yote yatakuwa yetu,” alisema Kisiwa.

Kwa upande wa Yanga Katibu Mkuu Dk David Ruhago alisema hawana wasiwasi wamepokea ratiba hiyo kwa mikono miwili, wanakwenda kujipanga kuhakikisha wanafanya vizuri na tayari kikosi chao kimeanza maandalizi ya mashindano yote.

Alisema wakati wakielekea kwenye mabadiliko ambapo kesho wataingia mkataba na La Liga kwa ajili ya kuwaelimisha mfumo wa uwekezaji anawaita wana Yanga kushuhudia hatua hiyo muhimu itakayowaingiza katika maendeleo ya soka kwenda kisasa.

MITAA ya mji wa Ruangwa imepambwa kwa bendera za rangi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi