loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga chupuchupu

MABINGWA wa Kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, jana walijikuta wakipunguzwa kasi katika Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.

Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 55 na kushindwa kuifikia Azam FC iliyopo katika nafasi ya pili yenye pointi 57, huku vinara Simba wako katika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi zao 72. JKT Tanzania imefikisha pointi 43 katika nafasi yake ya saba.

Katika mchezo huo, ambao ulijaa undava, JKT walianza kupata bao dakika ya 36 lililofungwa na Michael Aidan kwa shuti la mbali, akiuganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto na kudumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu na Yanga kufanya mabadiliko ambayo yalizidisha mashambulizi.

Patrick Sibomana ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Mapinduzi Balama, aliisawazishia Yanga bao dakika ya 76, akiunganisha mpira uliotemwa na kipa wa JKT, Mohammed Abdulrahman.

Baada ya Yanga kusawazisha walicharuka wakitafuta bao la ushindi, lakini kukosekana kwa utulivu kuliwafanya kushindwa kupata bao.

Mlinzi Lamine Moro alioneshwa kadi nyekundu kwa kucheza mchezo usio wa kiungwana kwa Mwinyi Kazimoto, ambaye naye anaoneshwa kadi nyekundu dakika ya 88 baada ya kutaka kumrudishia Moro, lakini alizuiwa.

Katika hatua nyingine mashabiki uwanjani hapo hawakuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona, kwani walijaa na kushindwa kupata ule umbali wa mita moja unatakiwa kulingana na mwongozo wa serikali.

Wakati huohuo, baada ya mchezo huo, klabu ya Yanga imetangaza kumkata Sh milioni 1 Moro katika mshahara wake kwa kumpiga teke Kazimoto na kuiomba radhi JKT na wadau wote wa soka kwa kitendo hicho.

Kikosi cha JKT Tanzana kilikuwa; Mohammed Abdulrahman, Michael Aidan, Abdallah Waziri, Frank Nchimbi, Edson Katamba, Jabir Aziz, Mwinyi Kazimoto, Kelvin Nashon/Mohammed Rashid (dk 63), Shaaban Mgandila/ Hafidh Mussa (dk 70), Hassan Materema na Adam Adam.

Yanga ni Metacha Metacha, Juma Abdul, Adeyum Saleh, Said Makapu, Lamine Moro, Feisal Salum, Kelvin Yondani, Balama Mapinduzi/ Patrick Sibomana (dk 50),Haruna Niyonzima/David Molinga (dk 75), Ditram Nchimbi, Yikpe Gislain/Deus Kaseke (dk 66).

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi