loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bunge lapitisha muswada sheria ya kinga viongozi wakuu

BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi Sura ya 3, ambayo inapendekeza mashauri yote ya madai dhidi ya Viongozi Wakuu wa nchi, yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akisoma maelezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi, kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 3 ya Mwaka 2020 ulijumuisha sheria 13. Alisema lengo la marekebisho hayo ni kukidhi maudhui ya dhana ya kinga ya mashtaka dhidi ya viongozi hao.

Profesa Kilangi alibainisha kuwa muswada huo, unalenga kufanya marekebisho katika Kifungu cha 4 ili kuweka masharti yatakayotaka mtu yeyote, anayekusudia kufungua shauri lolote la kikatiba chini ya Ibara za 12-29 zinazohusu haki za msingi kuidhihirishia mahakama ni kwa kiasi gani mlalamikaji ameathiriwa na ukiukwaji wa haki anayolalamikia.

“Lengo la marekebisho hayo ni kuhakikisha kuwa utekelezaji wa masharti ya Ibara hizi unazingatia matakwa ya Ibara ya 30(3), marekebisho katika kifungu hiki yanapendekeza mashauri yote ya madai dhidi ya viongozi wakuu wa nchi yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema.

Profesa Kilangi alisema marekebisho ya Sheria ya Masuala ya Rais Sura ya 9, yanalenga kurekebisha katika Kifungu cha 6 ili mashauri dhidi ya Rais kwa mambo anayodaiwa kuyatenda yeye binafsi kama raia yaliyoruhusiwa kufunguliwa dhidi yake kwa mujibu wa Ibara ya 46 (2) ya Katiba, yafunguliwe baada ya kutoka madarakani.

“Kifungu cha 7 kinapendekezwa kurekebishwa ili mashauri yoyote dhidi ya Rais yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lengo ni kuwa na maudhui ya dhana ya kinga dhidi ya Rais ambayo ni kulinda hadhi ya Rais na nafasi yake,” alisema.

Kuhusu Sheria ya Maboresho ya Sheria kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mengineyo Sura ya 310, Profesa Kilangi alisema marekebisho yamelenga kuongeza Kifungu kipya cha 18A ili kuwezesha mashauri yanayofunguliwa au maombi yanayoletwa chini ya Sheria hii dhidi ya uamuzi wa Viongozi wa Kitaifa (Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Jaji Mkuu) kufunguliwa ama kuletwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lengo likiwa ni kuendana na maudhui ya dhana ya kinga ya mashtaka dhidi ya Viongozi Wakuu wa Mihimili.”

Aidha, Profesa Kilangi alisema katika mabadiliko ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Sura ya 237, unafanya marekebisho kwa kuongeza kifungu kipya cha 65A, kwa lengo la kuweka masharti ya kinga dhidi ya mashtaka kwa Jaji Mkuu, Majaji na maafisa wengine wa mahakama katika utekelezaji wa majukumu yao ya kimahakama.

Kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ustawi wa Wanyama, Sura ya 154, Profesa Kilangi alisema umeongeza Kifungu kipya cha 9A kinachoweka utaratibu utakaoiwezesha Wizara yenye dhamana ya ustawi wa wanyama, kuchukua hatua stahiki dhidi ya mamlaka yoyote ya Serikali ya Mtaa, ambayo imepewa mamlaka ya kukusanya mapato yatokanayo na sekta ya mifugo na imeshindwa kusimamia masuala yanayohusiana na ustawi wa wanyama.

Katika Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi Sura ya 223, Profesa Kilangi alisema marekebisho yameongeza Kifungu kipya cha 20A ili kuweka katazo kwa wamiliki halali wa silaha na risasi, kuhamisha silaha hizo kwa watu wasioruhusiwa kumiliki silaha hizo, lengo likiwa ni kuhakikisha wakati wote silaha na risasi zinakuwa chini ya mmiliki halali.

Kwa mujibu wa Profesa Kilangi, marekebisho pia yamelenga Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania Sura ya 425 katika kifungu cha 2, ili kuwezesha Sheria hiyo kutoa msamaha kwa baadhi ya wanasheria wenye vigezo vilivyoainishwa, kutopitia kwenye mafunzo ya Shule ya Sheria.

Alisema Sheria ya Uendeshaji Bunge Sura ya 115, imerekebisha vifungu vya 5 na 7 kwa ajili ya kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu mamlaka ya kuanzisha idara, divisheni na vitengo katika Utumishi wa Bunge yanapaswa kupata idhini ya Rais.

Kuhusu marekebisho ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Sura ya 283, Profesa Kilangi alisema yamelenga kuondoa utaratibu wa Mkurugenzi wa Wanyamapori na maofisa wengine wa wanyamapori, kutaifisha mifugo kupitia utaratibu wa kufililisha makosa na badala yake utaifishaji wa mifugo, ufanywe kwa amri ya Mahakama.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezipa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi