loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ni vita Simba, Yanga, Azam

MZUNGUKO wa 31 wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara unahamia kwa Simba, Yanga na Azam FC leo kwenye viwanja tofauti wakitarajiwa kupambana kwa ajili ya kupigania pointi tatu muhimu.

Mabingwa watetezi Simba watakuwa wageni kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kuumana na Mbeya City, mchezo unaotazamwa kuwa mgumu hasa kwa wenyeji walioko hatarini kushuka daraja tena wakitoka kupoteza mchezo uliopita bao 1-0 dhidi ya Alliance mwishoni mwa wiki iliyopita.

Simba ambao ni vinara wa ligi hiyo wala hawana presha kwani wao wanahitaji pointi tisa tu ili kutangaziwa ubingwa mapema na hesabu zao zitaanza kuhesabika kuanzia mchezo huo kama watashinda.

Wekundu hao hawakamatiki kwani wanaongoza ligi wakiwa na pointi 75, wakijivunia safu bora ya ushambuliaji iliyofunga jumla ya mabao 67 na safu ya ulinzi iliyofungwa mabao 16 ikiwa ndio timu pekee yenye mabao mengi ya kufunga na machache ya kufungwa.

Wametoka kushinda mchezo wao uliopita dhidi ya Mwadui mabao 3-0, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hali itakuwa mbaya kwa wenyeji wanaoshika nafasi ya 18 wakiwa na pointi 30 kama watafungwa, basi jahazi litazidi kuzama.

Timu hii inaonekana dhaifu kwenye safu yao ya ulinzi kutokana na takwimu kuonesha kufungwa mabao mengi 36 kuliko waliyofunga wao 22.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana Dar es Salaam mzunguko wa kwanza, Simba ilishinda mabao 4-0. VITA IKO HAPA Vita kubwa katika timu zinazoongoza ipo kwa Yanga, Azam FC na Namungo, ambazo zinatofautiana kuanzia pointi mbili hadi nne.

Yanga inatarajiwa kuchuana na Namungo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ni mchezo mgumu kutokana na ubora wa kila timu rekodi zao zikionyesha wote wameshinda michezo 15 kati ya 30, sare 11 za wenyeji kwa tisa, mmoja amepoteza michezo minne na mwingine sita lakini wageni hao wa Ruangwa wakiwa na mabao mengi ya kufunga 38 na kufungwa 27 na Yanga wakifunga 33 na kufungwa 21.

Yanga ikiwa na pointi 56 katika nafasi ya pili na Namungo 54, hivyo kama watashinda, watamuombea njaa Azam FC wapoteze leo dhidi ya Kagera ili wapande nafasi ya pili, lakini pia wakifungwa, Namungo itamshusha kutoka nafasi ya tatu hadi ya nne.

Mara ya mwisho kukutana kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini Lindi, timu hizo zilitoka sare ya 1-1. Kila timu ina ubora wake na kila mmoja ana nafasi ya kuibuka na ushindi, hakuna

wa kumbeza mwenzake. Yanga inaweza kuwa na presha hasa baada ya kutoka kupata sare mbili mfululizo dhidi ya JKT Tanzania bao 1-1 na dhidi ya Azam FC 0-0 hivyo, kama wataruhusu kufungwa au kupata sare, mambo yatazidi kuwa magumu kwao katika kugombea nafasi ya pili. Vita nyingine itakuwa ni Azam FC dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Azam wanajua umuhimu wa mchezo huo kwao ili kuendelea kulinda nafasi ya pili na kama watashinda watabaki hapo lakini wakipoteza na Yanga inayowafukuzia ikashinda, basi watakuwa kwenye presha zaidi.

Mara ya mwisho Kagera iliilazimisha Azam FC sare ya bila kufungana kwenye mzunguko wa kwanza. Na timu hiyo imekuwa haitabiriki inapokutana na vigogo, imekuwa ikikaza. Kabla ya mechi za jana, Kagera ilikuwa inashika nafasi ya tisa kwa pointi 41 na mchezo uliopita imetoka kupoteza dhidi ya Namungo kwa kufungwa mabao 2-0.

Inahitaji kushinda pia, la sivyo, inaweza kushuka nafasi iliyopo ikiwa wengine waliofuatana watashinda mechi zao. Kutakuwa na mchezo mwingine Alliance dhidi ya Polisi Tanzania. Ni mchezo unaoweza kuwa mgumu, hasa kwa wenyeji hao wa Mwanza wanahitaji ushindi kutoka hatarini kwa kuwa wanashika nafasi ya 17 kwa pointi 32 ambazo haziwatoshi kuwa salama.

Alliance licha ya kutoka kushinda mchezo uliopita ugenini dhidi ya Mbeya City bado haitoshi, wanahitaji ushindi mechi zijazo kujihakikishia nafasi ya kubaki. Biashara United itakuwa mwenyeji wa KMC kwenye Uwanja wa Karume, Musoma, mkoani Mara.

Kila mmoja anahitaji matokeo ili kupanda na atakayefanya vibaya hana uhakika wa kubaki nafasi aliyopo, kwani anaweza kushuka kutoka nafasi ya moja kwenda nyingine au kubaki alipo

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wametajwa katika tetesi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi