loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Eymael alia ubovu wa viwanja

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael, amesema soka la Tanzania haliwezi kufanikiwa kama wachezaji wataendelea kucheza kwenye viwanja vibovu. Eymael ametoa kauli hiyo kutokana na ubovu wa baadhi ya viwanja vinavyotumika kwenye ligi hiyo.

Juzi Yanga ilibanwa na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ambao kocha huyo ameulalamikia kwa ubovu.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Eymael alisema ubovu wa sehemu ya kuchezea kwenye uwanja huo ilichangia kikosi chake kukosa ushindi ambao walikuwa wamedhamiria kuupata, ikiwa ni maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam FC unaotarajiwa kuchezwa Jumapili ijayo.

“Soka la Tanzania haliwezi kufanikiwa na wachezaji kucheza vizuri na kupata matokeo mazuri kama wataendelea kucheza kwenye viwanja ambavyo siyo rafiki, mpira hautulii muda wote unarukaruka na pasi zikitolewa zinashindwa kufika kwa mlengwa,” alisema Eymael.

Alisema hata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mwadui FC, walioshinda bao 1-0, uwanja walioutumia ulikuwa na shida hiyo hiyo na wachezaji wake walishindwa kujituma kwa kuhofia usalama wa afya zao kwa kuwa wanategemea mpira kama kazi ya kuendesha maisha yao.

Pia Eymael alitumia fursa hiyo kumwombea msamaha kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), mchezaji wake, Lamine Moro, aliyeoneshwa kadi nyekundu kwenye mechi hiyo kwa kumchezea vibaya, Mwinyi Kazimoto.

“Hali hiyo imemkuta akiwa kwenye kazi, hivyo TFF wamsamehe kwani mchezaji huyo kakosea kama binadamu mwingine, hivyo waangalie, nadhani atajirekebisha kwani hata mwenyewe anajutia tukio alilolifanya,” alisema Eymael, Kwa upande wake Moro ameeleza kujutia kitendo hicho na kuomba msamaha kwa Kazimoto, wapenzi na wadau wa mchezo huo na kuahidi kutorudia tena.

“Namuomba msahama Kazimoto kwa kitendo nilichofanyia pamoja na wapenzi na wadau wa soka, sitarudia tena, zaidi nitakuwa mfano mzuri na balozi wa kukemea mabaya uwanjani,” alisema Moro.

Baada ya mchezo huo, uongozi wa Yanga ulisema utamkata Moro Sh milioni moja kwenye mshahara kwa kitendo cha kumpiga teke Kazimoto na kuiomba radhi JKT Tanzania na wadau wote wa soka kwa kitendo hicho. Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 55 na Azam FC inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 na Simba inaongoza kwa pointi 72, zote zikiwa zimecheza michezo 29.

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi