loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba yaanza kusheherekea ubingwa

SIMBA SC imewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuanza kusherekea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons unaotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya.

Kauli hiyo imekuja baada ya kikosi hicho kushinda mchezo uliopita kwa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City na kufikisha pointi 78, hivyo kubakisha mechi moja dhidi ya Tanzania Prisons kabla ya kutangaza ubingwa.

Simba inahitaji pointi mbili tu ili kutwaa ubingwa mara tatu. Simba kama watashinda mchezo huo dhidi ya Prisons watafikisha pointi 81, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, kwani Azam FC wanaoshika nafasi ya pili hata wakishinda michezo yote saba iliyobaki, watafikisha pointi 79.

Akizungumza Mbeya juzi, Kocha Msaidizi wa Simba, Suleman Matola licha ya kuwashukuru mashabiki wa timu kwa kutimiza wajibu wao na kufanikiwa kushinda mchezo huo dhidi ya Mbeya City, alifurahishwa na uwingi wa mashabiki waliojitekeza.

“Namshukuru Mungu kwa yote, lakini wachezaji pia kwa kutimiza kile wanachotakiwa, na binafasi nimefurahishwa na uwingi wa mashabiki waliojitokeza kutusapoti, pia nawaomba waendele kufanya hivyo mchezo unaokuja, kwani tutafanya hivyo ili tuanze kusherekea ubingwa wetu,” alisema.

Alisema wachezaji wake walifanya kazi kubwa hadi kupata ushindi, kwani mazingira ya uwanja huo sio rafiki, hivyo walilazimika kucheza kwa mfumo wasiouzoea ili kutafuta ushindi ikiwa ni maandalizi ya mchezo unaokuja.

Matola alisema ushindi huo walioupata, umekisaidia kikosi chake kupunguza idadi ya pointi wanazotakiwa kufikisha ili kutetea ubingwa huo na kukata tiketi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa upande wake, nahodha wa kikosi hicho, John Bocco aliyefunga mabao yote mawili kwenye mchezo huo alisema, kucheza kwa umoja na kujituma ndio kumewapata ushindi.

“Kucheza kwa umoja na kujituma kwa wachezaji wote ni mchango unaoendelea kujitokeza na naendelea kutoa wito kwa wachezaji wangu kuzidisha umoja hadi tufanikiwe kutetea ubingwa kwa mara nyingine,” alisema Bocco.

BAADA ya Namungo FC ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi