loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TMA yastahili pongezi ufanisi utabiri hali ya hewa

UTABIRI wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), umekuwa chanzo kikubwa cha taarifa kwa wananchi, katika kupanga mipango yao ya biashara, kilimo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji madini, maeneo ya kujenga yanayofaa, usafiri wa angani, nchi kavu na majini na masuala mengineyo.

Katika miaka michache iliyopita, tumeshushudia TMA ikitoa taarifa ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kuokoa maisha ya watu na mali zao. Kwa mfano, mwaka jana mwishoniTMA ilitabiri uwepo wa mvua kubwa zenye kuambatana na upepo mkali na matokeo ya utabiri yamekuwa sahihi kwa zaidi ya asilimia 90 na kile kilichotabiriwa.

Hata jana TMA ilitoa taaarifa kwa vyombo vya habari, ikieleza kuwa leo kutakuwa na kupatwa na jua maeneo ya Afrika ya Kati na Afrika Mashariki, ikiwemo Dar es Salaam , Bukoba, Arusha na Dodoma nchini Tanzania kuanzia saa 2.50 asubuhi.

Kwamba katika tukio hilo la leo, sehemu ya jua itakayofunikwa na mwezi wakati wa kilele cha kupatwa kwa jua, itatofautiana baina ya eneo na eneo.

Maeneo yaliyo ndani ya njia ya kupatwa kwa jua, yataona kupatwa kwa jua kwa kiwango kikubwa zaidi, ikilinganishwa na maeneo yaliyo mbali zaidi na njia hiyo.

Kwa hiyo, kwa dhati tunaipongeza TMA kwa kazi kubwa na nzuri, inayofanya kwa miaka mingi katika kufuatilia na kuhabarisha umma juu ya mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri, ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi na wananchi.

Tunaiomba TMA iendelee kutumia vifaa vyake, kutoa tahadhari za hali ya hewa zinazohitajika mno nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote.

Pia, tunaomba watendaji na wafanyakazi wa TMA, kuongeza juhudi na maarifa katika utendaji wao wa kazi ili kuwafanya wananchi, waendelee kujivunia uwepo wa taasisi hiyo muhimu katika ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa.

Aidha, tunaunga mkono kauli iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe hivi karibuni kuwa TMA inatakiwa iendelee kufuatilia mifumo hiyo ya hali ya hewa na kutoa utabiri wa hali ya hewa, kwani utabiri unachangia kulinda vyanzo vya maji na hivyo kuboresha upatikanaji wa maji, ambao ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya taifa na Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Ni imani yetu kuwa mafanikio hayo makubwa ya TMA, katika kutabiri matukio ya hali ya hewa kwa uhakika mkubwa, yametokana na namna serikali inavyoendelea kuijengea uwezo, kwa kuipatia wataalamu na vifaa zaidi; hivyo kuifanya kuwa moja ya taasisi zinazoaminika nchini, tofauti na hali ilivyokuwa miaka iliyopita.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi