loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Morrison aomba radhi Yanga

WINGA wa Yanga, Bernad Morrison, amemalizana na klabu yake baada ya kuomba radhi kwa yaliyotokea na anatarajiwa kuungana na wenzake kesho kutwa, kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Azam FC.

Mchezaji huyo alishindwa kuungana na wenzake tangu kurejea kwa ligi mwishoni mwa wiki iliyopita, huku kukiwa na taarifa za kuhusishwa kuwa anatakiwa Simba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na mtandao wa klabu hiyo, mchezaji huyo alifanya mazungumzo na Kaimu Katibu Mkuu, Mwanasheria, Simon Patrick na kumalizana naye.

Taarifa hizo zilisema Morrison pamoja na mambo mengine, aliomba radhi wanayanga kwa usumbufu uliojitokeza. “Tulimuita ofisini na kuzungumza naye, akatueleza yanayomsibu, mchezaji ameomba radhi kwa uongozi na wanayanga na kuahidi kuungana na kikosi kambini Alhamisi,” alisema Patrick.

Kwa mujibu wa Patrick, Morrison alipata maumivu kwenye kidole hali iliyomfanya kushindwa kuvaa viatu na hivyo kukosekana mazoezini kwa siku kadhaa na baadaye akaanza kushughulikia matatizo binafsi ya kifamilia.

Awali, kulikuwa na tetesi kuhusiana na mkataba wake, ikidaiwa ulimalizika na alikuwa hajamalizana na timu hiyo, lakini baadaye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM Hersi Said, ambao ni wadhamini wa timu hiyo, akathibitisha alimalizana na mchezaji huyo kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.

Morrison alikuwa gumzo hivi karibuni bungeni baada ya kutajwa katika utani kwenye Bunge la bajeti kama mchezaji aliyemchoma Simba mkuki mmoja wa sumu katika mechi ya watani wa jadi ambapo wekundu hao walifungwa bao 1-0 Machi 8, mwaka huu, mfungaji wa bao hilo akiwa yeye.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi