loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Digidigi anaongoza kwa uaminifu katika ‘ndoa’

“DIGIDIGI anapofiwa mume au mke; akabaki mjane, hubaki mjane hivyo hivyo na kuchukua muda mrefu akiwa anaishi peke yake. Kwa kweli mmoja anapokufa, anayebaki huwa na mtihani na kazi ngumu sana kupata na kujenga uhusiano mpya.”

Ndivyo anavyosema Ofisa Msimamizi wa Wanyamapori katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Gregory Mtega anapozungumzia maisha ya mnyama huyu mdogo zaidi katika kundi la wanyama jamii ya swala; digidigi anayepatikana pia katika Hifadhi ya Ngorongoro.

Hata hivyo Mtega anasema: “Mmoja kati ya baba au mama anayebaki mjane, baada ya kufiwa mwenza, huendelea na jukumu la kutunza mtoto kama walikuwa naye…”

Ofisa huyo anazidi kufahamisha akisema digidigi ni miongoni mwa wanyamapori wadogo jamii ya swala ambao ni kivuutio kikubwa japo hawajulikani sana kwa kuwa ni wachache tofauti na wanyama kama nyumbu na swala wengine ambao huishi katika makundi makubwa na huishi katika vichaka wakipatikana zaidi asubuhi sana na jionii hivyo, kutumia mchana kupumzika katika vichaka.

Hali hiyo imewafanya wasionekane wala kujulikana sana japo wana mikasa ya kuvutia na kusisimua. Wanapatikana Tanzania karibu katika mbuga na hifadhi zote ikiwamo Hifadhi ya Ngorongoro.

Anasema: “Sifa kubwa ya uadilifu waliyo nayo wanyamapori hawa ni kwamba, kama ni dume asiye na mke ama kwa kufiwa au kama hajawahi kupata mwenza, hutafuta himaya, lakini haingii kwa mwingine, bali hutafuta jike ambaye naye hana dume.”

Anaongeza: “Kama hajapata mwenza ambaye naye alikuwa pekee, bila jike au bila dume lake, basi atabaki hivyo hivyo katika maisha yake yote, lakini kamwe hawezi kwenda kuingilia mahusiano katika familia nyingine na katu, hawezi kupita katika himaya isiyo yake maana kila himaya inatambulika.” Kwa mujibu wa mtandao wa https://www.giraffecentre. org,

“Wapendanao hao huishi pamoja na kupata watoto, lakini ikitokea bahati mbaya mmoja amekufa kwa sababu yoyote iwayo, anayebaki huishi maisha ya msongo hata kukaribia kujiua; anaweza hata kujipeleka kwa makusudi kwa adui (muuaji) ili auawe na kuachana na upweke unaomkumba.”

Chanzo kimoja cha kimtandao kinaandika: “Jike ni mkubwa kidogo kuliko dume, lakini dume ana pembe fupi na nyembamba. Wana ushungi katika utosi unaoficha pengine pembe za dume.

Rangi yao ni ya mchanga, lakini mgongo una rangi ya majivu.” Kinaongeza: “Digidigi hula majani, matunda na beri. Wanapata maji ya kutosha kutoka katika chakula chao, hivyo hawana haja ya kunywa maji kila wakati hivyo huweza kustahimili kutokunywa maji kwa muda mrefu ikilinganisha na wanyamapori wengine wasio jamii ya swala.”

Mintarafu suala hili, Mtega anasema: “Digidigi wana uwezo mkubwa wa kutokunywa maji kwa muda mrefu kwa kuwa hupata maji hayo katika majani na mimea wanayokula yenye asili ya maji na pia hupenda kula wakati wa asubuhi ili wapate umande kutoka kwenye majani wanayokula, hivyo, hata kinyesi chao ni kikavu sana kwa kuwa mfumo wa miili yao kwa asili hukamua maji ili yatumike mwilini.”

Anasema: “Tabia hii ni kwa wanyamapori karibu wote wa jamii ya swala ndiyo maana hupenda kula asubuhi katika umande na jioni’ na muda mwingine wa mchana, huutumia kupumzika vichakani.”

MAISHA YA ‘NDOA’ NA FAMILIA

Vyanzo mbalimbali vinamwelezea mnyama huyo mla nyasi anayeishi katika vichaka vidogovidogo kuwa, tofauti na wanyama wengine wanaoishi katika makundi makubwa, wao huishi kifamilia pekee yaani bibi na bwana (dume na jike). Inaelezwa kuwa, kila digigidi jike na dume (familia) huanzisha himaya ya ukubwa wa kati ya ekari 12.5 hadi 75.

Ekari moja ni takribani ukubwa wa uwanja wa mpira wa miguu. Kila siku wanyama hawa wakiwa katika jozi ya bibi na bwana, hutembea pamoja katika himaya yao wakila majani, nyasi na matunda na katika vitu hivi, ndipo hupata maji.

Mtega anasema: “Daima digidigi hutembea wawili wawili isipokuwa kama wana mtoto, yaani, inapotokea wana mtoto, ndipo utawakuta wakiwa zaidi ya wawili na huishi katika mfumo wa umiliki ya himaya.”

“Mnyama huyu huzaa mtoto mmoja kila baada ya miezi sita na hunyonyesha kwa takriban miezi sita. Uzao wa digidigi hauna ukomo. Huzaa zaidi katika kipindi cha masika kwa kuwa kunakuwa na chakula cha kutosha.”

Anaongeza: “Kutokana na kuwa na tabia hiyo ya kuwa na himaya zisizoingiliana na pia kuzingatia maisha ya familia yao, digidigi wanamudu kuepuka migogoro baina yao wenyewe hivyo, wanyamapori hawa hawana migogoro ya kifamilia baina ya himaya moja na nyingine” Ofisa Msimamzi wa Wanyamapori huyo anasema:

“Kwa asili yao, wanyama hawa huishi maisha ya mke mmoja na mume mmoja yaani, ni waaminifu sana katika mahusiano yao, (monogamous) kwa wanyamapori hawa ni tofauti na wengine hawa huwa na mahusiano ya kudumu kati ya jike na dume kwa muda wote wa maisha yao na madume hulinda sana wake zao.”

Anasema: “Mtoto wa digidigi hukaa na wazazi wake hadi anapofukuzwa na wazazi wake yapata miezi saba hivi jike anapozaa mtoto mwingine,” anasema. Chanzo kimoja cha kimtandao kimeandika:

“Digidigi jike na dume (familia) hutumia takriban asilimia 65 ya muda wao wakiwa pamoja. Mtindo huu wa maisha huwaondoa katika hatari nyingi zinazoweza kuwakumba kama wangezagaazagaa kutafuta uhusiano mwingine.” Kinaongeza: “… Mtoto wa digidigi hufukuzwa kutoka katika himaya ya wazazi wake anapofikisha umri wa kujitegemea ambao ni umri wa takriban miezi saba ambao mara nyingi hukutana na mimba ya uzao mwingine wa mama.”

“Digidigi jike ndiye humfukuza ‘binti’ nyumbani huku digidigi dume akiwajibika kumfukuza ‘kijana wa kiume’ aliyetimiza umri wa kutoka nyumbani.”

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, kwa wanyama hawa, kijana akitimiza umri huo sahihi, anaweza kukutana na kijana mwenzake au mjane na kuanza uhusiano wa kifamilia.

MAADUI WA DIGIDIGI

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, mnyama huyu anao maadui wengi wakubwa hasa wanyama walao nyama kama vile chui, mbwa mwitu, mbweha, fisi, simbimanga, simba, mamba na chatu bila kuwasahau binadamu.

Mara nyingi watoto wa digidigi pia huchukuliwa na mwewe au nyani.

Wanapokumbana na tishio la maisha, digidigi hutoa ishara kwa kutumia pua zinazotoa mlio wa “zik-zik” au “dik-dik,” na kutimua mbio kwa mtindo wa zigi-zaga kwa kasi ya takriban kilomita 40 kwa saa.

Wanapofika penye bonde au shimo, huingia na kujificha. Kama sungura, digidigi nao hupenda kujificha kuliko kukimbia dhidi ya hatari inayowakabili.

HIMAYA INAVYOPATIKANA

Wanyama hawa wana alama nyeusi katika kona ya kila jicho zinazowasaidia kutoa ute unaotumika kuweka alama za himaya anayoishi.

Alama hiyo chini ya jicho hutoa alama zinazotumika kuweka alama nyeusi katika vimti vidogo ute mweusi ambao hutumika kutofautisha umiliki wa himaya zao Hata hivyo, kwa nadra sana, tena sana, inaweza kutokea digidigi mmoja akapoteza mwenza na kubaki mjane sasa katika harakati za kumtafuta akiwa na msongo, au ndama ambaye hajawa na familia anaweza kujikuta ameingia katika himaya ya mwingine, au wakati wa kiangazi katika kutafuta chakula, akajikuta ameingia.

Anapobainika, au kushituka, hutoka haraka. Lakini hii haitokei sana.”

Kwa mujibu wa Mtega, digidigi hutumia ute kuweka alama katika himaya na kutambua himaya isiyo yake maana kila moja inatambulika. Jina la kisayansi la wanyama hawa digidigi (dik-dik) ni Madoqua Kirk.’

Kwa wastani huishi kwa miaka kumi. Uzito wao ni kati ya kilogramu tatu hadi sita. Kwa umbo, jike ni mkubwa kuliko dume. Urefu hadi begani ni sentimeta kati ya 30 hadi 40 na urefu wa umbai ni kati ya sentimeta 50 na 70.

Kwa mujibu wa Ofisa Msimamizi wa Wanyamapori katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), wanaotaka kuona na kujua mambo mengi kuhusu wanyama waiwamo wale maarufu na wengine maarufu, lakini wasiojulikana kama digidigi, pofu, nyegere na fisi, wafike na kutembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili wafaidi vivutio hivyo na vingine vya asili na kiutamaduni.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi