loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ligi Kuu yarejea kwa sura tofauti

ULE uhondo wa Ligi Kuu Tanzania umerejea, na sasa mashabiki na wapenda soka wanashuhudia burudani safi waliyoikosa kwa takribani miezi mitatu kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Ligi hiyo ilirudi tena Juni 13, yaani mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kupigwa michezo miwili ya viporo, ukiwemo ule wa Yanga dhidi ya Mwadui ya Shinyanga uliofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage.

Kwa matokeo ya baadhi ya timu yaliyopatikana kwenye michezo iliyopita ya viporo imeonesha kwamba wachezaji wa vikosi vingi hawakubweteka kwenye kipindi hicho cha mapuziko ya corona, kwani walikuwa wanafanya mazoezi binafsi kwa kufuata programu za makocha ili kulinda viwango vyao.

Ukizitoa timu za Simba, Yanga na Azam FC, ambazo kimsingi zilikuwa zinategemewa kufanya makubwa kutokana na uwezo wa kigezo cha nguvu ya kiuchumi ikilinganishwa na klabu zingine ambazo zinalia na ukata, bado vigogo hao wanaonekana kupata wakati mgumu kupata ushindi.

Niwazi viongozi na wachezaji wameungana pamoja na kutanguliza maslahi ya kupigania timu, lakini pia kwa kila mchezaji kuonesha ubora ili kujiweka soko ili kusajiliwa tena na timu yake au kupata ulaji mahali pengine.

YANGA AFRICANS

Yanga walioanza kufungua pazia kwa ushindi kidunchu wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga. Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani ilishuhudiwa Yanga wakipata matokeo kwa shida dakika ya 30 kupitia kwa mchezaji Balama Mapinduzi.

Katika mchezo huo licha ya Yanga kupata ushindi, lakini walishindwa kuibuka na ushidi mnono baada ya washambuliaji wake kukosa umakini kila walipolifikia lango la wapinzani wao.

Siku tatu baadaye, Yanga walishuka tena uwanjani kwenye mchezo mwingine wa ugenini dhidi ya JKT Tanzania mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ambao ulikuwa na ushindani pamoja na ufundi mwingi ulishuhudiwa hadi unamalizika timu zote zikitoka sare ya kufungana bao 1-1.

Matokeo hayo yalionekana kuibua hali ya sintofahamu kwa Yanga, kwani mategemeo yao yalikuwa ni kuibuka na ushindi ili kuzidi kasi ya kuwania nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Azam FC wenye pointi 57 zote zikiwa zimecheza michezo 29.

SIMBA SPORTS

Simba ambao ni vinara wa ligi hiyo kwa pointi 72, walijikuta wakianza vibaya ligi hiyo baada ya likizo ya corona baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 Ruvu Shooting katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Simba walipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi, lakini walijikuta wakiambulia pointi moja baada ya dakika 90 kumalizika na kudhihirisha kuwa wapinzani wao nao walijiandaa.

Katika mchezo ni wazi wachezaji wa Simba walionekana kutoyatumia vizuri mapzumziko ya Covid-19, kwani hawakuwa fiti tofauti na wapinzani wao, ambao walikuwa vizuri zaidi. Hata hivyo, kocha wa kikosi hicho Sven Vandenbroeck amekiri wachezaji wake hawajarejea vizuri hivyo ana kazi ya ziada kuhakikisha anawapa mazoezi maalumu yatakayosaidia kurejesha ubora waliokuwa nao kabla ya ligi hiyo kusimama.

Sven kuonesha mkazo kwenye suala hilo alianza kuwapa wachezaji wake mazoezi makali na mechi za kirafiki kujiandaa na michezo ya ligi hiyo, ikiwemo unaotarajiwa kupigwa leo dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Sven anasema kuelekea kwenye mchezo huo, wamejipanga kikamilifu kwanza kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wao wa mzunguko wa kwanza kwa bao 1-0, lakini pia ushindi watakaoupata utasaidia kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia, tayari kwa michezo inayokuja na ile ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA).

AZAM FC

Klabu ya Azam licha ya kuanza vyema kwenye mchezo wao dhidi ya Mbao FC kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 uliofanyika Uwanja wa Azam Complex ,walikutana na ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao pamoja na kwamba kikosi cha Mbao hakina wachezaji wenye majina makubwa.

Matokeo hayo yaliwashangaza wapenda soka wengi, kwani Mbao wanasumbuliwa na ukata wa fedha hata safari ya kuja Dar es Salaam ilitawaliwa na changamoto lukuki. Kwa upande wake kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba anasema ushindi walioupata dhidi ya Mbao ni maandalizi makubwa kwa kuwakabili Yanga kwenye mchezo wa ligi hiyo unaotarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Cioaba anasema anajua Yanga wana kikosi bora kilichosheheni wachezaji nyota, kwa kutambua hilo wamejipanga kuonesha kitu cha tofauti kwenye mchezo huo kupata ili kupata ushindi utakaowafanya kuendelea kujikita katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo.

COASTAL vs NAMUNGO

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, kwani timu hizo zinapishana nafasi moja, ambapo Namungo wanashika nafasi ya nne kwa pointi 51 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati Coastal wanafuatia nafasi ya tano kwa pointi 47.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkali hadi unamalizika timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2 mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Katika kupindi cha kwanza, Namungo walitawala mchezo na kufanikiwa kupachika mabao 2-0 na ilionekana kama wangeweza kulipa kisasi cha kufungwa kwao Lindi mabao 3-1, lakini Coastal walipambana na kurejesha mabao hayo na matokeo kuwa 2-2.

Kiujumla, wengi walitarajia kuwa vigogo vya Simba na Yanga vingeshinda mechi zao zote za kwanza nakuendeleza ibabe, lakini mambo hayakuwa hivyo kwani yamekuwa tofauti baada ya kubanwa na `watoto’.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa adhabu ya kumfungia miaka ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi