loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jiepusheni na rushwa, uvunjifu amani

AGIZO la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa makamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia hatua wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu, tunaamini litachukuliwa kwa uzito mkubwa.

Agizo hilo ni muhimu katika kipindi hiki kama alivyonukuliwa Waziri Mkuu, kwa kuwa wapo wengi ambao wanachukulia kipindi hiki kama cha kuchumia tumbo.

Waziri Mkuu anajua vyema kwamba yapo wamezoea vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi, hivyo akasema serikali imeagiza taasisi hiyo nyeti kwa kushirikiana kwa kamati za ulinzi na usalama kuhakikisha hakuna vitendo vya rushwa katika uchaguzi na yeyote ambaye anajihusisha na rushwa asiachwe.

Katika kipindi hiki, tuseme kwamba tunaamini, agizo hilo ni muhimu na vyombo vya usalama kwa kushirikina na Takukuru kwani ulaji wa rushwa ni chanzo cha uvunjifu wa amani iliyopo.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Lindi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Nachingwea akiwa njiani kuelekea wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi.

Waziri Mkuu akasema kitendo cha kutoa na kupokea rushwa ni kosa, hivyo viongozi hao wa Takukuru nchini hawana budi kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Akawataka Makamanda wa Takukuru katika wilaya zote nchini kuhakikisha wanawakamata watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa, wakiwemo na wapambe ambao ndio wachochezi wakuu wa vitendo hivyo.

Tunaamini, agizo hilo likitelezwa vyema, uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu utakuwa huru na wa haki.

Waziri Mkuu pia akawasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kulinda amani na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa uchaguzi Mkuu.

Watanzania waelewe kwamba amani ambayo imekuwa ni moja ya utambulisho kwa nchi, ni kitu adimu kinachobidi kulindwa kwa gharama zozote.

Tukumbuke Rais John Magufuli wakati akivunja Bunge hivi karibuni jijini Dodioma, alisisitiza kwamba pamoja na maandalizi ya uchaguzi Oktaba kwenda vizuri, lakini wale wenye nia ya kuvunja amani, serikali haijalala.

Tunawasihi wenye kuchumia tumbo na wenye nia ya kuleta vurugu, iwe ni wapambe, wagombea wa nafasi mbalimbali kupitia vyama vilivyosajiliwa au viongozi wa vyama na wale wanaoptia mlango wa nyuma wa kutetea haki za binadamu, waache mapema nia mbaya zao hizo kwani badala ya kuleta vurugu, wataishia mikononi mwa vyombo vya usalama na nchi itaendelea kuwa kisima cha amani.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi