loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba bingwa 2019/2020

SIMBA SC imetetea kwa mara ya tatu mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kutoka suluhu dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya jana.

Vinara hao wamefikisha jumla ya pointi 79, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, wakati Prisons wenyewe wamefikisha pointi 43 na kubaki katika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi hiyo, baada ya wote kushuka dimbani mara 32.

Wekundu hao wamechukua ubingwa huo huku wakisaliwa na michezo sita mkononi ili kuhitimisha ratiba ya michezo ya ligi hiyo kwa msimu wa mwaka 2019/2020.

Tangu msimu wa mwaka 2017/2018, Simba wametwaa ubingwa kwenye viwanja vya ugenini, na sasa wameifikia rekodi ya Yanga ya kulitwaa taji hilo mara tatu mfululizo.

Misimu miwili iliyopita mwaka 2017/2018 na 2018/2019, Simba walitwaa taji hilo mbele ya Singida United mechi zote zikifanyika kwenye Uwanja wa Namfua (sasa Liti) mjini Singida.

Kwa kulitwaa taji hilo, Simba sasa italiwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, huku ikiacha mchuano mkali wa kuwania nafasi ya pili uliopo kati ya Yanga, Azam na Namungo FC zilizopo katika nafasi ya pili, ya tatu na ya nne kwa sasa.

Mchezo wa jana kati ya Mabingwa wapya na Prisons ulianza kwa kasi ,kwa maafande hao ambao walikuwa wenyeji wa mechi hiyo kucheza kwa kasi wakiwa wamedhamiria kupata ushindi, lakini kila muda ulipokwenda walionekana kuridhika na matokeo ya sare, wakipoteza muda mara nyingi.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abubakar Mturo aliyesaidiwa na Janeth Balama na Paschal Joseph, timu hizo zilishambuliana kwa zamu huku makipa, Aishi Manula wa Simba na Jeremiah Kasubi wa Tanzania Prisons wakiwa na kazi kubwa ya kuokoa michomo.

Hilo ni taji la 21 la Ligi Kuu kwa Simba, huku watani zao Yanga wakiwa mabingwa wa kihistoria kwa kulibeba mara 26.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo jana, Mbao FC iliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku bao hilo pekee likifungwa na Waziri Junior katika dakika ya 65.

Singida United ni kama imeshuka na sasa inasubiri kukamilisha ratiba baada ya kuendelea kuwa mkiani wakiwa na pointi zao 15 na hata kama watashinda mechi zao sita zilizobaki, watafikisha poinri 33, ambazo zimefikiwa na Mbeya City iliyopo katika nafasi ya 18.

Kikosi cha Prisons: Jeremiah Kisubi, Michael Ismail, Benjamin Asukile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya/Ismail Azizi (dk 61), Ezekia Mwashilindi, Samson Mbangula, Jeremiah Juma na Adil Buha.

Simba: Aishi Manula, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Gerson Fraga, Hassan Dilunga/Luis Miquissone (dk 67), Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Clatous Chama (dk 46) na Miraji Athumani ‘Madenge’/John Bocco (dk 80).

MWIGIZAJI maarufu wa tamthilia ya Karma, Wema Sepetu amewaomba radhi ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi