loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga kuikabili JKT Tanzania leo

BAADA ya kubeba pointi tatu kwa Mwadui FC, Yanga leo itakuwa na kibarua kingine dhidi ya JKT Tanzania, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 walioupata Jumamosi iliyopita dhidi ya Mwadui FC kwa bao lililowekwa wavuni na Mapinduzi Balama.

Kuelekea mchezo huo wa leo, kocha wa Yanga, Luc Eymael, jana alisema alifanya tathmini ya kikosi chake baada ya mchezo dhidi ya Mwadui na kufanya marekebisho mapungufu ambayo yalionekana kwenye mchezo huo.

Alisema eneo la ushambuliaji lilikuwa na mapungufu mengi, hivyo alimelifanyia kazi ili kuhakikisha linakuwa bora katika mchezo wa leo na kuongeza lengo lake ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

“Eneo la ushambuliaji linaonekana kuwa na mapungufu, nimelifanyia kazi, kusudi ni kuendelea kupata matokeo mazuri ili kutimiza adhma ya kumaliza ligi katika nafasi za juu,” alisema Eymael.

Alisema ili kuhakikisha anatimiza hilo, ameweka mikakati ya kushinda kila mchezo na kuendelea kufanyiakazi mapungufu yatakayojitokeza kwenye kila mchezo.

Eymael ambaye alirejea nchini Ijumaa iliyopita ikiatokea nchini kwao, leo atakuwa kwenye benchi la ufundi baada ya kujuimuika na kikosi hicho kwenye mazoezi yaliyofanyika kwa siku mbili kwenye Uwanja wa John Merlin High Dodoma.

Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 54, Azam wenye 57 inashika nafasi ya pili na Simba inaongoza ikiwa na pointi 72.

Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

foto
Mwandishi: Rahimu Fadhili

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi