loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kushindana na JPM ni kutumia vibaya rasilimali fedha, muda

MWALIMU Nyerere alipata kusema kwamba, katika zama hizi tulizonazo, mtu kuzungumzia umuhimu wa kurudi kwenye siasa ya ujamaa, unapaswa kuwa na kichwa kama cha mwendawazimu.

Mwalimu ambaye kwa maelezo yake alikuwa anatembea na kitabu cha Azimio la Arusha kilichosheheni misingi ya ujamaa na kujitegemea pamoja na Biblia Takatifu, alimaanisha kwamba ujamaa bado ni itikadi sahihi kuifuata, lakini kwa jinsi mitazamo ya Watanzania ilivyobadilika ni vigumu kuwashawishi.

Kwamba Watanzania wengi wamekumbatia uliberali (ubepari), bila kujali madhara yake kwa wanyonge wa nchi hii na hivyo kuwaambia tena habari za ujamaa wanabaki wakikushangaa tu.

Wasiokumbuka ni kwamba, hatua ya nchi yetu kuachana na ujamaa bila kuweka miiko ya uongozi ndiyo iliyosababisha ufisadi wa kutisha ulioitafuna nchi yetu kwa takribani miongo mitatu iliyopita.

Tumshukuru Rais John Magufuli ambaye amekomesha saratani hii hatari.

Andiko hili halikusudii kuelezea umuhimu wa ujamaa, bali kuonesha kwamba yapo mengi yanayotufaa tukiwa Watanzania na kama Waafrika, lakini kinachoitwa demokrasia na kukumbatia mitazamo ya kimagharibi vinatufanya hata mambo mazuri kwetu tuyaone mabaya au yaliyopitwa na wakati. Mfano wa hayo ni pamoja na mtu kusimama hadharani na kueleza faida za kuoa wake wengi au kuzaa watoto wengi.

Najua hata wewe unayesoma hapa umeanza kunishangaa, lakini ukweli ni kwamba kuna faida kadhaa za kuoa mitala ingawa Wazungu wanataka kutuaminisha kwamba eti ushoga ni bora kuliko mwanaume kuoa wake wengi. Ingawa si mada yangu, lakini faida moja tu kati ya nyingi ya kuoa mitala na hasa kwa kuzingatia kuwa wanawake ni wengi kuliko wanaume ni kuwanusuru wanawake ambao hawatabahatika kuolewa endapo kila mwanamume ataoa mke moja ili wasigeuke kuwa ‘mali ya umma’.

Ni vyema pia nimshukuru Rais John Magufuli kwa kuwahimiza Watanzania kuzaana zaidi huku wakizingatia uwezo wa kuzalisha mali na kuhudumia familia kwani ilianza kuwa ‘fasheni’ ya sisi Waafrika tulioko Tanzania kutaka kuzaa ‘katoto kamoja’ au ‘viwili’ huku kila siku

Wazungu wakituhimiza uzazi wa mpango, wakati wenzetu kumbe wana hofu kubwa na kuongezeka kwetu! Tuyaache nayo, tuje kwenye mada niliyoikusudia leo ambayo ni kuendekeza hii kasumba inayoitwa demokrasia katika muktadha wa kinachoitwa vipindi vya utawala na uchaguzi hata pale ambapo hakuna umuhimu. Mtu mmoja alipata kuandika kwamba, Waafrika wengi bado tunaishi kiporipori.

Akasema bado tuna ubinafsi mwingi, uchoyo, ukabila na hata udini; mambo yanayosababisha wakati mwingine kuuana hovyo.

Akasema tunapofanikiwa kupata kiongozi mwadilifu na anayeguswa kwa dhati na maendeleo ya wanyonge kama ilivyokuwa kwa Kanali Muammar Gaddafi pale Libya, tumruhusu atutawale hata kama ni kwa mkono wa chuma ingawa Wazungu hawatompenda na kundi dogo la wananchi lenye uchu wa madaraka.

“Ukiruhusu demokrasia ya vitabuni, hapakaliki. Nadharia za demokrasia ni nzuri sana, lakini haziwezi kufaa kila mahala,” akaandika huyo mtu. Mwingine pia alipata kuandika hivi:

“Demokrasia siyo kama Coca- Cola kwamba ilivyo Cola ya Brazil ndivyo ilivyo ya Kenya au USA. Demokrasia na kitu kinachoitwa haki za binadamu ni dhana za Wazungu kuidhibiti Afrika.” Bila shaka mwandishi alimaanisha kwamba, wakati mwingine wanatumia dhana hizo kutuwekea vibaraka wa kulinda maslahi yao. Huyo mtu akazidi kuandika:

“China hakuna demokrasia wala kinachoitwa haki za binadamu, bali kuheshimu haki na ulinzi wa rasilimali zao na sote tunaona walikofika.”

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Watanzania ‘tulilamba dume’ kwa kuchagua rais ambaye hata aliyekuwa Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde, hivi karibuni alikiri bungeni mjini Dodoma kwamba kwa kipindi kirefu hata wapinzani waliamini kwamba ndiye anayefaa kuongoza Tanzania.

Akasema, pamoja na kumpiga kinafiki, wakikaa kwenye vikao vyao wanakiri kwamba Magufuli ni kiboko, amewafilisi kila hoja. Kila walicholalamikia yeye anajibu kwa vitendo.

Akawakumbusha Watanzania kufuatilia hotuba za miaka mitano za wapinzani kwamba takribani yote waliyolalamikia Magufuli anayafanya kwa vitendo.

Silinde akataja baadhi ya hayo kuwa ni kutaka nchi kuwa na ndege zake, kuwa na reli ya uhakika, meli katika maziwa, umeme, maji, elimu bure, kukomesha ufisadi na kadhalika, mambo ambayo sasa hivi Magufuli anayafanya.

Kimsingi ninachotaka kusema ni kile ambacho baadhi ya wabunge walishawahi kukisema bungeni hadharani na wenye kasumba zao za umagharibi wakabaki kuwashangaa.

Wabunge wamependekeza wapinzani kukubali Rais John Magufuli apite bila kupingwa kama ambavyo TLP ya Augustine Mrema tayari kimeshapitisha kwamba Magufuli ndiye mgombea wake.

Katika Bunge lililopita, baadhi ya wabunge waliona kwamba ilikuwa ni jambo jema wapinzani kukubali Magufuli apite bila kupingwa ni pamoja na Abdallah Bulembo, Nape Nnauye, Livingstone Lusinde na hata Silinde aliyependekeza Magufuli atawale angalau kwa miaka 20 mfululizo.

Bulembo anasema: “Nilibahatika kushiriki katika kampeni za bwana mkubwa wakati anatangaza ilani na baadaye kukabidhiwa kijiti.

Aliyatangaza yaliyokuwa kwenye ilani na mengine… nikamuuliza mbona kama umejitwisha mzigo mzito, haya yatawezekana? Akanijibu, nakuahidi tena ndani ya mwaka mmoja yatawezekana.

Sasa mwenye macho haambiwi tazama.” Bulembo akawataka wapinzani wakubali Rais Magufuli apitishwe bila kupingwa kwani utekelezaji wa ilani unaonekana, aliyoyafanya yanaonekana wazi na kwamba kila akitazama upande wa upinzani haoni kama wana mgombea makini wa urais.

Kisha akasema jambo ambalo ni la uhakika lakini sijui kwa nini wapinzani wameshindwa kuunga mkono:

“Badala ya kutumia fedha nyingi kwa ajili ya uchaguzi (wa Rais), fedha hizo ziende kwenye kukabiliana na corona (na huduma nyingine kwa wananchi) halafu wabunge na madiwani ndio wagombee. Nyiye (wapinzani) kikubwa mkipata wabunge si mnaongeza pato, kwani pato si linatokana na ubunge lakini siyo urais?”

Alishauri Bulembo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wazazi (CCM). Hili jambo alilosisitiza Bulembo ni la kweli kabisa na kama kweli wapinzani wana uchungu na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi yetu, ulikuwa ni wakati wa kufanya kama Mrema maana ni ukweli ulio wazi kuwa, kupambana na Magufuli ni matumizi mabaya ya rasilimali fedha na muda.

Bulembo anasema: “Tukubaliane vyama vyote vya upinzani kama mna mtu atakayeweza kumshinda Magufuli… Kwa nini kupoteza fedha wakati mnakwenda kushindana na jiwe, haina sababu. Tuje humu tuwekeane taratibu Magufuli apitishwe, tufanye uchaguzi wa wabunge na madiwani ili tuokoe fedha zitumike kwa mambo mengine.”

Mwaka jana Aprili, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ndiye aliyeanza kuweka mezani hii hoja.

Alisema kwamba ni kupoteza muda kwa kuendesha uchaguzi wa Rais wakati ikiwa inajulikana dhahiri kwamba kwa kazi aliyofanya Magufuli, hakuna mpinzani anayeweza kushindana naye. Lusinde akasema:

“Mimi nawaomba wabunge na Watanzania wote, hivi kwa nini mwakani (mwaka huu) tusifanye uchaguzi wa madiwani na wabunge tu na Rais akapita bila kupingwa?

Wakati anaapishwa tumkabidhi hundi ya fedha ambazo taifa limeokoa ili aende kuzitumia kuondoa matatizo ya maji na barabara vijijini!”

“Kuna faida gani kwenda kupoteza fedha kwa uchaguzi wa Rais ambaye hana mpinzani… Sisi ni wabunge, tunatokana na familia masikini, tusisahau hilo. Watu maskini wanajinyima, badala ya kula milo mitatu wanakula mlo mmoja. Kwa nini na sisi tusijinyime kwa kula mlo wa madiwani, mlo wa wabunge na Rais apite bila kupingwa?

” Kimsingi, hakuna chama kinachoweza kumtengeneza mgombea sasa hivi akashindana na Magufuli hata kama ni wale waliofukuzwa au watakaojitoa CCM. Hakuna. Kwa vile hilo la kuweka mazingira ya kumpitisha Magufuli apite bila kupingwa limeshindikana bungeni, ni vyema sasa vyama vikafanya kama Mrema. Kukubali ukweli mchungu na kutoweka mgombea.

Kwa kutoa hoja hii, kuna watakaokuwa wanaona ni kutoitendea haki demokrasia lakini, kama nilivyoanza makala haya, sisi kama Waafrika, hatuwezi kung’ang’ania kinachoitwa demokrasia ya vitabu iliyoletwa na Wazungu wakati haina maana yoyote kwa wakati huu. Hata wale wanaosema kwamba kwa kupata kiongozi kama Magufuli ambaye mataifa wengi wanatamani kuwa naye, alipaswa kuongoza nchi yetu angalau kwa miaka 20 nao wana hoja ya msingi kabisa. Tuchukulie mfano wa China.

Baada ya kugundua kwamba Rais wa sasa, Xi Jinping, anafanya mambo makubwa kulinganisha na marais wengine waliopita baada ya Mwenyekiti Mao Zedong, hivi karibuni waliamua kumpa hadhi kama hiyo ya Mao.

Hata mimi kwa mtazamo wangu, baada ya Mwalimu Nyerere, hapo katikati zimepita awamu nyingine za uongozi ambazo zimefanya makubwa, lakini Magufuli amekuwa zaidi.

Tunaweza kufikiria siku moja kumpa heshima kama ya Baba wa Taifa aliyetawala nchi yetu kwa zaidi ya miaka 20 na kutujengea misingi mizuri tunayojivunia hadi leo hususani umoja wetu, mshikamano na amani.

Demokrasia ambayo haina tija kwetu hatuna sababu ya kuikumbatia kila wakati. Watakaodhani kwamba kusema hivi ni sawa na uendawazimu, warejee tena kusoma makala haya kwa umakini!

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

1 Comments

  • avatar
    Fadhili
    24/06/2020

    Ulichoandika hata hakiendani na kichwa cha habari. Hii ni porojo ya waandishi uchwara ambao wanafaidika na propaganda za kidikteta. Jifunze kuwatendea haki watanzania kwa kutumia elimu uliyonayo.

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi