loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tujitahidi kukata mnyororo wa wavutaji tumbaku

MEI 31 dunia iliadhimisha siku ya kupinga matumizi ya tumbaku. Tumbaku ina madhara makubwa katika mwili wa binadamu. Taarifa za kitaalamu zinasema moshi wa tumbaku una kemikali zaidi ya 4,000 ambazo kati yake, takribani 250 zinajulikana kuwa hatari na zaidi ya 50 husababisha saratani.

Muungano wa Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) kupitia kitabu cha Mtindo wa Maisha na Magonjwa Yasiyoambukiza unahimiza watu kuacha kuvuta tumbaku kupitia sigara, msokoto, kiko, kunusa na hata kutafuna. Unasema moshi wa sigara huwadhuru wengine wasiovuta wanapokuwa kwenye nyumba, mighahawa, ofisi au maeneo mengine yaliyofungwa.

Tancda inafafanua kwamba utumiaji wa tumbaku unahusishwa sana na kifua sugu, saratani ya mapafu, kioo, kizazi, mifupa na ya ngozi.

Pia unahusishwa na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, vidonda vya tumbo, meno kuoza, kupungua nguvu za kiume na magonjwa mengi. Katika semina kuhusu kupinga matumizi ya tumbaku iliyowahi kufanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi aliweka bayana kuwa sigara ni kitu ambacho ukitazama haraka, utasema kina faida kwa maana ya kuwa zao la biashara.

Lakini akasema likitazamwa kwa muda mrefu, hiyo faida ndiyo inakuja kutumika kwenye kutibu wanaoathirika na tumbaku.

Na matibabu yake si rahisi. Kwa mujibu wa Dk Janabi, kumtibu mtu mmoja ambaye mishipa yake imeharibika (sigara ikiwa miongoni mwa visababishi), gharama yake ni kati ya Sh milioni sita na milioni nane.

Vile vile alisema ukitazama sababu za watu kufa duniani, namba moja ni magonjwa ya moyo. Kila mwaka watu milioni 18 wanafariki kutokana na matatizo ya moyo ambayo moja ya tano yanasababishwa na sigara.

Dk Johnson Katanga kutoka Taasisi ya Saratani (ORC) Kitengo cha Kinga alisema kwa sasa duniani, saratani inayoogoza ni ya mapafu na kisababishi kikuu ni uvutaji wa sigara au tumbaku.

Anasema tumbaku inavyochomwa kila unapovuta, moshi wenye zaidi ya kemikali takribani 4000, kemikali zipatazo saba zinakwenda moja kwa moja kwa binadamu na kusababisha saratani. Kwenye sigara kuna kemikali inaitwa nikotini inayomfanya mtu kutamani kuendelea kuvuta.

Athari ya sigara kwenye magonjwa ya saratani imeonekana kwa kuchelewesha matibabu kwa wanaotumia kuliko asiyetumia.

Dk Francis Kuria kutoka Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto Tanzania (PAT) alisema duniani takwimu zinaonesha kwamba takribani asilimia 90 ya watumiaji wa sigara na mazao mengine wameanza kutumia wakiwa wadogo.

Mtaalamu huyo alizungumzia mazoea ya kutuma wavutaji wengi kuwatuma watoto wakawawashie na kusema ndivyo wanavyoweza kuwafanya nao waanze uvutaji. Lakini pia wavutaji wanaweza kuwavutisha watoto kutokana na kukaa karibu nao.

Wataalamu wanasema mtu kama anavutia sigara ndani ya gari au kwenye nyumba, watoto wakija wakakaa kwenye gari hata ndani ya nyumba, bado kunakuwa na mabaki (third hand) yanayoweza kuleta hatari.

Hivyo kuvuta sigara ndani ya nyumba au kwenye gari bado kunaweza kuwaathiri watoto watakaoingia. Lakini pia, mjamzito kama anavuta sigara au anavutishwa, madhara yanaweza kutokea kwa mtoto ambaye hajazaliwa.

Kutokana na athari hizi zinazoainishwa na wataalamu, upo umuhimu mkubwa wa wadau mbalimbali kuendelea kuhimiza jamii kuondokana na matumizi ya tumbaku, hususani uvutaji sigara ambao ndiyo unatumika zaidi.

Pamoja na kuhitajika mkakati wa watumiaji kupatiwa msaada wa kuacha kuvuta sigara, nguvu nyingine ielekezwe kuzuia wasiotumia tumbaku wasishawishike kujaribu.

Mkakati huu uelekezwe zaidi kuzuia watoto na vijana kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni sehemu ya kukata mnyororo wa matumizi ya bidhaa hii hatari ambayo taarifa zinasema wanaonufaika wamewekeza mamilioni ya shilingi kutangaza bidhaa hizo zaidi wakilengwa vijana.

WHO inasema kila mwaka tasnia ya tumbaku inawekeza zaidi ya dola bilioni tisa za kimarekani kutangaza idhaa zake zaidi ikiwalenga vijana.

Ni jambo la kufurahishwa kusikia kwamba WHO imezindua mwongozo au zana mpya kwa ajili ya wanafunzi wa umri wa kuanzia miaka 13 hadi 17 kuwatahadharisha na mbinu za tasnia ya tumbaku zinazotumika kuwavutia na bidhaa hiyo yenye kuleta uraibu.

Juhudi hizi zisambae zikiambatana na elimu kwa umma ujue madhara ya tumbaku na kuwalinda watoto, vijana dhidi ya bidhaa hiyo.

Stella.nyemenohi@tsn. go.tz

UZURI wa ngozi huanzia ndani. Hivyo unavyoitunza ngozi yako kwa ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi