loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Idris Sultan anusurika kupelekwa mahabusu

MSANII wa vichekesho, Idris Sultan, leo ameponea chupuchupu kupelekwa mahabusu baada ya kuchelewa kufika mahakamani kusikiliza shauri linalomkabili.

Hayo yamejiri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambako Idris anakabiliwa na mashitaka ya kurusha maudhui mtandaoni bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaid, Idris alipoulizwa alikuwa wapi alisema alishikwa na dharura ya kuumwa tumbo ghafla, jibu ambalo lilionesha kutomridhisha hakimu.

“Nina hakika haukuwa unaumwa tumbo kama unavyosema, kama suala la kuwahi linakupa shida sema tuna magari ya serikali yanaweza kukusaidia,” alisema Hakimu Shaid akimaanisha kumweka mahabusu Idris ili awe anapelekwa mahakamani kwa magari ya magereza.

Baada ya kumweleza hayo, Hakimu Shaid alifuta hati ya kumkamata Idris ambayo aliitoa awali kabla msanii huyo hajaingia mahakamani hapo na baadaye akaahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, mwaka huu.

Idris na wenzake wawili wanakabiliwa na mashtaka ya kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na kibali cha TCRA, makosa wanayodaiwa kuyatenda kati ya Machi 18, 2016 na Machi 12, mwaka huu.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Dokta Ulimwengu na Isihaka Mwinyimvua, ambao kwa pamoja na Idris wanadaiwa kuchapisha maudhui katika TV ya mtandaoni kwenye akaunti ya Lokomotion bila kibali cha TCRA.

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wametajwa katika tetesi ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi