loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga, Azam FC mtegoni

SIMBA huenda leo wakatangazwa mabingwa bila ya kushuka uwanjani, endapo Yanga na Azam FC watapoteza mechi zao za mzunguko wa 32 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam wanaoshika nafasi ya pili, wenyewe wana pointi 58 na Yanga wana pointi 57 na kama wote watapokea vichapo, basi hata wakishinda mechi zao zilizobaki baada ya mchezo wa leo zitakuwa sita, watafikisha pointi 76 na 75 wakati Simba tayari wana 78 hadi sasa.

Hivyo, Simba anayetarajia kucheza kesho dhidi ya Tanzania Prisons, atatangazwa bingwa kabla ya mchezo huo na kuwa kama Liverpool ya England, ambao juzi walitwaa ubingwa bila ya kushuka uwanjani baada ya Man City kufungwa na Chelsea 2-1.

Endapo timu hizo zitashinda au kutoka sare, Yanga dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Azam watakuwa ugenini wakicheza dhidi ya Biashara United ya Musoma, Simba itabidi kusubiri hadi kesho itakapocheza dhidi ya Tanzania Prisons Mbeya, na kama itashinda itatangaza ubingwa.

Aidha, mvutano mkubwa uko katika nafasi ya pili, timu tatu zinazofuatana za Azam, Yanga na Namungo zinawania nafasi hiyo huku zikiwa zimepishana kwa pointi chache.

Namungo wenye pointi 55, ambao Jumatano walitoka sare na Yanga, leo watakuwa wageni wa Ruvu Shooting katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.

Timu hizo tatu kila mmoja anamuombea mwenzake apoteze na yeye ashinde. Kwa maana atakayeteleza na mwingine akashinda, basi yupo atakayempisha mwenzake juu na mwingine kushuka, zitapishana katika nafasi walizopo.

Yanga na Ndanda zina historia ya kukamiana kila zinapokutana. Haijalishi nani yuko nyumbani mara nyingi mechi zao zinakuwa ngumu. Katika mechi tisa walizowahi kukutana, Yanga imeshinda tano na kupata sare nne.

Zinakutana Yanga ikitoka kupata sare tatu mfululizo dhidi ya JKT bao 1-1, dhidi ya Azam FC 0-0 na dhidi ya Namungo 2-2. Bila shaka watakuwa kwenye presha ya kutaka matokeo mazuri.

Itaendelea kukosa huduma za wachezaji wake wawili, Bernard Morrison na Lamine Moro wanaotumikia adhabu ya kufungiwa. Kwa upande wa Ndanda inashika nafasi ya 15 kwa pointi 35.

Wanahitaji matokeo mazuri ili wasiendelee kushuka chini na kuingia hatarini. Katika michezo mitatu iliyopita wamepata suluhu dhidi ya Ruvu, wameshinda mmoja dhidi ya Biashara United 1-0 na kupoteza mmoja dhidi ya Polisi Tanzania, walifungwa 1-0.

Katika mechi ya Azam FC dhidi ya Biashara haitakuwa nyepesi kutokana na umuhimu wa kulinda nafasi waliyopo. Wametoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar bao 1-0.

Iwapo watapoteza tena na wenzake wakashinda wanaweza kuporomoka kidogo. Wapinzani wao Biashara hawako vibaya sana wanashika nafasi ya tisa kwa pointi 43.

Wametoka kushinda mchezo wao uliopita dhidi ya KMC mabao 4-0. Lakini takwimu zinaibeba Azam FC kwani katika michezo mitatu waliyowahi kukutana ameshinda mbili na kupata sare moja. Je, ataendeleza rekodi hiyo? Mchezo mwingine ni Ruvu Shooting dhidi ya Namungo.

Ni mchezo muhimu kwa kila mmoja, Namungo inayopigania nafasi ya pili lakini pia Ruvu inayotaka nafasi za juu kubaki salama. Mara ya mwisho timu hizi kukutana mzunguko wa kwanza, Namungo ilishinda mabao 2-1. Ruvu inashika nafasi ya 11 kwa pointi 41 ni wazi wanahitaji matokeo kuendelea kujiimarisha katika nafasi za juu.

Ruvu haijafanya vizuri katika mechi tatu zilizopita baada ya kupata sare mbili na kupoteza mchezo mmoja, huku Namungo ikipata sare mbili na kushinda mchezo mmoja.

Kwa upande wa Kagera Sugar inayoshika nafasi ya nane kwa pointi 44, huenda ikaendeleza ubora wake kwenye uwanja wa nyumbani kwa kuhakikisha inaifunga KMC inayoshika nafasi ya 14 kwa pointi 36. Timu hiyo imetoka kushinda mchezo uliopita dhidi ya Azam bao 1-0, huku wageni wao KMC wakitoka kupoteza mchezo wa ugenini mabao 4-0 dhidi ya Biashara.

Ni mchezo mgumu hasa kwa KMC ambayo inapambana kujiondoa chini ili ipande juu iwapo itakubali kipigo kingine basi inaweza kushuka chini kama wenzake wanaomfuatia watashinda. Mtibwa baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya Singida United mabao 3-1 bado hapaswi kuridhika wanahitaji ushindi ili kujiimarisha zaidi juu.

Wanafuatana na Mwadui kwa pointi sawa 37 nao pia wanahitaji ushindi. Timu nyingine zilizoko hatarini zinazohitaji matokeo ni Mbeya City itakayocheza dhidi ya JKT, Singida United dhidi ya Lipuli na Alliance dhidi ya Coastal Union.

Ukitoa timu mbili hapo, ambazo ni JKT na Coastal zilizoko nafasi ya tano na sita kwa pointi 48 kwa 47 wengine wana kibarua kizito cha kuhakikisha wanapambana kufa au kupona, la sivyo, wataendelea kushika mkia.

BAADA ya Namungo FC ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi