loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

Mabadiliko uteuzi CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekuja na utaratibu mpya wa kupata wagombea wa Ubunge na Uwakilishi katika uchaguzi mkuu, baada ya kubaini uliotumika mwaka 2015 ulikuwa na upungufu.

Katibu Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kwamba tathimini iliyofanywa na chama, imebaini mchakato uliotumika katika uchaguzi mkuu huo, uliacha mianya ya rushwa na uvunjifu wa taratibu.

Mchakato mpya utakaotumika Oktoba mwaka huu, umefuta utaratibu wa awali ambao mgombea ubunge alitakiwa kupita kata kwa kata na kwenye matawi kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni.

“Chama baada ya tafakari kubwa, imekuja na utaratibu uliowekwa kwenye katiba na kanuni ya uchaguzi na utatumika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu,” alisema Polepole na kufafanua vitakavyohusika kujadili na kupendekeza wanaostahili kugombea.

Upande wa Zanzibar kwa maana ya Uwakilishi, itakaa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu kwenye ngazi ya jimbo. Kuhusu ubunge, vikao vitaanzia Kamati ya Siasa ya Wilaya kisha Kamati ya Siasa ya Mkoa na baadaye Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Mchakato utaendelea kwenye Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, itakayojadili kisha kuteua majina matatu ambayo yatakuwa ni siri kubwa.

“Yatafungwa na kuwekwa mhuri wa moto, kisha majina yale yatarejeshwa kwenye mkutano wa jimbo kwa maana ya wabunge na wawakilishi,” alisema.

Alifafanua kwamba mikutano ya jimbo ya CCM ina wanachama, viongozi na wajumbe kati ya 800 na 1,000 na ndipo bahasha hiyo itafunguliwa.

“Pale zitapigwa kura na wajumbe hao 1000... Mchakato utatengenezewa muhtasari...utafungwa kisha utaanza mchakato wa pili,” alisema na kuongeza kwamba taarifa hizo zitakwenda makao makuu ya CCM na kuanza mchakato wa kujadili hao watatu.

Polepole alisema Kamati ya Siasa ya Jimbo Zanzibar na Kamati ya Siasa ya Wilaya kwa maana ya wabunge, zitaketi na kujadili majina hayo na kupeleka mapendekezo kwa awamu ya pili.

Kamati ya Siasa ya Mkoa itajadili na kuweka mapendekezo kisha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa; Kamati Kuu ya Hamashauri Kuu ya Taifa. Baada ya vikao hivyo, cha mwisho ni Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kiko chini ya Mwenyekiti, Rais John Magufuli ambacho kitafanya uteuzi wa jina moja la mwana CCM atakayekuwa ameteuliwa kupeperusha bendera ya chama kwenye ubunge.

“Hilo ndilo jina ambalo tutalipeleka NEC kwa nderembo na mbwembwe,” alisema Polepole, ambaye alionya kuhusu uchukuaji na urejeshaji fomu kwa matarumbeta katika hatua za awali ndani ya chama.

Akieleza mabadiliko mengine katika mchakato wa uchaguzi, Polepole alisema yanahusu pia kadi na vitambulisho, ambavyo vyote vitakuwa katika mfumo wa kielektroniki, kuepuka mamluki kwenye vikao.

Alisema, “Kipindi hiki tumeweka utaratibu wa kielektroniki na vitambulisho janja ambavyo mjumbe atatoa kitambulisho na kutakuwa na king’amuzi hali itakayodhibiti mamluki. Tunataka haki itamalaki.”

Ratiba ya CCM Kwa mujibu wa Polepole, kabla ya chama kutangaza, hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya kitendo chochote kinachoashiria kuwa anataka kugombea.

Alisema pia baada ya kutangaza, hakuna anayeruhusiwa kwenda kwa mbwembwe za matarumbeta. Alisisitiza kwamba mchakato ndani ya chama, utaanza baada ya Bunge kuvunjwa rasmi kisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka utaratibu na ratiba.

Kwa mujibu wa Polepole, ratiba ya CCM itaendana na matakwa ya tume. Polepole alihimiza kwamba wakati huu ambao wabunge, wawakilishi na madiwani wanaendelea kutumikia wananchi, wapewe haki wamalize muda wao salama bila kuwabughudhi hadi hapo utaratibu wa chama wa kugombea utakapotangazwa.

Mkutano mkuu Akizungumzia maandalizi ya mkutano mkuu, alisema utaratiu unakwenda vizuri na juzi Mwenyekiti wa CCM, Magufuli alifanya ukaguzi wa ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete mjini Dodoma.

“Wajumbe watafika 2,000 na wageni wao, kuna kumbi ndogondogo za kisasa ambazo mpaka itakapofika Juni 15 kumbi hizi zitakuwa zimekamilika kwa ajili ya kuwapokea viongozi ,wajumbe wa mkutano mkuu, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi na wengine watakaoalikwa wakiwamo watendaji, Ofisi ya Msajili na vyama.”

Matapeli, walaghai Wakati huo huo, alisema chama kimebaini kuwapo matapeli na walaghai wakiwamo wanaojipitisha majimboni na wilayani, kwa kisingizio cha kuchangisha fedha kwa ajili ya fomu ya mgombea wa urais. “Sisi tunajua kwa utaratibu wa chama chetu, mpaka sasa mgombea wetu wa urais anajulikana. Ni desturi ya chama chetu. Tunaomba sana, watu matapeli na walaghai muwatolee taarifa polisi na Takukuru,” alisema.

Alitaja kundi lingine walilobaini ni watu wanaojiita watafiti wa chama, wakidai kutafiti kukubalika kwa wabunge wa CCM. Aliomba watu hao wapuuzwe na watakaowabaini watoe taarifa.

Polepole alisema wapo wengine wanaodai wametumwa na viongozi wakuu wa chama kwenda kugombea, jambo alilosema si kweli. Dawa yaandaliwa Polepole alisema chama kimeanzisha kituo cha taarifa za uchaguzi, ikiwa ni dawa ya kushughulikia watovu wa nidhamu.

Zipo namba mbili ambazo watu watawarekodi watu wanaotuhumiwa kutoa rushwa na kurusha taarifa zao kwenda kwenye chama. Watakaoripoti watatakiwa kuwasilisha pia ushahidi.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezipa ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

2 Comments

 • avatar
  Mohamedi Liwawa
  07/06/2020

  Namshukuru katbu mwenezi kwa maelezo mazuri hao wanaopita na kujifanya wanachangisha nio watakaotusababishia kugawanyika kwa wanachama wetu wa ccm naomba zoezi hilo liangaliwe kwa kina wagonbea wengine wenye pesa ndio wanajifanya wana haki ya kuwa viongozi kwa kutumia pesa zao hv kama wanaweza kuwasaidia wananchi kwann wasinge wapa kampan kwa kutumia pesa zao pasipo kugombea chochote sasa naomba viongozi wa wilaya, mkoa na taifa wawe makini katika wakati huu wa uchaguzi ahsante

 • avatar
  Mohamedi Liwawa
  07/06/2020

  Namshukuru katbu mwenezi kwa maelezo mazuri hao wanaopita na kujifanya wanachangisha nio watakaotusababishia kugawanyika kwa wanachama wetu wa ccm naomba zoezi hilo liangaliwe kwa kina wagonbea wengine wenye pesa ndio wanajifanya wana haki ya kuwa viongozi kwa kutumia pesa zao hv kama wanaweza kuwasaidia wananchi kwann wasinge wapa kampan kwa kutumia pesa zao pasipo kugombea chochote sasa naomba viongozi wa wilaya, mkoa na taifa wawe makini katika wakati huu wa uchaguzi ahsante

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi