loader
Katimiza ndoto zake baada ya miaka 7

Katimiza ndoto zake baada ya miaka 7

KATI ya mambo ambayo baadhi ya vijana wanakosa ni kuwa na dira thabiti ya kitu kikubwa ambacho wanataka kukifanikisha, kwa muda gani na lini hasa.

Kuwa na dira thabiti ndio kunazalisha mipango au mikakati ya kufanya ili kufikia hiyo dira ambayo kijana amepanga kuifikia kwa muda muafaka. Lakini hata kwa wenye dira wapo ambao hawana uthubutu wa kweli utakaowawezesha kuyafikia malengo husika kwa wakati muafaka.

Kila siku vijana wamekuwa wakiambiwa kuwa wao ni taifa la kesho, msemo ambao unapingwa na wengine kwa kusisitiza kuwa vijana si taifa la kesho tu bali ni taifa la leo na kesho.

Ni vema vijana nchini wakatambua kuwa uwepo wao leo ni lazima uwe na thamani kubwa ya kesho yao, iwe kwenye siasa, michezo, sanaa na shughuli yoyote ile ya kimaendeleo, hivyo kikubwa wanachopaswa kukifanya leo ni kuwa na mkakati wa kuwawezesha kuyafikia malengo yao huku wakitumia zaidi muda mwingi kufanya mambo yenye tija kwa kesho yao.

Mwanaharakati Getrude

Mhitimu wa Shahada ya Rasilimali Watu kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere- Kigamboni, Getrude Mligo (23) ni kati ya vijana ambao wameonesha mwenendo mzuri ambao unaweza kutumika kama mfano kwa vijana wenzake.

Akiwa na miaka 16 aliweka nadhiri ya kuandika kitabu chenye kuelezea masuala kadhaa yahusuyo haki za msichana yaani kitabu kinacholenga kuwahamasisha wasichana kupigania haki zao bila kukata tamaa.

Miaka saba sasa, Juni 10 mwanadada huyo alitimiza ndoto yake kwa kuzindua kitabu kiitwacho Dear Girl Child- I am Generation Equality Be Brave, uzinduzi uliohudhuriwa na wadau wa masuala ya haki za wanawake na watoto.

Getrude anabainisha kuwa kitabu hicho kimehusisha maandishi na picha za wanawake mbalimbali wenye mafanikio wakielezea changamoto walizokumbana nazo hadi kufikia hatua ya kufanikiwa.

Anasema ameamua kuelezea changamoto za wasichana huku akiyaandika mafanikio ya wanawake ili kuwahamasisha wasichana waliopo masomoni kutokata tamaa licha ya changamoto zinazowakabili.

Anaongeza kuwa wasichana wanakabiliwa na changamoto nyingi kama vile kuolewa wakiwa bado wadogo, mimba za utotoni, kubakwa pamoja na matukio mengine yanayowakatisha tamaa.

Getrude anasema kitabu hicho kinawapa mwanga wasichana kujua ni kwa namna gani wanaweza kupigania haki zao na wanawezaje kuwashirikisha wazazi, walezi au walimu katika kupigania haki hizo.

Anasema kitabu hicho kinapatikana katika maduka makubwa ya kuuzia vitabu huku pia msomaji anaweza kukinunua kwa njia ya mtandao kupitia duka mtandaoni la Soma Hub na Amazon kwa Sh 10,000.

Kwa mujibu wa Getrude ametumia miezi mitano kukiandaa kitabu hicho akishirikiana na wasichana, marafiki zake ambao ni MaryNsia Mangu, Sylvia Mkomwa, Thekla Schulte, Lilian Lema na UmmylKheri Said.

Anasema aliwashirikisha marafiki zake ambao nao walikuwa na mambo mengi ya kuzungumza na wasichana wenzao kwa njia ya kitabu hicho.

“Tangu nikiwa nasoma sekondari St Getrude mkoani Njombe nilikuwa na wazo la kuja kuandika habari kuhusiana na masuala ya wasichana pindi nitakapomaliza chuo na kilichonigusa zaidi hadi kuwaza kuja kuandika kitabu ni namna ambavyo niliona wasichana wakikosa nafasi ya kusikika au kuambiwa mambo mengi kuhusu usichana wao.

“Nilimaliza masomo yangu ya sekondari katika shule hiyo niliposoma kidato cha kwanza hadi nne na kisha masomo ya kidato cha tano na sita sekondari ya Maposeni mkoani Songea mkoani Ruvuma ambako pia wazo hilo tena likanijia,” anasema mwanadada huyo.

Anasema kuwa kila alipokuwa akikutana na wasichana wanaokabiliwa na changamoto kadhaa iwe katika familia zao au hata hapo shuleni au hata mitaani akisikia habari za wasichana wenzake, alikuwa akiingiwa na wazo na kutaka kuandika kitabu kitakachotoa suluhisho kwa wasichana wengi zaidi.

Getrude anasema muda huo alikuwa akishirikiana na wasichana wenzake hao kutoa elimu tu ya kuwaelimisha zipi ni njia bora kwa wasichana kukwepa changamoto shuleni na mitaani.

Lakini wakati alipojiunga na masomo ya Rasilimali Watu katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni ndipo sasa akawa anasoma na wasichana wakubwa kiumri.

Anasema kati ya changamoto alizokuwa akizisikia za wasichana sio tu chuoni hapo bali hata mtaani ni kuhusiana na mifumo dume kwenye mahusiano na masuala mengine kama unyanyasaji wa kijinsia.

Anabainisha kuwa akishirikiana na wasichana wenzake ambao baadaye ndio walikuja kuandika kitabu, walikuwa na jukumu la kutoa ushauri huku yeye akipenda zaidi kwenda kwenye vyama na makundi ya wanaharakati wa jinsia.

Anaongeza alijikuta akiwa karibuzaidi na mashirika yanashughulika na masuala ya jinsia kama vile Msichana Initiative, Her Initiative, Bright Jamii na Hope for young girls.

Akiwa katika kazi za kujitolea na mashirika hayo alijikuta akiongeza zaidi uelewa wa masuala ya haki za watoto, wasichana na wanawake kwa ujumla.

Siku moja akaalikwa kwenye uzinduzi wa kitabu cha Wajibu wa Mtanzania na Uongozi wa Rais John Magufuli kilichoandikwa na mwanadada Deborah Kiyuga hapo sasa ndio shauku ya kuandika kitabu cha haki za wasichana ikamjia zaidi huku ikichukuliwa kuwa alikuwa ameshapata uelewa kwa undani zaidi kuhusiana na haki za wasichana.

Getrude aliamua kuchukua hatua na kuandika kitabu hicho ambacho kipo kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza huku akifafanua kuwa lengo ni kuwafikia wasichana wa rika zote ndani na nje ya nchi.

Mawaidha ya wadau

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Bright Jamii Initiative, Irene Fugara alisema kuwa uamuzi wa Getrude kuandika kitabu cha kutetea haki za wasichana ni uamuzi muafaka kwa kuwa kitabu hicho kitawafikia wasichana, wazazi na walezi waliopo sehemu mbalimbali.

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeka Gyumi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kitabu hicho, anasema kuwa uamuzi wa Getrude kuandika kitabu unatoa taswira mpya ya ushiriki wa wasichana wadogo katika kupigania haki za wenzao.

Anasema kitabu hicho kinaweza kuchukuliwa kama njia mojawapo muhimu na ya msingi katika kuwasaidia wasichana kujitegemea, kujitambua, kupigania haki zao hata kuibadilisha jamii nzima kushiriki katika kuwasaidia wasichana nchini dhidi ya udhalimu wa mifumo gandamiziAnavutiwa na wanasiasa akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kutokana na mchango wake kwa vijana huku pia akivutiwa na mwanaharakati wa kiume Togolani Mavura.

Historia ya Getrude Mwanadada huyu amezaliwa mwaka 1997 mkoani Iringa na alianza elimu ya msingi mkoani Njombe katika shule iitwayo Mdete, Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne alisoma katika sekondari ya St Getrude iliyopo Njombe.

Masomo ya kidato cha tano na sita alisoma sekondari ya Maposeni iliyopo Songea mkoani Ruvuma kabla ya kujiunga na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere- Kigamboni.

Akiwa chuoni hapo alisomea fani ya Rasilimali Watu ambapo kitu kilichomvutia kusomea fani hiyo ni shauku yake ya kutaka kuona mazingira salama ya wafanyakazi kazini hususan wanawake.

“Ninakumbuka namna ambavyo baba yangu alikuwa akimsikiliza mama na hata kufikia hatua ya kumruhusu kwenda kusoma nje ya nchi wakati nikiwa mdogo kiumri, sasa nikianza kazi hii ya kuwa Ofisa Rasilimali Watu hakika nitahakikisha wanawake wanasoma popote wanapotaka,” anasema.

Getrude anasema atakabiliana na unyanyasaji wa kijinsia wa kila namna huku akibainisha kuwa ndio maana ameanza harakati hizo sasa.

Mwito wake kwa vijana

Anawataka vijana kusoma vitabu kwa kuwa kuna maarifa mengi katika kusoma huku akiwasihi waandishi wa vitabu hivyo kuwa na mbinu mbadala za kuwavutia vijana kusoma. Getrude anasema kitabu chake hicho kinapatikana katika mikoa sita ambayo ni Tanga, Dar es Salaam, Njombe, Songea,Morogoro na Iringa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/36473cd1f74555d44c89045a92aeca48.jpeg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi