loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchumi wa soko jamii unaweza kuwa agenda

OKTOBA 25, 2020 Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa Sita katika mfumo wa siasa wa vyama vingi kuchagua rais, wabunge na madiwani. Mchakato wa uchagauzi huu unaendelea katika ngazi na maeneo mbalimbali.

Kinachoonekana ni kwamba uchaguzi wa mwaka huu utashirikisha watu wengi wenye uelewa kuhusu faida za uchaguzi makini, tofauti na miaka ya nyuma ambapo baadhi ya watu hasa wapigakura, walisukumwa na mihemuko ya kisiasa.

Uchaguzi wa mwaka huu, PAZIA ZA UCHAGUZI MKUU MWAKA 2020 watu hawataki kusikia suala la udini, ukabila, umajimbo wala ‘ugonjwa’ wowote tofauti na kuchagua kiongozi anayelipeleka taifa katika tija na maendeleo tarajiwa ya watu na vitu kama inavyoonekana katika miaka mitano inayoishia sasa.

Ndiyo maana, watu wanataka mgombea katika nafasi yoyote sasa apimwe kwa uwezo wa kukuza uchumi na kuboresha zaidi maisha ya watu. Ndiyo maana katika mafunzo ya siku moja kwa wanahabari kuhusu Mfumo wa Uchumi wa soko Jamii kwa Tanzania Kuelekea Maendeleo Shirikishi na Endelevu yaliyofanyika Kurasini Dar es Salaam, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza, Ponsian Ntui, anasema upo umuhimu mkubwa ilani za vyama vya siasa kuonesha zina mpango gani kuhusu uchumi shirikishi usioacha watu wengi nyuma.

Anasema: “Ilani za vyama zioneshe kuakisi maisha halisi ya watu na changamoto za kiuchumi kwa nchi yetu ili wagombea waeleze mwelekeo wa kiuchumi, falsafa na sera za uchumi wetu yaani, wanasiasa waulizwe wana mwelekeo na itikadi gani za kiuchumi.”

Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, uchumi wa soko jamii ni uchumi unaolenga maendeleo ya watu kama msingi wa maamuzi katika shughuli za kiuchumi ukitazama utu wa binadamu.

“Hivyo hata katika ilani za vyama, wanasiasa wanapaswa kuonesha namna uchumi utakavyoaksi katika maisha halisi ya watu na changamoto za kiuchumi katika nchi,” anasema Ntui.

Mhadhiri mwingine wa SAUT, Doto Bulendu, anasema ni vema kila mmoja katika sekta ya uchumi, kuwa na mchango na kunufaika kupitia uzalishaji, ulipaji kodi na uongezaji wa thamani kwa bidhaa na mazao.

Kitabu kiitwacho, “Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii kwa Tanzania: Kuelekea Maendeleo ya Uchumi Jumuishi na Endelevu” kilichochapishwa Machi, 2019 kwa ufadhili wa Konrad Adenauer Stiftung kinasema: “Mfumo wa Uchumi Jamii unajumuisha ukuaji wa uchumi endelevu na ushirikishwaji ili kuleta maendeleo kwa watu wote. Mfumo huu unapendekeza aina ya uchumi wa soko, lakini unahakikisha kuwa binadamu ndiye kiini cha shughuli zote za kiuchumi.”

“Kupitia mfumo wa ulinzi na udhibiti katika jamii, binadamu pamoja na ujuzi wao, mahitaji na motisha wanalindwa kikamilifu. Mfumo huu pia unaheshimu binadamu kama watu huru. Unaleta usawa kati ya soko huru na mfumo wa udhibiti wa serikali ulio rafiki kwa biashara. Unaruhusu ushindani wa haki na upangaji wa bei za bidhaa na huduma kwa uhuru. Hii huzalisha ajira, hujenga sekta binafsi zilizo imara na husaidia uchumi kukua.” Akirejea chapisho hilo, Ntui, anasema: “Uchumi wa Soko Jamii ni tofauti na mifumo ya kijamaa inayodhibiti jamii.”

Kwamba: “Mfumo huu pia ni tofauti na ubepari unaoheshimu uhuru wa mtu, lakini usiolinda jamii zilizo pembezoni. Mfumo wa Uchumi Jamii unajumuisha na kuwalinda wazawa katika maendeleo ya kiuchumi katika nchi yao.”

Kwa mujibu wa mtoa mada huyo, uzuri wa mfumo wa uchumi wa soko jamii, ni kuchuja na kuchukua mazuri katika uchumi wa kijamaa na kibepari; na kuancha mabaya hasa suala la baadhi ya wananchi katika uchumi wa jamii kubweteka wakijua ‘watabebwa’ na serikali hata kwa yale wanayopaswa kufanya wao, huku katika uchumi wa kibepari wanyonge ‘wakiachwa nyuma’ na shida zao.

Ndiyo maana Ntui anasisitiza: “Uchumi wa Soko Jamii ni uchumi unaolenga maendeleo ya watu kama msingi wa maamuzi katika shughuli za kiuchumi ukitazama zaidi utu wa binadamu…”

Chapisho la Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT) la Julai 2010 liitwalo: “Ilani (2009): Ufuatiliaji: Tudhamirie Siasa Adilifu” linasema, lazima watu wapewe kipaumbele kabla ya vitu na kusisitiza: “Ukuaji wa uchumi na manufaa kwa wote lazima viende sambamba.”

Uchunguzi wa mwandishi wa makala haya umebaini kuwa, kwa kulifahamu na kulizingatia suala hili, ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais John Magufuli, imetia mkazo katika ujenzi na uboreshaji wa zahanati, vituo vya afya na hospitali sambamba na upatikanaji wa huduma bora za afya zikiwamo dawa na huduma nyingine za kibingwa.

Msukumo mkubwa umewekwa pia kuhakikisha kila mmoja anafikia huduma hizo kwa kusogeza huduma za bima ya afya kwa viwango mbalimbali na masharti nafuu ili watu wengi wazipate wakiwamo wazee wasiojiweza kupatiwa bure.

Aidha umuhimu wa kuzingatia utu wa watu kama kipaumbele ndio pia umeifanya serikali kuhakikisha kila mtu anapata haki ya elimu na hivyo, kuanza kutekeleza sera ya elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi kidato cha nne.

Kitabu hicho cha CPT kinasema: “Ukuaji wa uchumi pekee hauwezi kutuonesha kama jamii imeendelea au la, hata ikiwa ustawi wa hali ya maisha unawafikia watu wote au baadhi. Kipimo cha kweli kwa taifa ni kuona kama wote wananufaika na maendeleo yaliyofikiwa.”

Kinaongeza: “Watu kwanza; ni katika mwelekeo na nia ya kuongeza uwezo wa watu kuzalisha, kuwa wabunifu na wadadisi huku wakijiamini na kuthubutu…”

Mintarafu suala hili, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima, anasema wakati akifunga mafunzo hayo mwishoni mwa juma kuwa, ni wakati kwa vijana na wananchi kwa jumla, kuwezeshwa kimazingira na kimtaji ili wapate nguvu ya kuushinda umaskini na kila mmoja kushiriki kukuza uchumi wa nchi. Dk Kitima anasema: “ndiyo maana Kanisa Katoliki linajikita zaidi pia katika kuelimisha watu kuhusu kipato cha mtu mmoja mmoja.”

Anasema mazingira yaimarishwe ili kila mmoja atumie rasilimali zilizopo nchini kama bahari, visiwa, vivutio vya utalii kuzalisha uchumi kwa faida yake na taifa kwa jumla, ndiyo maana hata wanasiasa watakapokuja tuwaulize watatufanya tuwe washiriki katika uchumi, au wanatuengua na kutudhoofisha kama mtu mmoja mmoja na kama taifa.

“Jamii likiwamo Kanisa Katoliki linataka hata bajeti zetu ziguse maisha ya mtu mmoja mmoja hivyo, tutumie fursa mbalimbali zilizopo na zinazojitokeza,” anasema Dk Kitima na kuongeza: “Kwa mfano, baada ya corona kuna fursa kubwa zimekuja, sasa tujiulize, tumewekeza vya kutosha kuzitumia?... Lazima tuisaidie serikali kuona fursa zitakazotusaidia na sisi.”

Anazitaka balozi mbalimbali za Tanzania kushiriki zaidi kupanua masoko nje ya nchi na kunadi bidhaa na fursa za kiuchumi zilizopo Tanzania ili zipenye katika mataifa mengine.

“…Tuzingatie kuwa hakuna nchi iliyojikomboa kiuchumi kwa kutegemea wageni,” anasema na kuongeza: “Tujiulize hata katika sekta binafsi ya wazawa, ni lini tutatengeneza kamera au pikipiki (bidhaa) zetu wenyewe; lakini kama kipindi hiki cha corona tumeweza kutengeneza ‘sanitizer’ kwa nini tushindwe vitu vingine?”

Kwa munibu wa Dk Kitima, sekta binafsi ya wazawa itaimarika pia kwa wananchi kupenda kutumia huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini na wazawa ili kuongeza ajira na mzunguko wa fedha nchini.

“Kwa mfano, Watanzania wengi hatujui kuwa kusomesha mtoto nje ya nchi ni kuondoa ajira nchini na kupeleka pesa nje maana wanafunzi wana mchango mkubwa katika uchumi wa nchi; lazima kila tukio tulitafakari kuichumi; faida na madhira yake,” anasema Dk Kitima.

Anawahimiza vijana kuanzisha miradi mbalimbali ikiwamo ya biashara, lakini anatahadharisha: “Vijana msianzishe biashara kwa kiwango kikubwa ghafla, bali hatua kwa hatua ili kupata uzoefu na biashara iwe yako; au na mkeo au mtoto, mwenzako mshirikishe akuletee bidhaa umlipe siyo eti kuchangia; mara nyingi kuchangia hamfiki mbali kwa kuwa kila mmoja ana mawazo yake…”

Katika michango ya washiriki, ilipendekezwa ufanyike utafiti zaidi kubaini kiasi (idadi) ya wanaochangia kukua kwa uchumu wa nchi ili ukuaji wa uchumi usiwe unabebwa na watu au sekta chache zikiwamo madini, utalii na mawasiliano pekee huku wengine wakiwa watazamaji huku sekta nyingine zikiwamo biashara ndogondogo, ufugaji, kilimo, madini, michezo, sanaa na nyingine.

Ntui anasema: “Mafunzo vyuoni yawe na tija zaidi kwa kuzalishja wahitimu ambao soko linawahitaji, kuliko hali ilivyo sasa ambapo wahitimu wengi soko la ajira linawakataa na ndiyo sababu, ajira ni chache ukilinganisha na wahitimu kila mwaka.”

“Tufike mahala badala ya wanavyuo kwenda ‘field’ (mafunzo kwa vitendo), tuwe na mfumo ambapo mwanafunzi anasoma huku akiwa ‘attached’ (amejishikiza) katika soko la kazi ili aoanishe elimu na soko… Hii inamaanaisha kuwa na ufundishaji wa maarifa na vitendo zaidi kuliko maneno na kujaribu sokoni.”

Anafafanua: “Matatizo ya kampuni au taasisi ndiyo yawe ‘assignment’ za wanafunzi kwa sababu wanafundishwa ili waingie katika soko kwa lengo maalumu siyo tu, kuhitimu.”

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi