loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shiboub azuiwa tena Sudan

KUNA uwezekano kiungo wa Simba, Sharaf Shiboub kutorejea nchini hivi karibuni kuungana na kikosi cha timu hiyo, baada ya Serikali yao kuongeza tena siku 10 za kuifungia Sudan, kutokana na mlipuko wa virusi vya corona kuendelea kushika kasi.

Mwanzoni mwa mwezi Juni, mlipuko wa virusi vya corona nchini humo ulishika kasi, hali iliyofanya kuongeza wiki mbili za kufunga shughuli za kijamii na safari za anga, hata hivyo tarehe ya kuifunga nchi hiyo ilimalizika juzi na jana asubuhi, Kamati Kuu ya Dharura ya Afya kuongeza muda mwingine.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara mchezaji huyo anashindwa kurejea kutokana na nchi hiyo kuwa kwenye kifungo cha tahadhari dhidi ya mlipuko wa virusi vya corona, ambapo kufikia jana watu 8,020 waliambukizwa na 487 kufariki

Akitoa ufafanuzi jana Manara alisema, Simba inamhitaji kiungo huyo kwa lengo la kuendelea kuisaidia timu yake, hivyo wadau wanapaswa kuwa watulivu wakisubiri siku rasmi ya Msudani huyo kurejea.

“Tungetamani sana mchezaji huyu aungane na sisi na unajua kuunganisha moja kwa moja kutoka Sudan kuja Dar es Salaam ni ngumu sana, nafasi zote tumeziangalia namna ya kumleta kwahiyo tutalizungumza siku tatu zijazo,”alisema Manara.

Shiboub ni mchezaji pekee wa Simba ambaye hadi sasa hajaungana na timu hiyo, huku baada ya wengine kutoka nje ya Tanzania, akiwemo Clatous Chama na Meddie Kagere kurejea na kuungana na wenzao.

Ukosekanaji wake, unawafanya Simba waendelee kuwatumia Mzamiru Yassin na Hassan Dilunga, kwenye eneo la kiungo, wakati wakimsubiri Jonas Mkude ambaye ameanza mazoezi mepesi, kutoka kwenye majeraha aliyopata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi