loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Chikichi itamaliza changamoto ya kuagiza mafuta ya kula nje’

KATIKA ilani yake ya uchaguzi inayomalizika mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi kiliahidi kuielekeza serikali yake kuhakikisha taifa linajitosheleza kwa chakula; kuimarisha uchumi; kuongeza kipato cha wakulima; kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda; na kuongeza ajira kwa wananchi.

Kupitia ibara ya 22 ya ilani hiyo, CCM iliwaahidi wapigakura kuielekeza serikali kuboresha mfumo wa utafiti wa kilimo nchini ili matokeo ya tafiti hizo, pamoja na mambo mengine, yawafikie wakulima kwa kugundua na kutathmini aina za mbegu bora za mazao zenye sifa ya kutoa mavuno mengi.

Kwa upande wa chikichi ambalo ni moja ya mazao ya kimkakati, ukisoma makala haya hadi mwisho utaona namna ambavyo ilani ya CCM imefuatwa vyema katika eneo hilo.

Mei 23 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua upandaji wa miche bora ya chikichi aina ya tenera inayotoa mazao mengi pamoja na ugawaji wa miche hiyo, mkoani Kigoma.

Majaliwa aliweka wazi kwamba hatua ya kuzindua upandaji wa miche hiyo bora inatokana na jitihada za Rais John Magufuli kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM iliyomfanya akaagiza kwamba ni lazima serikali ifufue zao la chikichi.

Kutokana na Tanzania kulazimika kuagiza asilimia zaidi ya 50 ya mafuta ya kula nje na kutumia dola milioni 445 mpaka 470 kila mwaka, Waziri Mkuu anasema serikali inataka kuona wananchi wengi zaidi wanalima chikichi, zao ambalo hutoa mafuta mengi kulinganisha na mazao mengine ya mafuta kama alizeti, karanga, nazi, ufuta, pamba na kadhalika.Waziri Mkuu anasema mkoa wa Kigoma umebahatika kuwa na ardhi nzuri ya kulima chikichi na kwamba hata wananchi wa Kigoma wanapenda pia kulima zao hilo na wanachohitaji ni kusaidiwa.

Anasema hali ya hewa ya Kigoma kwa ajili ya kilimo cha chikichi ni nzuri na kwamba mti unapopandwa unakua wenyewe huku kazi ya mkulima ikiwa ni kuwekea kisahani ili uendelee kusitawi vizuri.

Waziri Mkuu anampongeza Mbunge Peter Selukamba ambaye kila mara amekuwa akiikumbusha serikali kuhusu kutolitega mgongo zao la chikichi.

Anasema Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imefanya kazi nzuri ya kutafiti mbegu bora ya michikichi inayotoa mafuta mengi ikilinganishwa na ile ya zamani aina ya dura ambayo inatoa mafuta kidogo.

Anasema serikali ilipoanza kuboresha zao la chikichi, iliangalia pia historia ya mkoa wa Kigoma na nchi kwa ujumla na kuona kuwa, Tanzania ndio nchi ambayo wakati fulani ilikuwa juu kwa kilimo cha chikichi duniani.

“Leo hii duniani nchi ya Malaysia inaongoza kwa uzalishaji wa mafuta ya mawese wakati Malaysia walipata mbegu hapa Kigoma.

“Kulikuwa na askari mmoja wa Malaysia alikuwa nchini Kongo kwenye vita baada ya kumaliza mapigano alisafiri akaja Kigoma akaona zao la chikichi akatamani kuchukua mche. Aliubeba akapeleka kwao, leo ndio wanaongoza duniani kwa kulima zao hili kwa kiasi kikubwa,” anasema na kuongeza kwamba Watanzania wanaweza kuipuku siku moja Malaysia.

Mbali na waziri mkuu kupanda mche, wabunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko walishiriki pia kupanda mbegu.

Wengine walioshiriki ni viongozi wa taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Tari Taifa, Dk Geofrey Mkamilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Tari, Dk Yohana Budeba na wengineo. Waziri Mkuu anasema jitihada za serikali katika kuhakikisha chikichi inasimama kwa kasi kubwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha utafiti wa kilimo cha zao hilo kilichoko Kihinga. Kwa hatua iliyofikiwa, Majaliwa anawataka wananchi wa Kigoma kuandaa mashamba ili wapate miche bure.

“Kitakachofanyika kwa kila halmashauri kila anayetaka kulima chikichi, kwanza aandae shamba kisha amwone ofisa kilimo wa kata yake ili akalione shamba. Yeye ndiye atatoa kikaratasi cha kwenda kwenye kitalu kupata mbegu bure,” anasema.

Anasema serikali inataka kujua wakulima wangapi wamelima chikichi ili huduma nyingine zote wazipate ikiwemo za pembejeo na ushauri wa kitaalamu na wanaolima mashamba makubwa wapate fursa ya kukopa kwenye benki ya kilimo.

“Rais ana matumaini makubwa kwa sababu toka tumeanza kuzalisha miche tumeona hamasa ya wana Kigoma. Ana matumaini makubwa sana nanyi. Na ana matumaini makubwa kuwa zao hili Kigoma litakuwa ndio mkoa wa kwanza wa mfano ili baadaye twende huko Kilosa, Lindi na Mtwara wanakolima nazi lakini chikichi pia inastawi,” anasema.

Anawataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi na maofisa kilimo kuwasaidia wakulima ili walime chikichi kitaalamu huku wakiwasaidia wale wenye michikichi iliyozeeka kuanza kuipunguza kidogo kidogo kwa kupanda mipya.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba anasema mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni takribani tani 570,000 na kwamba kati ya hizo takribani tani 365,000 huagizwa kutoka nje ikiwemo tani 370,000 za mawese.

Anasema Tanzania huzalisha tani 40,500 za mafuta ya mawese kwa mwaka. Kati ya tani hizo mkoa wa Kigoma unazalisha tani 31,750 katika mashamba yenye ukubwa wa hekta 19,640.

Kwa sasa uzalishaji wa mawese kwa hekta ni wastani wa tani 1.6, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na tani nane hadi tisa za mawese kwa hekta ambazo huzalishwa katika baadhi ya nchi ikiwemo Malaysia na kwamba matumizi ya mbegu bora za tenera yanatupeleka huko.

“Pamoja na kutumika kama mafuta ya kula, mawese pamoja na mazao yake mengine yana matumizi mbalimbali yakiwemo kutengeneza sabuni, mishumaa, gundi, pombe, mbolea, nishati na shampoo,” anasema.

Mgumba anasema zao hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za uzee wa miti ya michikichi, usindikaji duni wa mafuta, zana duni za kilimo na ukosefu wa elimu ya kilimo bora.

Anasema changamoto hizo zinatazamiwa kufanyiwa kazi na kituo cha utafiti na uendelezaji wa zao la chikichi cha Tari-Kihinga mkoani Kigoma. “Ili kupeleka huduma karibu na wananchi katika Ukanda wa Mashariki, Kusini na Nyanda za Juu Kusini, wizara imeanzisha mashamba mama ya miti vizazi vya chikichi kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza mbegu kwa wakulima katika maeneo hayo.

“Kwa ukanda wa Mashariki, shamba mama lenye ukubwa wa eka tano limeanzishwa kwenye Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ilonga Morogoro. Ukanda wa Kusini shamba lenye ukubwa wa eka nane limeanzishwa katika Kituo cha Utafiti Naliendele Mtwara na Nyanda za Juu Kusini shamba lenye ukubwa wa eka tano limeanzishwa katika kituo kidogo cha utafiti wa Kilimo Kikusya katika wilaya ya Kyela Mbeya,” anasema.

Anaongeza kuwa juhudi za kuanzisha mashamba mama katika kanda nyingine zenye fursa ya kulima chikichi kama vile Kanda ya Ziwa zinaendelea.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tari, Dk Yohana Budeba anasema Wizara ya Kilimo kupitia taasisi hiyo imefanikiwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Majaliwa la kupanda michikichi ya kisasa.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo anasema hatua wanayochukua anaamini italeta mafanikio kwa kuwa licha ya kutoa mafuta kidogo, miche mingi ya michikichi mkoani Kigoma ilipandwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na hivyo imezeeka Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), ambaye ni mjumbe wa bodi ya Tari, Amos Nungu anasema tume hiyo inasimamia shughuli za utafiti nchini, hivyo kwenye utafiti wa mbegu bora ya michikichi walifadhili Sh milioni 120.

“Tunakwenda hatua kwa hatua. Hatua ya kwanza watafiti wameweza kuzalisha mbegu bora zenye uwezo wa kutoa tani sita za mafuta kwa hekta, sasa wataandikia tena kwa ajili ya kufanya maboresho zaidi ya utafiti huo ili zitoe mafuta mengi zaidi ya hapo,” anasema.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi