loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli amefanya vyema kuhimiza utafiti mitishamba na tiba mbadala

Hivi karibuni Rais John Magufuli aliitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuimarisha nguvu na kutenga fedha zaidi kwa ajili ya Kitengo cha Tiba Asili / Tiba Mbadala ili kutengeneza dawa za asili kwa ajili ya kuponya magonjwa mbalimbali.

Wito huo wa Rais ambao umeitikiwa na Wizara ya Afya, umetolewa wakati ambao maneno ‘tiba mbadala’ yamekuwa yakifuatiliwa sana katika kipindi hiki cha virusi vya corona.

Licha ya kuwa katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Rais John Magufuli sekta ya afya imepata maendeleo makubwa na vituo vya afya zaidi ya 200 kujengwa, changamoto ya virusi vya corona imetukumbusha kuwa bado mifumo yetu ya afya ina udhaifu katika maeneo fulani, na hivyo tiba mbadala inaweza kuziba pengo lililoachwa na dawa za kimagharibi, wakati serikali ikiendelea kuboresha huduma za afya.

Kwa Tanzania, ugonjwa wa Covid-19 umekuja katika wakati mbaya, kwani kwa kiasi fulani umetibua kasi ya maendeleo ya uchumi na kuyumbisha ufuatiliaji wa watawala wetu kutoka kuendeleza uchumi wa nchi na kuuelekeza juhudi zao kwenye kulinda afya na maisha ya watu.

Busara kubwa imetumiwa na serikali yetu kuweka uwiano kwenye mambo hayo mawili, bila kuegemea zaidi upande mmoja sana na kufuata maagizo na kanuni za wataalamu wa afya katika kupambana na Covid-19.

Tukiangalia kwa undani, moja ya nyenzo zilizotoa mchango katika kuweka uwiano huo, ni matumizi ya dawa za asili. Mwanzoni baadhi ya watu hawakumwelewa Rais Magufuli aliposhauri wananchi kutumia tiba asilia zikiwemo za kujifukiza nyungu ili kukabiliana makali ya virusi vya corona.

Sasa wengi wanaona ulikuwa ni uamuzi wa busara, na matokeo yake tunayaona. Kama tungeendelea kung’ang’ania tiba za kimagharibi peke zinazohitaji pesa nyingi na rasilimali nyingine nyingi ukiwamo muda ambao ungetumika kwa uzalishaji, labda sasa tungekuwa tunazungumza lugha tofauti.

Ni kweli kuwa kwa muda mrefu tumejipanga zaidi kuwekeza kwenye tiba za kimagharibi, kwa kuwa tunaamini kwamba ni tiba za kisayansi na matokeo yake yana ushahidi wa kisayansi. Lakini, hii haina maana kuwa mitishamba yetu yenye ufanisi ambayo bado haijapita kwenye maabara za kisasa haina ufanisi.

Ndiyo maana Rais Magufuli amesisitiza kuimarisha nguvu kwenye utafiti wa tiba asili na tiba mbadala. Nikiangalia hapa China, baada ya mamlaka za nchi kuthibitisha kuwepo kwa virusi vya corona, wataalamu wa afya walikuwa mstari wa mbele kuandaa mpango wa kuhakikisha virusi havienei, vinadhibitiwa na kutokomezwa.

Serikali iliwasikiliza wataalamu na kusimamia utekelezaji wa hatua zilizopendekezwa na wataalamu wa afya. Moja kati ya mapendekezo hayo ni kutumia vizuri matibabu ya jadi ya Kichina (TCM).

China ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwenye mbinu za matibabu za kimagharibi na imetumia njia hizo vizuri sana, lakini haikusahau hata kidogo matumizi ya matibabu ya jadi na tiba mbadala kwenye kupambana na virusi vya corona.

Ukimuuliza Mchina yeyote anayefuatilia matibabu ya jadi, basi atakuwa anafahamu dawa zinazoitwa Lianhua Qingwen (vidonge), Jinhua Qinggan (ya unga) na Xuebijing (ya kudunga), hizi ni dawa zilizotumika kwa viwango tofauti kwa wagonjwa wa virusi vya corona, na ufanisi wake umethibitishwa kwenye maabara, pia na wagonjwa wenyewe.

Hata baadhi ya nchi jirani na China zimetumia dawa hizo za jadi na kupata ufanisi. Nyumbani Tanzania, kuna watu wamekuwa wakibeza ‘nyungu’ na matumizi ya mchanganyiko wa malimao, tangawizi, kitunguu swaumu na pilipili kichaa bila kujua kuwa wenzetu waliopata mafanikio kwenye vita hii ya corona, hawakusahau nyungu zao.

Kwa sasa wengi tunafahamu kuwa dawa ya aina ya Artemisinin ni dawa ambayo imethibitishwa na inatambuliwa na Shirika la Afya duniani WHO, kuwa inatibu malaria. Historia ya dawa hii ni mitishamba iliyokuwa inatumiwa na Wachina, walijua ina ufanisi fulani wa kimatibabu, lakini hakukuwa na ushahidi wa kisayansi.

Mtaalamu aliyepata tuzo ya Nobel, Tu Youyou, alifanya utafiti wa muda mrefu wa kimaabara na hatimaye kuthibitisha kuwa, mitishamba hiyo ina uwezo wa kutibu ugonjwa wa malaria na sasa dawa ya Artemisinin inatambuliwa kuwa ni dawa rasmi ya kutibu malaria.

Jambo la kufurahisha na kutia moyo zaidi ni kwamba, kutokana na serikali kutambua mchango wa dawa za jadi kwenye mapambano ya magonjwa ya kuambukiza, kama ‘nyungu’ na mcnganyiko wa malimau ilivyosaidia kwenye corona, serikali imeongeza bajeti ya wizara ya afya kwa ajili ya utafiti wa dawa za mitishamba kwa mwaka huu wa fedha.

Kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti wa dawa za asili iliyopo katika Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (ITM) na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR), Tanzania inaweza kupiga hatua kwenye sekta hiyo, na kuwa njia moja ya kujitegemea likitokea tatizo lingine kama hili.

Lakini vilevile tusisahau kuwa, maendeleo ya China kwenye sekta ya mitishamba na tiba mbadala, vinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi zetu za Afrika. China ina mfumo kamili wa utafiti, utengenezaji na matumizi ya dawa za mitishamba na tiba mbadala. Katika hospitali nyingi za China, kuna vitengo maalumu vya dawa za jadi na tiba mbadala.

Kuna wakati hata kwenye maduka ya dawa ya China ukinunua na kuangalia dawa za jadi zilivyofungashwa, huwezi kujua kama ni dawa za mitishamba au ni za kimagharibi, au ni za mseto. Wakati mwingine ukiuliza dawa imetengenezwa kwa mitishamba gani, utaambiwa ni mitishamba au mizizi adimu. Mitishamba hiyo inayoitwa adimu au mizizi inayoitwa adimu kwa wenzetu, inapatikana kwenye maeneo mengi ya Tanzania.

Kwa hiyo, tayari tuna mazingira mazuri ya rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya kutengeneza dawa hizo. Hivi karibuni tumesikia baadhi ya nchi za Afrika zikijaribu kutengeneza dawa za mitishamba kupambana na virusi vya Corona.

Jumuiya ya kimataifa na hasa Shirika la Afya Duniani (WHO) limetilia shaka dawa zote hizo. Mapema mwezi Machi, WHO lilirekebisha mwongozo wake wa awali kuhusu namna za kujikinga dhidi ya virusi vya corona, na kufuta moja ya mapendekezo yake kuhusu kutotumia dawa za mitishamba kujikinga au kutibu virusi hivyo.

Baadhi ya watu wamekuwa wakidhani huo ni ubaguzi wa kisayansi dhidi ya nchi za Afrika. Lakini sababu kubwa ya hatua hii ya WHO ni kwamba dawa hizo hazijapita kwenye utafiti wa kimaabara, na kuthibitishwa kuwa hazina madhara kwa matumizi ya binadamu na zinaweza kutibu.

Kibaya zaidi ni kuwa baadhi ya watu hata wamepoteza maisha kutokana kuweka imani kwenye dawa za mitishamba zisizo na ufanisi wa kimatibabu, au kutumia dawa za mitishamba bila vipimo maalumu na kufanya magonjwa kuwa sugu kwa dawa za kimagharibi, na wakati mwingine kutumia dawa hizo bila msingi wa kisayansi na kupoteza maana halisi ya dawa.

Kama hali hii itaendelea kuwepo, na kama hakutakuwa na uwekezaji makini na utafiti wa kutosha kwenye dawa za mitishamba na tiba mbadala, basi hali hii itaendelea kuwepo. Mara kwa mara tumekuwa tunakumbushwa na watawala wetu, kuwa kuna Tanzania tuna dosari ya kutojiamini.

Kuna baadhi ya mambo yako ndani ya uwezo wetu, lakini kutokana na kujitweza na kuthamini vya wengine tunaacha kufanya mambo tunayoweza ambayo yana manufaa kwetu.

Changamoto ya virusi vya corona imetukumbusha kuwa kama tungekuwa tumeipa msukumo wa kutosha sekta ya matibabu ya mitishamba na tiba mbadala, inawezekana kabisa kuwa tatizo la virusi vya corona lisingeleta taharuki kama lilivyofanya. Mwandishi wa makala haya ni mwanahabari wa Radio China International (RCI)- Swahili

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Fadhili Mponji, Beijing

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi