loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ufaransa yaisifu Tanzania, yaikopesha bil 593/-

SERIKALI ya Ufaransa imeisifu Serikali ya Tanzania kwa namna inavyotekeleza miradi ya maendeleo inayogusa jamii na kuimarika kiuchumi kwa kasi huku ikiahidi itakuwa nayo bega kwa bega kuhakikisha inafikia katika uchumi wa kati mwaka 2025.

Ufaransa pia imeeleza mafanikio na hatma yake imebebwa na Afrika na wameichagua Tanzania kwao kuwa si tu mshirika wa maendeleo bali rafiki wa kweli katika nyanja zote za uchumi, ulinzi na usalama na hilo linachagizwa na amani, utulivu na usimamizi mzuri wa miradi unaofanywa na serikali.

Kuthibitisha hilo, jana Ubalozi wa Ufaransa na shirika lao la Maendeleo (AFD) ulisaini mikataba mitatu ya makubaliano na Tanzania ya mkopo wa masharti nafuu ya Sh bilioni 592.57 (Euro milioni 230) ili kutekeleza miradi mikubwa mitatu ya maji Ziwa Victoria, nishati ya umeme vijijini na kuunganisha umeme kati ya Tanzania na Zambia.

Mikataba hiyo ilisainiwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, na kwa Ufaransa waliosaini ni Balozi Frederic Clavier na Mkurugenzi Mkazi wa AFD nchini, Stephanie Essombe.

Ulishuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Zena Said na watendaji wa taasisi zinazosimamia maji na nishati ikiwamo Shirika la Umeme (Tanesco), Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa).

Akizungumza katika hafla hiyo baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Balozi Clavier aliielezea Tanzania kama taifa kubwa na kitovu cha ustawi na moyo wa ukanda wa Afrika mashariki na kusini ambayo Ufaransa inajisikia si tu mshirika wake wa maendeleo, bali rafiki wa karibu aliyebeba hatma yake.

Balozi Clavier alisema Ufaransa inaguswa namna Tanzania inavyotekeleza miradi inayogusa jamii moja kwa moja ikiwamo maji, nishati na elimu chini ya uongozi thabiti wa Rais John Magufuli na kuahidi kuwa itahakikisha dhima yake ya kufikia uchumi wa kati mwaka 2025 inafikiwa.

“Ufaransa inajisikia Tanzania kama nyumbani. Nchi hizi mbili zimejenga uhusiano imara unaodhihirishwa hata na tukio hili la kusaini mkataba wa kutekeleza miradi hii mitatu muhimu. Ufaransa ina mchango mkubwa kwa Tanzania kufikia uchumi wa kati 2025 na hatuna mashaka kwamba itafika. “Tanzania ni nchi kuu na moyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ina mchango mkubwa kwa kanda hizi. Ni nchi ya mfano katika maendeleo ya nishati, elimu na usafirishaji. Tuna imani na hatma yetu tunaposhirikiana na Tanzania hasa kutokana na amani na utulivu kwani bila amani, hakuna kinachofanyika,” alisema Balozi Clavier. Alisema nchi yake imejikita kushirikiana na Tanzania kwenye miradi ya maendeleo kutokana imani walionayo namna fedha wanazotoa zinavyotumika vizuri na kuahidi kuendelea kutoa fedha ili kushiriki kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa masuala mbali mbali kwani mafanikio ya Ufaransa yamebebwa na Afrika, Tanzania ikiwemo. “Nimeishawishi nchi yangu ifanye kazi na Tanzania kwa sababu ni nchi makini na imara katika kusimamia masuala ya uchumi, amani na utulivu,” alisema huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo na kuhamasisha kampuni nyingi za Tanzania ziende kuwekeza Ufaransa kama zilivyo za nchi hiyo nchini. Alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya kwenye miradi inayotekelezwa vijijini inayosaidia kupunguza uhamaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini kwa kuwa sasa vijiji vingi vina umeme, maji safi, usafi wa mazingira, shule, vituo vya afya na miundombinu bora ya usafirishaji. Naye Mkurugenzi Mkazi wa AFD alisema wataendelea kushirikiana na Tanzania kuwezesha miradi ya nishati na maji ili kuimarisha huduma za jamii, na kuwa pamoja na uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 600 katika sekta ya maji, wana imani mwaka ujao utakuwa wa utekelezaji wa miradi mingine ya mikopo ya masharti nafuu katika sekta nyingine ikiwamo kilimo. Katibu Mkuu Hazina, Dotto James alisema mikataba hiyo ya mikopo ya masharti nafuu ya jumla ya Euro milioni 230 sawa na Sh bilioni 592.57 ni kwa ajili ya miradi mitatu ya kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Aliitaja miradi hiyo kuwa ni wa Usambazaji wa Umeme Vijijini, Awamu ya Pili unaogharimu Sh bilioni 257.64 (Euro milioni 100) utakaosambazwa katika mikoa 16 ya Tanzania Bara; Mradi wa Umeme wa Kuunganisha Tanzania na Zambia unaogharimu Sh bilioni 257.64 (Euro milioni 100) na wa Kazi za Nyongeza kwenye Mradi wa Maji Safi na Maji Taka kwa miji inayozunguka Ziwa Victoria wa Sh bilioni 77.29 (Euro milioni 30). Katibu Mkuu huyo alisema miradi hiyo mitatu inawiana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inayoongoza juhudi za maendeleo na inayotekelezwa kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) wa Mwaka 2016/17 na 2020/21.

MBUNGE wa Mbeya mjini Dk Tulia ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi