loader
Msomi UDSM alivyotimiza azma kusaidia wanawake, watoto

Msomi UDSM alivyotimiza azma kusaidia wanawake, watoto

KARIBIA kila mradi chanzo chake hutokana na kitu ambacho mwanzilishi wake amekipitia na kukifanyia kazi baada ya kujifunza katika mapito yake na kumsukuma kuanzisha wazo la kuanzisha mradi husika.

Mfano mzuri hasa ni miradi ya kijamii ambapo waanzilishi hutumia ujuzi wa waliyopitia au waliyojifunza kwenye kazi hapo ndipo hupata maono ya kuanzisha mradi wa kusaidia jamii dhidi ya jambo fulani.

Hivi ndivyo ambavyo mwanadada Irene Fugara, Mkurugenzi wa Shirika la Bright Future Initiative alivyoanzisha shirika lake lililolenga kuwakinga watoto na wanawake dhidi ya unyanyasaji katika jamii.

Shirika hilo hadi sasa likiwa na mwaka mmoja na nusu tangu kuanzishwa kwake limeshawafikia watoto 4,000 kutoka mikoa minne huku wanawake waliofikiwa ni 1300.

Mikoa iliyonufaika ni pamoja na Iringa, Mbeya, Dodoma na Kagera pamoja na baadhi ya shule za Dar es Salaam. Wazo la dada huyu kuanzisha shirika hilo lilitiliwa mkazo wakati akiwa kikazi nchini Marekani, alienda kushiriki mradi wa kumjengea uwezo wake kwenye kazi.

Irene ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, akijikita zaidi katika masomo ya sheria, wakati akipata maono ya kubadilisha maisha ya wanawake na kuwakinga watoto dhidi ya unyanyasaji alikuwa akifanya kazi kwenye Chama cha Wanasheria wa Mazingira.

Akiwa kwenye chama hicho alijikuta akifanya kazi kwa ukaribu zaidi na Chama cha Wanasheria Wanawake Nchini (Tawla).

Anasema alijiunga na chama hicho huku akifanya kazi za miradi kama mwanasheria na alikuwa mwanasheria kijana zaidi. Irene anasema alipewa kazi ya kufuatilia namna ambavyo rangi ya nyumba zinawaathiri watoto ambapo utafiti wake huo ulibainisha madhara mengi yanayotokana na rangi hizo na anaongeza kuwa alikuja kubaini kuwa wapo watoto ambao wakiathiriwa na rangi hizo wanathirika moja kwa moja kisaikolojia na kujikuta wanakuwa watoto watukutu zaidi.

Anabainisha kuwa aliona pia ni kwa kiasi gani suala hilo linaathiri makuzi ya watoto hao kwa kuwa wengi wao wanaishia kupigwa na wakichukuliwa ni kama watoto wakaidi kumbe sio akili yao. Irene anasema akiwa anaendelea na kazi zake akatumwa kushiriki mradi wa Tawla uliokuwa ukihusiana na kupigania haki za wanawake na matumizi ya ardhi.

Anaongeza kuwa mradi huo ulimfungua macho kuona ni kwa kiasi gani wanawake wanapaswa kusikilizwa hasa katika ushirikishwaji wa matumizi bora ya ardhi na kuwa wanawake wapo ambao walikuwa wakikosa mahala pa kulima wala kuchota maji kwa kuwa ardhi imechukuliwa na mwekezaji.

“Hapo nilianza kuona namna ambavyo hawa wamama wetu wanavyotakiwa kusikilizwa na kusaidiwa kwani walikuwa wakikosa haki zao za msingi, wapo ambao walikuwa hawana mahali pa kutolea mawazo yao juu ya nini kifanyike waendelee kunufaika na ardhi…hapa nikakumbuka kuwa lengo langu la kusomea sheria ni kusaidia kuchangia katika jamii kwa maana ya kushiriki kufanya kazi za kuimarisha utu,” anasema.

Irene anasema kuna wakati alikuwa akilala usiku sauti za wanawake aliozungumza nao huku wakionesha imani kubwa kwake na sauti hizo zimekuwa zikijirudia masikioni mwao huku akiona kuwa kuna kitu kikubwa zaidi cha kuwafanyia wanawake.

Lakini wakati huo huo alikuwa akiingiwa na mawazo ya kusaidia watoto ambao aliona wanaathiriwa na rangi za ndani ya nyumba.

Aenda Marekani kujinoa

Akiwa anaendelea na kazi zake kama kawaida kuna siku aliitwa na bosi wake katika chama hicho cha mazingira na kuambiwa kuwa anatakiwa kwenda nchini Marekani katika jiji la Washington katika Taasisi ya Word Resource.

Anasema aliambiwa kuwa anaonekana kufanya kazi vema zaidi na hivyo anatakiwa kwenda kuongeza maarifa kutokana na uwezo wake katika kushughulikia masuala ya ardhi.

Mwanadada huyu anasema akiwa Marekani akiendelea na mafunzo kuna siku aliitwa na waratibu wa mafunzo hayo na kumtaka azungumzie namna ambavyo wanawake hapa nchini wanakosa kushirikishwa kikamilifu katika masuala ya ardhi.

Anasema kwake ilikuwa ni fursa ya kuzizungumzia kero za ardhi kwa wanawake huku akiwa na imani kuwa atasaidia kitu lakini wakati huo akiwa na uoga kidogo kutokana na ukubwa wa mkutano wenyewe.

“Ulikuwa ni mkutano wa haki za wanawake katika ardhi lakini uliandaliwa na Benki ya Dunia, kwa kuwa nilikuwa ninahusika na masuala ya ardhi kwa wanawake hapa nchini, waratibu wa masomo wakanichagua mimi kuzungumzia uzoefu wangu,”anabainisha.

Anasema akaona hapo ndipo mahala pa kumaliza kiu yake ya kuwasaidia wanawake huku akijipanga kuhakikisha analeta tija kwa wanawake na ardhi nchini. Irene anaongeza kuwa alizungumza mengi kuhusiana na nafasi za wanawake wa Tanzania katika ardhi, nafasi ya ardhi katika kumkomboa mwanamke kiuchumi na mengine mengi zaidi yakiwemo mapungufu ya kisheria katika kumsaidia mwanamke kunufaika na ardhi.

Anaongeza kuwa baada ya kumalizika kwa mkutano huo alipata maoni mengi hadi kufikia hatua ya kupata fedha za kusaidia mradi wa haki ardhi wa Tawla.

Anasema zikiwa zimebakia siku chache kurejea nchini alipigiwa simu na bosi wake kutoka hapa nchini akimtaarifu kuwa amepewa nafasi ya kwenda jimbo la Oregon.

Irene anabaisha akiwa jimboni humo alikutana na mradi wa kuwasaidia watoto kujiepusha na madhara mbalimbali katika jamii na kati ya aliowakuta ni pamoja na mradi wa kuwaepusha watoto dhidi ya madhara ya rangi pia, hivyo akakumbuka yale aliyojifunza akiwa nyumbani.

Hapo sasa akaliona wazo lake la kuwa mtu wa kusaidia wanawake na watoto likimrejea tena na tena na akafanya maamuzi kuwa asiwe tu mshiriki wa mafunzo tu katika jimbo hilo ila sasa aone nini cha kuiga.

Irene anasema alimaliza muda wake Marekani na akarejea hapa nchini lakini safari hii alikuwa na kiu ya kutimiza mambo mawili kwake moja ni kuwasaidia wanawake kwa kuwa sauti yao na pili ni kuwakinga watoto.

Alirejea kwenye chama hicho na kufanya kazi hadi mkataba wake ulipokwisha, sasa akawa na wazo la kuanzisha shirika lake lakini tena akapata mwaliko kutoka kwa rafiki yake aitwaye George Ndaisaba wa Shirika la People Development Forum, alifanya kazi kuanzia Juni 2017 hadi Desemba 2018.

Anasema hapo alienda kufanya kazi ili kujua ni kwa kiasi gani anaweza kujipanga na kuimarisha shirika lake sasa, alifanya kazi tangu mwaka 2017 hadi 2018 muda huo alishafungua shirika lake lakini halikuwa likifanya kazi rasmi. Irene anasema alipoona amejifunza mengi sasa akatoka rasmi huku akisaidiwa kimawazo na rafiki yake huyo njia bora za kufanya kazi zakujitolea na kuwa na nidhamu ya kazi.

Alivyoanza shirika lake Anasema alikuwa akiweka katiba na taarifa zote muhimu za shirika lake katika begi tena katika buti la gari, huku akiwasiliana na marafiki zake na kisha kwenda kutoa elimu kwa watu aliowalenga.

Irene anasema kuna siku aliandika ombi la fedha kwenda shirika linalosaidia mashirika madogo, Azaki za Kiraia, ombi lilikubaliwa isipokuwa watendaji walikuwa wakitaka kumjua zaidi kwa kufika ofisini kwake.

Alilazimika kutafuta ofisi ya muda kwa lengo la wahusika washirika hilo waone akiwa ofisini, lakini hapo ndipo akajikuta akipata fedha za kukodisha ofisi kwa ujumla. Alipewa fedha za awali na kuanza kazi.

Kwa kuwa alionesha nia ya kuanzisha mradi wa kuwakinga watoto dhidi ya matatizo mbalimbali akaamua kuwakinga dhidi ya changamoto za udhalilishwaji kutoka katika jamii, huku wanawake alinuia kuwakinga dhidi ya unyanyasaji wa kingono hata kimwili katika maeneo yao ya kazi.

Bright Jamii Initiative inavyofanya kazi Shirika hilo limekuwa likishirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na watoto hasa katika kuwafikia wanawake kwenye viwanda kwa kuimarisha mfumo wa utoaji wa taarifa za unyanyasaji.

Anasema wanawake wanaombwa rushwa za ngono ili kupata ajira viwandani au kuongezewa mikataba ya ajira waliyonayo na anaongeza kuwa wamewafikia wanawake 1,300 kupitia vyama vya wafanyakazi mbalimbali ambavyo vimeshiriki kuwajengea uwezo wanawake kwa kuzungumzia haki zao.

“Niliamua kuanza na wanawake viwandani hasa Dar es Salaam tumeshiriki kuweka mifumo ya utoaji taarifa, usikilizwaji wa kesi za ajira pia tumechagiza kuharakishwa kwa kesi hizo sehemu mbalimbali za haki kazini,” anasema mwanadada huyo.

Amejikuta akirejea kufanya kazi na taasisi alizokuwa akifanya kazi awali akitokea kwenye shirika lake, katika kupigania haki za wanawake hao.

Anasema kwa upande wa watoto hushirikiana pia na walimu kufanya sanaa zenye kuwaelimisha watoto dhidi ya udhalimu wanaofanyiwa, pia wana mbinu za kuwawezesha watoto kujitambua hasa kwa kuimarisha fikra zao.

Anabainisha kuwa anaamini kuwa watoto wanapaswa kusikilizwa kabla ya kuadhibiwa kwa kufanya hivyo inawajenga ubongo wao zaidi na kuwa watu wenye uwezo wa kuepuka mabaya.

Anasema wanatumia pia klabu za watoto na kuwataka wadau wengine wakiwemo wazazi au walezi kufuatilia na kujifunza mambo mbalimbali kupitia mitandao yao ya kijamii ya @bjinitiative katika Twitter, Instagram na tovuti ya bjinitiative.org. Irene anasema ameona kupata furaha ya moyo sasa kwa kuwa ameanza kutimiza ndoto ya malengo yake ya kusaidia wanawake na watoto kwa namna yoyote ile.

Mwanadada huyu anapenda kusoma hasa mambo yatakayomjengea uwezo wa kuihudumia jamii, kiu yake kubwa ni kuzungumza na kubadilisha mtazamo wa jamii. Irene ambaye alisoma elimu ya msingi na sekondari katika shule ya Wasichana ya Barbro Johanson amekuwa mshabiki mkubwa wa Mbunge wa Muleba, Mama Anna Tibaijuka.

Anasema akiwa kidato cha pili shuleni hapo alimuona siku moja mwanamama huyo akiingia na kuwagombeza wanafunzi wa kushindwa kufanya vema somo la hisabati.

Irene anasema aliwaambia kuwa wanaweza kufaulu kama wanavyofaulu wavulana, kauli hiyo ilimfanya ajipange na kuhakikisha akifika kidato cha tano anafaulu kwa kiwango kikubwa, akaja kupata daraja la kwanza huku somo la hisabati akipata daraja la kwanza.

Alishukuru ujio wa mama huyo kwa kuwa ulimjengea hali ya kujiamini na kuona kuwa atakuja kuwa mtu wa kubadilisha maisha ya watu wengine huku akiwa na shauku ya siku moja kuja kuwa kama mama huyo.

Akiwa hayupo katika shughuli zake za kusaidia jamii, Irene hupenda kusoma vitabu vyenye mafunzo mbalimbali na kwa mwezi lazi ajue kitu kipya, hupenda kuongeza wigo wa marafiki hasa wenye mawazo mapya, kujifunza zaidi na husafiri mara kwa mara kufuata ujuzi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/51f59af4b12c703f444729aba7e268f9.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi