loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

CCM bila kitanzi cha ahadi hewa

“SASA kumekucha… kada wa CCM apewe kura za ndiyo”, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole anaimba wimbo huu wa hamasa kuashiria kuanza kwa mchakato wa uchaguzi.

Mbele ya waandishi wa habari, Polepole anatangaza kuanza kwa uchukuaji na urudishaji wa fomu za kuwania udiwani, uwakilishi, ubunge na urais Tanzania Bara na Zanzibar, ndani ya chama.

Kwa upande wa urais, dirisha liko wazi kuanzia Juni 15 hadi 30 mwaka huu. Matakwa ya Katiba yanayompa kila Mtanzania nafasi sawa ya kuomba ridhaa ya wananchi kuongoza nchi, yamezingatiwa kuruhusu wanaotaka kugombea, wachukue fomu.

Hata hivyo, CCM ina utaratibu uliozoeleka tangu mwaka 1985 ambao kila anayepitishwa kugombea urais, anapewa kipindi kisichozidi miaka 10 kuongoza nchi kisha anamuachia mwingine.

Kupokezana kijiti chini ya utaratibu huo kumedumu tangu Rais Ali Hassan Mwinyi alipopewa ridhaa ya kuongoza kutoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1985, kisha naye kumwachia nafasi hiyo Benjamin Mkapa mwaka 1995. Naye Mkapa akafanya hivyo kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005.

Utaratibu huo umekubalika si tu ndani ya chama, bali pia kwa umma wa Watanzania ambao hautegemei mgombea tofauti na RaisJohn Magufuli wa kupeperusha Bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Magufuli ameshachukua fomu kuomba kuteuliwa na chama kugombea urais kwa kipindi cha pili. Ameomba wanachama wamuombee katika safari yake ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro hicho.

Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza rasmi kuanza kampeni za uchaguzi, Rais Magufuli ataungana na wagombea wengine kutangaza sera zao kuomba ridhaa ya wananchi.

Wakati vyama vingine vikitarajiwa kueleza vitafanya nini kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu, kwa upande wa Magufuli, atakuwa akionesha umma wa Watanzania mambo aliyofanya tangu mwaka 2015 alipopewa ridhaa ya kuongoza nchi hadi sasa.

Safari ya Rais Magufuli ya kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huu mkuu inaainishwa na watu mbalimbali kuwa ni nyepesi kutokana na alivyotekeleza ahadi zake.

“Mara nyingi binadamu wanakupima kwa tija. Kama anajitahidi kutatua changamoto zilizowakabili wananchi, ni dhahiri atashinda. Tunakwenda kwenye uchaguzi ambao tayari unajua mtu gani atashinda,” anasema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Keregero Chirongo akirejelea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya elimu.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja anaweka bayana kwamba, kazi ya Rais Magufuli itakuwa ni kuainisha mambo makubwa yaliyofanywa na serikali yake huku mengi yakionekana wazi kwa wananchi. Kada wa CCM, ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili wa UDOM, Samson Mwigamba anasema:

“Sisi kama wanachama tunafurahi kuwa na mgombea asiye na deni la ahadi kwa wananchi. Ukweli, uchapakazi na mafanikio ndiyo yanambeba Rais Magufuli katika kinyang’anyiro cha urais.”

Miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanywa na serikali katika miaka mitano yanayotarajiwa kuwa kete katika kinyang’anyiro, yanawekwa wazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 19 wa Bunge hivi karibuni kabla ya Bunge la 11 kuvunjwa hivi karibuni.

Mafanikio hayo ni pamoja na kurekebisha nidhamu kwa watumishi wa umma, uwajibikaji serikalini, uwepo wa miradi mingi ya kimkakati hadi kwa wananchi wa kawaida, mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Serikali na nje ya Serikali kulinda mali na fedha za umma.

Mengine ni kwenye mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, utambuzi wa watumishi hewa na kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo wenye vyeti feki, ongezeko la mapato, ongezeko la viwanda, kuimarisha masoko na kilimo cha mazao makuu.

Waziri Mkuu Majaliwa anaeleza serikali ilivyodhibiti biashara haramu na utoroshaji wa madini, kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma, kuboresha miundombinu na taaluma ya sekta ya elimu kwa ngazi zote kuanzia awali hadi elimu ya juu.

Serikali imeimarisha pia huduma za afya, ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme na usambazaji wa umeme vijijini. Mambo mengine ni ujenzi wa barabara nyingi kwa kiwango cha lami, madaraja, bandari, ukarabati wa meli na ujenzi wa mpya wa meli katika maziwa makuu.

“Kwa namna ya pekee kabisa nitumie fursa hii kumpongeza Rais John Magufuli kutokana na fikra na uongozi makini katika ujenzi wa taifa letu… Maono yake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 - 2020 na mipango ya serikali, imeleta mafanikio makubwa ambayo sasa wote tunayaona,” anasema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Rais Magufuli katika hotuba ya kuvunja Bunge la 11 hivi karibuni, alieleza anavyofarijika kwa kuona mambo mengi ambayo serikali imefanikiwa kuyatekeleza.

“Kazi kubwa imefanyika… Tumefanya mengi sana ambayo nikianza kuyaelezea yote hapa tunaweza kukesha,” akasema Magufuli na kuongeza kuwa, bahati nzuri Watanzania wengi wameona na wanajua. Ana imani kubwa kuwa, Watanzania wataendelea kumwamini pamoja na viongozi wengine na kuwapa dhamana ya kuongoza nchi katika vipindi vingine vijavyo.

Anahakikishia umma akisema: “Endapo wananchi wataendelea kutuamini, nchi yetu katika miaka mingine mitano ijayo tutafanya mambo mengine makubwa zaidi.”

Rais Magufuli anasema kwa kufanya mambo hayo watakuwa wametimiza ndoto na dhamira ya kuifanya Tanzania yenye uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi