loader
Msomi- Vijana tumieni fursa tehama mtajirike

Msomi- Vijana tumieni fursa tehama mtajirike

SEKTA ya Mawasiliano nchini imezidi kuchagiza maendeleo ya jamii na nchi nzima kwa ujumla huku kukiwa na changamoto kadhaa za matumizi bora ya mitandao hapa nchini.

Katika sekta hii hivi sasa kuna mabadiliko makubwa kwani tofauti na ilivyokuwa awali hivi sasa imehusisha zaidi teknolojia na kuigeuza kuwa Sekta ya Teknolojia na Mawasiliano ambapo mfumo wa intaneti imekuwa ni kunganishi kikubwa.

Licha ya umuhimu wake mkubwa katika kuifanya dunia kuwa kama kijiji katika nyanja za mawasiliano lakini pia zimeibuka changamoto katika kuitumia sekta hiyo kifaida.

Wapo wanaoitumia kupata fedha nyingi kwa njia mbalimbali ambazo ni sahihi lakini pia wapo ambao wanaitumia kupata fedha ila kwa njia ambazo si sahihi huku wengine wakikiuka maadili ya watanzania kupitia mitandao hiyo, hata hivyo zipo mamlaka za kiserikali ambazo zimekuwa mstari wa mbele kukabiliana na matumizi mabaya ya mitandao huku pia wakiwepo wadau mbalimbali waliojitokeza kuhakikisha vijana wanatumia mitandao kujiongezea kipato.

Mary Msuya ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Nchini(TCRA-CCC) ambaye licha ya kutetea haki za watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini pia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi hasa kundi la vijana linanufaika na huduma hiyo.

Mwanamama huyo mwenye Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kutoka Chuo Kikuu nchini Marekani anasema kuwa upo utajiri mkubwa kwenye sekta ya mawasiliano ambao vijana wa kitanzania wameanza kunufaika nao.

Anasema akiwa kama Katibu Mtendaji wa Baraza hilo aliyeanzia kazi mahali hapo tangu mwaka 2008 akiwa katika kitengo kinachojihusisha na elimu na hamasa kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano ameona ni kwa kiasi gani vijana wa kitanzania wamekuwa wakitumia fursa za mawasiliano kujiendeleza kimapato.

Mary anasema akiwa kama mdau ameona vijana ambao wamekuwa wakitengeneza maudhui kama vile kuanzisha huduma za masomo, mapishi hata maudhui mengine kadhaa na hutengeneza duka mtandaoni(App) na kisha kuuza kwa watu.

Kwa mujibu wa Mary hatua kama hizo ndio ambazo zinachagiza matumizi bora ya huduma ya mawasiliano nchini huku akibainisha kuwa ofisi yake inashirikiana na wadau kuchagiza mafanikio hayo.

“Sekta ya mawasiliano ina vitu vingi ndani yake, hasa kwa upande wa huduma za mawasiliano kwa njia ya mtandao kuna mambo mengi ambayo hakika vijana kama wakiyatumia kama fursa watakuwa na fedha nyingi hapa nazungumzia huduma kama za facebook, youtube, instagram na nyinginezo nyingi,” anasema.

Akerwa na wanaotumia vibaya mitandao

Kwa muda wa miaka kadhaa aliyofanya kazi kama Katibu Mtendaji wa TCRA CCC, Mary ameonekana kuchukua hatua stahiki pia katika kuwawezesha vijana kwa ujumla wakiwemo wasichana na wanawake kukabiliana na udhalilishwaji mitandaoni.

Anasema kundi la vijana hasa wa jinsia ya kike wamekuwa wakidhalilishwa huku wengine wakijidhalilisha wenyewe katika mitandao ya kijamii bila ya kujua hatari zinazoweza kujitokeza.

Akianza na wanaodhalilishwa na wenza wao anasema kuwa wanapaswa kuripoti katika vituo vya polisi jirani na kufungua kesi kwa kuwa ni kosa la kisheria kwa mtu kumfanyia mwingine udhalilishaji katika mitandao ya kijamii.

Mary anasema, lakini imekuwa ni kawaida kusikia mtu kadhalilishwa na kisha aliyehusika na udhalilishaji huo anaendela na maisha kama kawaida kana kwamba hakuna kilichotokea huku aliyedhalilishwa akizidi kuugulia machungu.

Anasema kuwa wapo ambao wanapigwa picha za utupu na kisha waliohusika wanazitumia kama vyanzo vya mapato kwa kuendelea kuomba fedha kwa waliowapiga picha hizo huku wengine wakiomba rushwa ya ngono.

“Nimekumbana na malalamiko kama hayo, kikubwa ambacho ofisi yangu imekuwa ikifanya ni kuwashauri nini cha kufanya ili kukwepa aibu hiyo,” anabainisha.

Kuhusiana na wale wanaojiuza kwenye mitandao kwa kuweka picha za utupu, Mary ambaye ni mama wa watoto wawili anasema anakerwa na kuna wakati hutamani hata kutupa simu anapokutana na picha za aina hiyo.

Anasema ni udhalilishaji wa hali ya juu kwa kuwa licha ya kuwa wanaofanya uchafu huo kujidhalilisha wenyewe lakini wanakuwa wakidhalilisha utu wa watu wengine pia ambapo anafafanua kuwa wapo wanaoweka picha za utupu wanawake kwa wanaume.

Anabainisha kuwa asilimia kubwa ya wanaotafuta wateja wa ngono kwenye mitandao hiyo ni wanawake na kuwa kwa kufanya hivyo wanalivutia kundi la watoto kujiingiza kwenye biashara hiyo.

Ushauri kwa wazazi

Mary anasema ni muda sasa kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanazikagua simu za watoto wao wote wa kike na kiume ili kujua wanachokuwa wakiwasiliana na kufuatilia kwenye simu hizo.

Anasema kwa kuwa kipindi hiki simu ni sehemu ya masomo kwa watoto hasa kipindi hiki cha makabiliano dhidi ya ugonjwa wa covid 19 ambapo watoto wengi wanasoma masomo yao kwenye simu, lakini kuna mambo mengine mabaya ambayo hawatakiwi hata kuyasogelea.

Mary anasema imekuwa ni kawaida kwa watoto wengine kujihusisha hata na mahusiano ya kimapenzi na watu waliowazidi umri kwa kuwa wanatongozwa kwa njia za simu na kuwekeana miadi.

“Wazazi hasa wamama ni lazima tuendane na wakati katika kujua nini kinaendelea kwenye ulimwengu wa mitandao, yani kwa sasa malezi yanayoendelea kwenye baadhi ya mitandao kwa watoto kama tusipokuwa makini ni wazi kuwa watalelewa kwa njia za mitandao na huko ndio kuna kudanganyana,” anasema.

Anaongeza kuwa, “kuwa wapomaisha yasiyokuwa yao kwa kulingishia vitu ambavyo hata hawana, mfano kuweka picha wakiwa mbele ya gari na kusema wamenunuliwa na wapenzi wao, hali ambayo inawafanya wasichana wenzao kuona kuwa kumbe wanaweza kuwa na magari kwa njia za ngono tu, yani ni kama wanaihalalisha vile ngono.”

Anawasihi wazazi wasiyaache malezi ya kuwafuatilia na kuwaweka watoto wao katika maadili mema kwa kuwa bado kuna nafasi yao kama wazazi au walezi kuwaongoza watoto badala ya kuwaachia walimu tu.

Maisha yake

Mary mzaliwa wa Moshi mkoani Kilimanjaro, ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne, anasema kwa kuwa wakati huo wazazi wake hasa mama yake kama ilivyokuwa kwa wanawake wengine wengi wa miaka hiyo, malezi kwa watoto ilikuwa ni zaidi ya kawaida.

Mwanamama huyo aliyehitimu elimu yake ya sekondari katika shule ya wasichanaya Kibosho kwa elimu ya kidato cha kwanza hadi cha nne kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Zanaki, anasema kuwa makuzi yalikuwa yakianzia tangu shuleni ambapo elimu ilikuwa siyo tu kusoma ila hata shughuli za kijamii na mienendo mizima ya maisha yalikuwa yakifundishwa.

Anasema akiwa sekondari ya Kibosho, wasichama walikuwa wakifundishwa hata staha za mwanamke anazotakiwa kuwa nazo kama vile kutozungumza kwa sauti, kuepuka ugomvi, kujilinda na kujistiri kama msichana.

Kwa mujibu wa Mary walikuwa wakipata miongozo hiyo ya maisha shuleni lakini pia wakirejea nyumbani wanakutana na wazazi ambao nao walikuwa wakiwakuza katika misingi hiyo huku akitolea mfano wa yeye na wadogo zake wengine wawili wa kiume walivyokuwa wakipewa majukumu sawa na kazi za nyumbani.

Mary anaamini kuwa kuelimika siyo kusoma peke yake ila inahusisha mambo mengi hasa mwanafunzi kujitambua kwani mara zote kujitambua huko kunatokana na miongozo ya kimafunzo ya maadili.

Anasema kutokana na malezi kumwelekeza zaidi katika masuala ya kujitambua alikuta akivutiwa zaidi kusoma masomo ya maendeleo ya jamii na alipohitimu kidato cha sita alijiunga na masomo ya maendeleo ya jamii katika Chuo cha Tengeru Arusha kusomea Stashahada ya Juu ya Maendeleo ya Jamii.

Baada ya hapo mwaka 1999 alijiunga na Kituo cha Luninga cha ITV akiwa mfanyakazi kwenye kitengo cha masoko kabla ya kujiunga na uliokuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) akifanya kazi kwenye kitengo cha Mahusiano mwaka mmoja baadaye, huo ukiwa ni mwaka 2000.

Anasema alifanya kazi hapo hadi mwaka 2006 kisha akaenda nchini Marekani kusoma, huku akiwa na shauku zaidi ya kuja kurejea nchini na kujikita katika kazi ambazo zitamuwezesha kuwa karibu zaidi na jamii na hasa kuibadilisha.

Anabainisha kuwa aliporejea tu akajiunga moja kwa moja na TCRA CCC ambapo alianza kama Ofisa, kisha alipanda na kuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo na kisha aliidhinishwa rasmi kuwa Katibu Mtendaji nafasi anayoitumikia hadi sasa.

Anasema yeye hushiriki kufundisha, kujadiliana na kuelekezana mbinu za kujinufaisha kupitia sekta ya mawasiliano pamoja na kujilinda dhidi ya udhalilishaji kwake ni kazi ambayo yupo tayari kuifanya hata akiamshwa asubuhi tu tena bila ya kujiandaa.

Akiwa TCRA CCC amefanya kazi ya uelimishaji akiwa karibu na wasanii kama Hamisa Mobeto, Elias Barnaba, Duvani, Jay Mondi na wengine wengi huku akionesha kiu kubwa ya kutaka kuendeleza zaidi mapambano.

Nje ya muda wake wa kazi, anasema hupendelea zaidi kusoma vitabu na kutazama filamu zenye mafunzo kadhaa ya kimaisha, lakini pia ni shabiki mkubwa wa muziki laini na mpenzi wa kusafiri.

Kazi za nyumbani hupendelea zaidi kupika, kufanya usafi wa nyumba tena mwenyewe hasa siku anazo kuwepo nyumbani.

Mary anasema matamanio yake ni kuona siku moja Tanzania inakuwa nchi ya mfano kwa kuwa na wananchi wengi wanaonufaika na sekta ya mawasiliano tena kwa kujiongezea kipato lakini sio kuwa na watumiaji wa mitandao kwa kazi za zisizofaa.

Ushauri

Anasema,“kwa kuwa suala la viwanda ni dhana inayosukumwa na utendaji, wananchi wazione fursa za huduma ya mawasiliano kama njia ya kujiingizia fedha hasa kwa kutengeneza maudhui kwa wale wanaotumia mitandao kama Instagram, Facebook, Youtube na mingineo, maudhui yatakayofundisha watanzania namna ya kujiingizia kipato zaidi.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1e45b8acc76891c3df0a4c816627d2d5.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi